Friday, May 15, 2015

Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za Filamu Tanzania yashauriwa kutangaza Tasnia ya Filamu kimataifa

Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo (Kulia) akifungua kikao kati ya wajumbe kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Kamati ya maandalizi ya Tuzo za TAFA leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akizungumza na wadau wa filamu waliofika katika Ofisi za Wizara hiyo kuwasilisha taarifa ya maandalizi ya Tuzo za TAFA nchini itakayofanyika tarehe 23 Mei mwaka huu. Kulia ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za TAFA Bibi. Caroline Gachara Gul (kulia) akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya Tuzo za TAFA nchini kwa Uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na watendaji kutoka Bodi ya Filamu nchini leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mjumbe wa kamati hiyo Bibi. Siima Rubibira.
Wajumbe kutoka Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za TAFA pamoja na maafisa wanaosimamia Filamu nchini kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakimsikiliza kwa makini mjumbe aliyekua akichangia (hayupo pichani) wakati wa kuwasilisha taarifa ya maandalizi ya Tuzo hizo kwa uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Bw. Saimon Mwakifwamba (kushoto) akichangia wakati wa kuwasilisha taarifa ya maandalizi ya Tuzo za TAFA nchini kwa uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na watendaji kutoka Bodi ya Filamu nchini leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni mjumbe wa kamati hiyo Bw. John Kalage.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Mchezo Prof. Elisante Ole Gabriel (waliokaa katikati), Mkurugenzi Idara ya Utamaduni Prof Elimas Mwansoko (wapili kushoto), na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo (wapili kulia) katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za TAFA na watendaji wanaosimamia shughuli za filamu nchini. Picha na Genofeva Matemu - Maelezo.

Na Lorietha Laurence-Maelezo

Kaimu  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel  ameishauri kamati ya maandalizi ya  Tuzo ya Tanzania Film Awards kuhakikisha kuwa wanaitanganza tasnia ya filamu kimataifa.

Akiongea na kamati hiyo leo jijini Dar es Salaam katika kikao cha kupokea taarifa ya Maandalizi ya   Tuzo hizo kilichofanyika katika ukumbi wa wizara ambapo aliwapongeza viongozi wa kamati hiyo kwa juhudi walizozifanya.

“kazi mnayoifanya ni nzuri kwa kuwa inasaidia kukuza na kuitangaza tasinia ya filamu  na hivyo  kuwavutia wadau mbalimbali kuwekeza zaidi” alisema Prof.Elisante.

Aidha  amewataka viongozi wa kamati hiyo kuhakikisha kuwa tuzo zitakazotolewa siku hiyo ziwe za ubora na kiwango cha juu ili kuwahamasisha waandaji wa filamu kuandaa filamu zenye viwango vizuri zaidi. 
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Maandalizi ya Tuzo hizo Bibi. Caroline Gul ameeleza kuwa mpaka sasa wamefanikiwa katika maandalizi mbalimbali ikiwemo ukumbi,tuzo zitakazotolewa na amajaji.

 “Mpaka sasa tumefanikisha  katika suala la ukumbi na kupokea filamu 300 ambazo zipo katika vipengele 12  zenye jumla ya washiriki 50 watakaoshindanishwa siku hiyo” alisema Bibi. Caroline.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fisoo ameishukuru kamati hiyo kuweza kushirikiana na Serikali kwa kila hatua wanayoifanya katika maandalizi ya tuzo hizo.

“Serikali inatambua mchango wenu katika kukuza na kuendeleza tasnia ya filamu nchini ni jambo zuri kwa kuwa inasaidia  kukuza soko la tasnia hii kimataifa” alisema Bi.Fisoo.

Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia nia Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw. Saimon Mwakifwamba ameeleza kuwa wamefanikiwa  kualika  majaji kutoka  East Africa Film Network  ambao watasaidiana na majiaji wa hapa nchini  katika  kupata washindi. 


Tuzo za Tanzania Film  Awards   zinatarajiwa kufanyika tarehe 23 May katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa  Mwalimu Nyerere ambapo tikite zitauzwa kuanzia elfu 50 mpaka laki moja kwa VIP.

No comments: