Friday, May 15, 2015

HATIMAYE TUZO ZA FILAMU TANZANIA 2015 MLANGONI! SI YA KUKOSA.

Siku 8 zimebaki kufikia kilele cha tuzo za filamu mwaka 2015.

Ikiwa zimebaki siku chache kufikia kilele cha tuzo za filamu kwa mwaka huu ambapo Tuzo za Filamu Tanzania (TAFA) zinafanyika kwa mara ya kwanza nchini Mei 23, 2015 Mwalimu Nyerere International Conference Center jijini Dar es Salaam. 

Haya ni mapinduzi makubwa katika tasnia ya filamu nchini kwani ni kuonesha mafanikio. Ni vipengele mbalimbali vilivyopo katika kinyang’anyiro cha tuzo za filamu mwaka huu 2015. Tuzo hizo ambazo ni kubwa na zenye hadhi ya juu zimeandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania na washirika mbalimbali .

 “Kazi kubwa ya Shirikisho la Filamu Tanzania ni kusaidia kukuza tasnia ya filamu na kuunga mkono jitihada za wasanii kwa namna mbalimbali. Mbali na hilo pia ni daraja linalowaunganisha wasanii wa tasnia ya filamu na Bodi ya Filamu nchini hivyo kurahisisha utendaji wa kazi zao. Ninayo kamati ya maandalizi iliyo imara na thabiti ambayo imefanya kazi katika mazingira magumu usiku na mchana kuhakikisha tunapata halfa nzuri na ya namna yake ambayo haijawahi kutokea”, Alisema Simon Mwakifwamba, Raisi wa Shirikisho la Filamu Tanzania.

Aliongeza kwa kusema kuwa tasnia ya filamu nchini bado ina safari ndefu ukilinganisha na Hollywood ambao wameshapiga hatua kubwa. Tuzo hizi sasa ni jambo wanapaswa kujivunia kwa wasanii na watengeneza filamu kujivunia. Imeripotiwa kuwa tasnia ya filamu imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa pato la taifa hili linathibitishwa na taarifa ya mapato nchini ya hivi karibuni, na hili linadhihirisha kuwa tasnia ya filamu inafanya kazi kubwa ya kupunguza tatizo la ajira nchini ambalo limekua ni tatizo kwa vijana wengi hapa nchini.

Mara baada ya uzinduzi wa tuzo za Filamu mwishoni mwa mwaka 2014 uwasilishwaji wa kazi za filamu ulianza kwa wakati na baadae zilichaguliwa kwa ustadi mkubwa chache zilizoingia katika kinyang’anyiro cha tuzo hizi na hatua hiyo ilifanikiwa kikamilifu na baadae kutangaza washiriki wanaowania tuzo hizi za filamu. 

Kuna filamu 24 ambazo zimeingia katika kinyang’anyiro cha tuzo hizi na kati ya hizo filamu 12 zitaibuka vinara wa tuzo za Filamu Tanzania 2015. Majaji nao wamefanya kazi kubwa na wana mchango mkubwa, kwani ushindi wa tuzo utategemea 70% kutoka kwa majaji na 30% zitakua ni kura za mashabiki. Majaji wote wanatoka katika Mtandao wa Filamu Afrika Mashariki ambapo Shirikisho la Filamu Tanzania ni mshirika.

Wanatasnia wa filamu wanayo furaha kwa Shirikisho la Filamu kupiga hatua kubwa na hatua walizochukua hata kufanikisha kuwapo kwa tuzo hizi pia wamewashukuru wanakamati wa maandalizi ya tuzo hizi ambao wengi wao wamejitolea kuhakikisha tunapata kitu cha kujivunia.

Nae Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tuzo hizo Bi Caroline Gul alisema, “tunategemea kuwa na hafla nzuri na ya kipekee.  Tumepokea maombi mengi kutoka kwa wanatasnia ya filamu ambao wanataka kuhudhuria kutoka sehemu mbalimbali za Afrika kuwaunga mkono wenzao. 

Mbali na hilo tumeanda burudani kabambe kwaajili ya siku hiyo. Tunachowaomba watanzania ni kutuunga mkono kwa kununua tiketi na kuhudhuria kwa wingi kwani ni kuonesha uzalendo kwa kupenda na kuunga mkono jitihada za kazi za wasanii wetu”


Pia alizungumzia swala la udhamini kwa kusema kuwa bado muda upo hivyo wadhamini wajitokeze kudhamini tuzo hizi kwani bado vitu vingi vinahitajika kufanyika. Alizishukuru taasisi zilizounga mkono tuzo za filamu ambao ni TCRA, International Eye Hospital na Foreplan Clinic bila kusahau EATV & EA Radio, Push Mobile na R&R Associates.

No comments: