Balozi Tuvako Manongi Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa akizungumza wakati wa uzinduzi wa onyesho la picha lililoandaliwa kwa ubia baina ya Wakilishi za Kudumu za Italia na Tanzania. Onyesho hilo linahusu huduma za afya ya mama na mtoto zinazotolewa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Doctors with Africa CUAMM katika hospitali ya Tosamaganga, Mkoani Iringa. Kushoto kwa Balozi Manongi ni Balozi wa Italia katika Umoja wa Mataifa, Bw. Sebastioano Cardi na kulina ni mmoja wa Wabunge kutoka Italia anayehudhuria mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya Wanawake.
Balozi Manongi akiteta jambo na Dkt. Andrea Atzori ambaye katika maelezo yake amesema taasisi hiyo ya Doctors with Africa CUAMM inampango wa kupanua huduma zake katika maeneo mengine ya pembezoni mwa Tanzania, mbali ya Tosamaganga na Mikumi.
Dkt. Andrea Atzori akiwa na Bi. Tully Mwaipopo, Afisa wa Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mara baada ya uzinduzi wa onyesho hilo.
baadhi ya picha zinazoonesha huduma ya utoaji wa afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Tosamaganga , huduma hiyo ainayoendana manafumzo kwa wataalamu wa afya imeweza kuokoa maisha ya wanawake wajawazito pamoja na watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda.
Na Mwandishi Maalum, New York
Tanzania imeelezea kuridhishwa kwake na ushirikiano uliopo baina ya Serikali na Taasisi Binafsi katika uboreshaji na utoaji wa huduma za afya zikiwamo zinazomlenga mama na mtoto. Na hivyo kuchangia katika upiguzaji wa vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Kauli hiyo imetolewa siku ya jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati wa uzinduzi wa onyesho kwa njia ya picha kuhusu huduma za afya zinazotolewa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Doctors with Africa CUAMM inayofanya shughuli za utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Tosamaganga, Mkoani Iringa.
Picha hizo zinaonyeshwa katika corridor za Umoja wa Mataifa, sambamba na mkutano wa 59 wa Kamisheni ya Hadhi ya Wanawake ( CSW) unaofanyika hapa Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mkutano unaojadili masuala mbalimbali yanayomhusu mwanamke na mtoto wa kike, kuanzia elimu, fursa na haki sawa, huduma bora za afya, uwezeshwaji , haki za mwanamke na mtoto wa kike pamoja na changamoto zinazo wakabili.
Balozi Manongi amesema ni kwa kushirikiana ndipo nchi kama Tanzania inaweza kuongeza kasi ya kuwafikishia huduma za afya wananchi wengi, na kuwa uwepo wa Taasisi kama ya Doctors with Africa CUAMM na mchango wake katika utoaji wa huduma za afya huko Tosamaganga na maeneo mengine ni kielelezo sahihi cha ushirikiano anaouzungumzia.
Akasema mchango wa Taasisi hiyo ni mfano wa kuigwa na ndiyo maana Tanzania katika maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015 moja ya maeneo inayoyapigia chapuo ni pamoja na hilo la afya ya mama na mtoto pamoja na ushirikiano miongoni mwa wadau mbalimbali.
“ Nyinyi ni kielelezo sahihi cha ubia na ushirikiano tunaouhimiza. Asanteni sana kwa mchango wenu na asanteni kwa kudhirisha kwamba inawezekana kufanya kazi kwa ushirikiano”. akasema Balozi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi hiyo, Bw. Andrea Atzori, amesema Taasisi yake ambayo imekuwa nchini Tanzania tangu mwaka 1968 imejielekeza Zaidi katika utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya vijijini hususani kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga wakiwamo wanaozaliwa kabla ya muda.
Huduma nyingine zinatolewa na taasisi hiyo ni pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa afya, huduma za uzazi salama kupitia mpango wao wa miaka mitano walioupa jina la “mama na mtoto kwanza”.
Aidha kwa mujibu wa Dkt. Andrea Atzori, Taasisi hiyo inatarajiwa kupanua huduma zake katika maeneo mengine Zaidi ya pembezoni kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma ya afya pale walipo.
Pamoja na Tanzania, Doctors with Africa CUAMM iliyoanzishwa mwaka 1950 na makao yake yakiwa nchini Italia,pia inaendesha shughuli zake katika nchi za Angola, Ethiopia, Msumbiji, Sudani ya Kusini, Uganda na Sierra leone.
No comments:
Post a Comment