MHARIRI Msanifu wa Gazeti la Mtanzania, Khamis Mkotya (35) juzi alitangaza rasmi nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Chemba, lililopo Mkoa wa Dodoma.
Mkotya ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari na kijana msomi mwenye Shahada ya Siasa na Uongozi, alitangaza nia hiyo mbele ya waandishi wa habari, katika ukumbi wa Dodoma Hotel.
Mkotya ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi ni miongoni mwa waandishi wa habari za Bunge, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wananchi wa Chemba kupitia taaluma yake.
Mkotya ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi ni miongoni mwa waandishi wa habari za Bunge, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea wananchi wa Chemba kupitia taaluma yake.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkotya ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Mirijo Chini wilayani Chemba, alisema changamoto za jimbo hilo ndizo zilizomsukuma kuwania nafasi hiyo.
Katika mkutano huo, Mkotya alisema kwa muda mrefu ametumia taaluma yake kupiga kelele kuibua matatizo na kero za wananchi wa Chemba na baadhi kupatiwa ufumbuzi, hivyo umefika muda kuomba ridhaa yao ili aweze kuwatumikia kimamlaka zaidi.
Uzoefu wake katika masuala ya Bunge kama mwandishi wa habari za Bunge, pia utakuwa chachu na msaada mkubwa kwake katika kutimiza dhana ya uwakilishi ndani ya Bunge.
Ndugu zangu sijakurupuka katika kufikia uamuzi huu, nimekaa, nimetafakari na kujipima mwenyewe na kubaini kwamba ninatosha. Uwezo wa kutekeleza majukumu ya kibunge ninao, nia ya kuwatumikia wananchi wa Chemba ninayo na sababu za kugombea ninazo.
Endapo nitafanikiwa kupata ridhaa ya chama changu, baada ya kupitia mchakato wa kura za maoni na baadaye kushinda uchaguzi wa nje, nitajitahidi kutimiza wajibu wangu ipasavyo.
Natambua kero nyingi zinazowazonga wananchi wa Chemba kama vile shida ya maji, uduni wa huduma za afya, miundombinu mibovu ya barabara, anguko la elimu, ukosefu wa masoko ya mazao na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Katika kuhakikisha tunaondoa changamoto hizo, kipaumbele changu cha kwanza ni maji. Naamini tatizo la maji likimalizika , itawafanya wananchi kufanya shughuli nyingine za maendeleo, kwani hivi sasa uchumi wao mwingi unaishia katika maji.
Pili, nitasimamia ipasavyo fedha za Mfuko wa Jimbo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa na Serikali, katika kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi, kama ilivyoainishwa katika Sheria namba 16 ya mwaka 2009 ya Mfuko wa Jimbo (CDCF).
Tatu, mbali na kufanya jitihada nyingine za kupata fedha kwa ajili kusukuma maendeleo yetu, nitatumia uwezo wangu wote kuisimamia halmashauri yangu ya wilaya, iweze kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kujiunua kiuchumi.
Nne, nakusudia kurejesha imani ya wananchi wa Chemba kwa Chama Cha Mapinduzi, ambayo imetikiswa katika kipindi hiki cha miaka mitano. Hii ni kutokana na aina ya uongozi wa kisiasa wa sasa uliotawaliwa na ubabe zaidi badala ya mbinu shirikishi.
Chama Cha Mapinduzi ni chama kilichojengwa katika misingi ya usawa na umoja, hivyo katika ushindani wa kisiasa wa sasa ni vigumu chama kushinda, kwa kuendeleaa kukumbatia viongozi wasiokuwa waadilifu na wanyenyekevu kwa wananchi.Chemba kama wilaya inahitaji mbunge mwajibikaji, mchapakazi, mtu jasiri, mwenye uadilifu usiokuwa na shaka na anayejua matatizo ya watu wa Chemba.
Sina shaka na uadilifu wangu, uwezo wangu na wala uzalendo wangu si wa kuokoteza. Maendeleo ni mchakato (process), binafsi naamini katika U3 ili kufikia maendeleo. Ukweli, Uwazi na Uwajibikaji.
Viongozi pamoja na wananchi wote kwa ujumla wetu tukiishi katika U3, naamini maendeleo yatapatikana. Kupitia waraka huu natangaza rasmi nia ya kugombea ubunge Jimbo la Chemba katika uchaguzi mkuu wa 2015.
No comments:
Post a Comment