Na: Veronica Kazimoto, MOSHI
AFYA ya Uzazi na Mtoto ni viashiria
vizuri vinavyoonyesha maendeleo ya uchumi na kijamii na vinaainishwa na utoaji
endelevu wa huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa
Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na Usitawi wa Jamii wakati
akifungua rasmi mafunzo ya Wasimamizi, Wahariri na Wadadisi wa Utafiti wa Afya
ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
"Kutokana na umuhimu wa
viashiria hivyo, Serikali kupitia Mpango wake wa Afya ya Uzazi na Mtoto
imefanya juhudi za ziada katika kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na
matatizo ya uzazi na vifo vya watoto wachanga nchini", Amesema Dkt.
Rusibamayila.
Dkt. Rusibamayila amesema kuwa vifo
vya akina mama vinavyotokana na uzazi vimeendelea kupungua ambapo kwa mwaka
2012 kulikuwa na vifo 432 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa hai
ikilinganishwa na vifo 454 kwa kila watoto waliozaliwa hai 100,000
iliyopatikana kwenye Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa mwaka 2010.
Vifo vya watoto wachanga vimepungua
kutoka vifo 51 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai kama ilivyopatikana kutoka
kwenye Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto wa mwaka 2010 na kufikia vifo 45 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai kwa mwaka
2012.
Aidha, Dkt. Rusibamayila ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo amewaasa washiriki hao kufanya kazi yao
kwa weledi ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata takwimu sahihi za Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 kwa ajili ya
kupanga maendeleo.
Pamoja na ufunguzi wa mafunzo hayo,
Mgeni rasmi huyo amezindua matokeo muhimu ya Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa
Huduma ya Afya Nchini wa mwaka 2014/2015.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha
kuwa, vituo
saba (07)
kati ya kumi (10)
vinatoa huduma zote za msingi za afya yaani tiba kwa watoto, chanjo pamoja na ufuatiliaji wa
mwenendo wa ukuaji wa mtoto.
Aidha, huduma za matibabu kwa watoto
wagonjwa zinapatikana kwa asilimia 98
katika vituo vyote vinavyotoa huduma za afya Nchini, pia zaidi ya vituo
vinane (8) kati ya kumi (10) nchini
vinatoa huduma za chanjo kwa watoto.
Kwa huduma za kisasa za uzazi wa mpango
zinapatikana kwa asilimia
80 ya vituo vyote vinavyotoa huduma za afya, ikilinganishwa na asilimia 76 kwa
utafiti wa namna hii wa mwaka 2006.
Aidha, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2014/2015 karibu vituo vyote
vya Serikali
(sawa
na asilimia
97) vinatoa huduma za uzazi wa mpango ikilinganishwa na asilimia 35 ya vituo
binafsi vya kibiashara na asilimia 41 ya vituo vinavyomilikiwa na asasi za
kidini.
Kwa upande wake mwakilishi wa
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo amesema utafiti
huu wa Afya
ya Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 unalenga kukusanya taarifa nyingi za sekta ya
afya zinazotumika katika kutathmini malengo mbalimbali na pia kusaidia katika
kupanga mikakati mipya.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mara
nyingine tena inafanya Utafiti wa Afya ya
Uzazi na Mtoto na Malaria wa mwaka 2015 ambao kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2010. Utafiti huu
utaanza rasmi mwishoni mwa mwezi Agosti, 2015 kwa nchi nzima yaani Tanzania
Bara na Visiwani.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya
na Usitawi wa Jamii akiwahutubia washiriki wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya
Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika leo Moshi,
mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu
akitoa maelezo ya awali wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya
Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika leo Moshi,
mkoani Kilimanjaro.
Baadhi
ya washiriki wa mafunzo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria
Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mgeni
rasmi, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na
Usitawi wa Jamii akizindua matokeo muhimu ya Utafiti wa Tathmini ya Utoaji wa
Huduma ya Afya Nchini wa mwaka 2014/2015 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015
yaliyofanyika leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mgeni
rasmi, Mkurugenzi wa Kinga, Dkt. Neema Rusibamayila kutoka Wizara ya Afya na
Usitawi wa Jamii akionyesha kijitabu cha matokeo muhimu ya Utafiti wa Tathmini
ya Utoaji wa Huduma ya Afya Nchini wa mwaka 2014/2015 wakati wa ufunguzi wa mafunzo
ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015 yaliyofanyika
leo Moshi, mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment