Wednesday, July 15, 2015

TFF YAUNDA KAMATI YA USHAURI YA LIGI

RAIS wa Shirikiso la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Jamal Malinzi ameteua Kamati ya ushauri ya Ligi Kuu (VPL) na ligi Daraja la Kwanza (FDL) nchini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Alhaj Ahmed Mgoyi na katibu wa Kamati ni mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi nchini (TPLB) na wajumbe wengine saba.

1. Alhaji Ahmed Idd Mgoyi (Mwenyekiti)
2. Boniface Wambura (Katibu)
3. Kennedy Mwaisabula- Mjumbe
4. Idd Mshangama- Mjumbe
5. Amiri Mhando- Mjumbe
6. Grace Hoka- Mjumbe
7. Ibrahim Kaude (Vodacom)- Mjumbe
8. Baruan Muhuza (Azam Media)- Mjumbe
9. Peter Simon- Mjumbe

Kazi za kamati hiyo zitakua ni:
(i) Kufuatilia mwenendo wa Ligi
(ii) Kuishauri Bodi/TFF namna ya kuboresha Ligi
(iii) Masoko
(iv)  Leseni za Vilabu (Club Licensing)
(v)  Mipango ya Maendeleo ya Vilabu
(vi) Viwanja vya mazoezi
(vii) Utoaji wa tuzo za ligi mbalimbali
(viii) Kutengeneza vigezo (criteria) vya washindi wa tuzo


CECAFA KUENDESHA MTIHANI WA UTIMAMU WA MWILI KESHO
Baraza la Vyama Vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kesho Alhamis tarehe 16 Julai, 2015 litaendesha mtihani wa utimamu wa mwili (Pysical test) kwa waamuzi wa watakochezesha michuano ya kombe la Kagame inayoanza mwishoni mwa wiki huu.

Zoezi hilo la utimamu kwa waamuzi watakochezesha mashindano ya Kagame, litafanyika kuanzia saa 2 asubuhi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam litasimamiwa na kamati ya waamuzi yay a CECAFA.

Waamuzi wanaotarajiwa kuhudhuria zoezi hilo ni Ali Ahmed, Suleiman Bashir (Somalia), Ahmed Djama (Djibout), Yetayew Belachew (Ethiopia), Kakunze Herve (Burundi), Davis Omweno, Peter Sabata (Kenya), Issa Kagabo, Hakizimana Louis (Rwanda), Ahemd El Faith (Sudan), Lee Okelo na Mashood Ssali (Uganda), Israel Mjuni na Ferdinand Chacha (Tanzania).


AL SHANDY, MALAKIA, KMKM KUWASILI KESHO
Timu ya Al Shandy kutoka nchini Sudan, Al Malakia kutoka Sudan Kusini na KMKM kutoka Visiwani Zanzibar zinatarajiwa kuwasili kesho jijini Dar es salaam tayari kwa ushiriki wao kwenye michuano ya kombe la Kagame.

Al Shandy wanatarajiwa kuwasili kesho Alhamisi saa 3 kamili asubuhi kwa usafiri wa shirika la Ndega la Kenya (KQ), KMKM wakitarajiwa kuwasili majiraa ya saa 5 kamili asubuhi kwa boti ya Kilimanjaro, na Al Malakia wakitarajiwa kuwasili saa 10 jioni kwa ndege ya Rwanda Air.

Viwanja vya mazoezi vitakavyotumika kwa timu zinazoshiriki michuano ha Kagame ni Chuo cha Ualimu (Duce), TCC – Chang’ombe, Sekondari ya Loyola, Bora Kijitonyama, Polisi Kurasini, Chamazi, Uwanja wa Uhuru.

Timu 11 zitafikia katika hoteli za Durban (Mnazi Mmoja), Chichi (Kinondoni) Ndekha, Grand Villa, Travertine (Magomeni), wakati wenyeji Azam na Yanga watakua na kambi zao kwa ajili ya mashindano hayo.


Wasifu wa Al Khartoum:
Al Khartoum ni kati ya wawakilishi wawili wa Sudan kwenye kombe la Kagame. Al Khartoum ni kiboko ya vigogo  katika Ligi ya Sudan kutokana na kutoa upinzani mkali katika ligi ya nchi hiyo inayozijumuisha timu za Al Hilal, El Merreikh na Al Shandy.

Wachezaji wa kuangaliwa:
Mshambuliaji Ismail Baba ambaye ni mchezaji wa zamani wa Coton Sports ya nchini kwao, Kameruni anategemewa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hii kutoka jiji la Khartoum.

Kiungo mshambuliaji, Dominic Aboy, raia wa Sudani Kusini anategemewa kuonesha ufundi katikati ya dimba. Salah Al Amini ni mchezaji mwingine wa kutupiwa jicho.

Benchi la ufundi:
Katika kujaribu kufurukuta kutoka kwenye ubabe wa timu mbili maarufu za Sudan, Al Merriekh na Al Hilal, wawakilishi hawa wa Sudani walivuka mipaka na kumuajiri kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Ghana, Kwesi Appiah.

Huu utakuwa mtihani wa pili mkubwa kwa kocha Kwesi Appiah baada ya kushindwa kufurukuta kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho mbele ya Power Dynamos ya Zambia.

Kundi ililopo:
Al Khartoum iko kwenye kundi A la michuano ya kombe la Kagame kwa mwaka huu ikijumuishwa pamoja na Yanga, Gor Mahia ya Kenya, KMKM ya Zanzibar na Telecom ya Djibout.

Bila shaka ni kundi gumu kwenye michuano ya mwaka huu.

Rekodi kombe la Kagame:
Al Khartoum ni wageni wa mashindano haya. Rekodi ya kubwa nje ya Sudan, ni kufanikiwa kufika kwenye hatua ya kumi na sita bora ya mashindano ya Kombe la shirikisho la CAF mnamo mwaka 2011.

Wasifu wa KMKM
Klabu ya KMKM  itawaiwakilisha Tanzania kwa upande wa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Jumamosi kwenye viwanja vya Taifa na ule wa Karume.

Historia ya KMKM kwenye Kombe la Kagame:
Imeshiriki mara kadhaa bila kushinda taji hili. Ushiriki wao  haukuwa mzuri kwenye michuano ya mwaka jana iliyofanyika jijini Kigali, Rwanda.

Hata hivyo, KMKM wameonesha nia ya kufanya vizuri mwaka huu kwa kufanya maandalizi mapema.

Tayari wamecheza mechi tatu mfululizo za kirafiki kama sehemu ya maandalizi yao ya kujaribu kufungua ukurasa mpya wa kufanya vyema kwenye mashindano ya Kagame.

Benchi la Ufundi:
KMKM iko chini ya kocha mzoefu Ali Bushiri.

Wachezaji wa kuangaliwa:
Kiungo mshambuliaji, Juma Bwawa, mshambuliaji Matheo Anthony na Hamisi Ally ni miongoni mwa wachezaji wanaopewa nafasi ya kuisadia klabu hii. Wengine ni pamoja na mlinzi Khamisi Ally, na Musa Saidi.


NB: Logo maalumu ya michuano ya CECAFA KAGAME CUP 2015 imeambatanishwa, pamoja na wadhamini DTB Bank na AAR.
  
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)



No comments: