Tuesday, March 10, 2015

Tatizo la mgawo wa umeme Arusha kumalizika Juni

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Jimbo la Singida, Martha Mlata (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Dkt. Miganda Manyahi (kulia), jijini Arusha kabla ya kuanza kwa ziara kwenye miradi ya umeme. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini inafanya ziara katika miradi ya umeme iliyopo katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ili kujionea hatua ya utekelezwaji wake pamoja na kuzungumza na watendaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Richard Ndassa (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Felix Ntibenda (kulia) mara baada ya Kamati hiyo kuwasili ofisini kwake kwa ajili ya kupokea taarifa ya mkoa kabla ya kuanza kwa ziara kwenye miradi ya umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Felix Ntibenda ( wa nne kutoka kushoto waliosimama mbele), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Richard Ndassa ( wa tano kutoka kushoto waliosimama mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini mara baada ya kumalizika kwa kikao.
Meneja Mradi wa Kusambaza Umeme unaojulikana kwa jina la Electricity V unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi Florence Gwang’ombe (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Richard Ndassa (kulia) mara baada ya kamati hiyo kuwasili kwenye eneo la mradi huo ili kujionea maendeleo ya utekelezwaji wake.
Mtaalam kutoka Kampuni ya Sweco International AB, Pal Aberg (kushoto) akiielezea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiendelea na ziara katika eneo la kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo Njiro nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mtaalam kutoka Kampuni ya Sweco International AB, Pal Aberg (kulia) akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye eneo la kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Wataalam kutoka kampuni ya Sweco International AB, wakiendelea na ujenzi katika kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mtaalam kutoka Kampuni ya Sweco International AB, Pal Aberg (kushoto) akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye chumba cha kuendesha mitambo ya umeme ( control room) ndani ya kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo Njiro nje kidogo ya jiji la Arusha.
Meneja Mradi katika Kituo cha Kupooza na Kusambaza Umeme cha KIA Mhandisi Emmanuel Manirabona (kulia) akiielezea Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo hicho kilichopo mkoani Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa (wa kumi na moja kutoka kushoto), Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Felchesmi Mramba (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati hiyo na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini mara baada ya kukamilisha ziara yake katika kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha KIA kilichopo mkoani Kilimanjaro.
  • Ni baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa bilioni 72.5 
  • Wateja wapya 30,000 kuunganishwa

Na Greyson Mwase, Arusha

Meneja Mradi wa  Kusambaza  Umeme unaojulikana kwa jina la  Electricity  V unaofadhiliwa na  Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi  Florence Gwang’ombe amesema kuwa  tatizo la kukatika katika kwa  umeme katika mkoa  wa Arusha litakwisha mapema Juni mara baada ya kukamilika kwa  kituo cha kupooza na kusambaza umeme  kilichopo katika eneo la Njiro, nje kidogo ya jiji la  Arusha.

Mhandisi Gwang’ombe aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu  ya Bunge ya Nishati na Madini  iliyofanya ziara katika kituo hicho ili kujionea maendeleo yake pamoja na kuishauri  serikali  jinsi ya  usimamizi wake.

Alisema mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho mbali na kuboresha upatikanaji wa  nishati ya umeme katika jiji  la Arusha,  wateja wapya wapatao  30,000 wanategemewa kuunganishiwa umeme kutoka katika kituo hicho.

Akielezea   mradi huo  kwa ujumla Mhandisi  Gwang’ombe alisema kuwa  mradi huo unaofadhiliwa na  Benki ya Maendeleo  ya Afrika (AfDB) kwa  mkopo wa kiasi cha shilingi za kitanzania 72,588, 506,400 unahusisha  ujenzi wa njia za umeme wenye  urefu wa kilomita 480 za msongo wa kilovoti 33 na ufungaji wa transfoma 102 za kusambaza umeme zenye ukubwa wa 33/0.4 kV.

Alisema pia mradi huu unahusisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme vya  Ilala, Sokoine katika mkoa wa Dar es  Salaam  na  upanuzi wa kituo cha  kupoozea umeme cha Njiro.

Alisisitiza kuwa mradi  unatekelezwa na Mkandarasi  National Contracting  Company ambaye alishinda zabuni  ya ujenzi  na ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme katika mikoa ya Dar es  Salaam na  Arusha  na mkandarasi  Eltel Networks TE AB ambaye alishinda zabuni  ya ujenzi na ukarabati wa mifumo   ya kusambazia umeme  katika mikoa ya Shinyanga na  Mwanza.

Akielezea   hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa  kituo cha kupoozea umeme cha Njiro,  Mhandisi Gwang’ombe alisema kazi zinazoendelea katika kituo hicho ni pamoja na ufungaji wa transfoma mbili  na ufungaji wa mitambo  ya kisasa kwa ajili ya kuendesha  na kulinda mifumo ya umeme.

Aliongeza kuwa uagizaji na utengenezaji wa vifaa umekamilika  kwa asilimia 85,  kazi za ujenzi  zimekamilika kwa  asilimia 76 pamoja na kumalizika kwa kufunga na kuunganisha  vifaa na mifumo  ya umeme.

Alisisitiza kuwa mradi huu unategemewa kuongeza ukuaji wa uchumi katika mkoa wa Arusha pamoja na mikoa mingine   kama Shinyanga na Mwanza kwani utachochea ukuaji   wa viwanda vidogo vidogo na biashara katika maeneo husika pamoja na  kuongeza fursa za ajilra kwa wananchi.

Aliendelea kusema kuwa mradi huo utaboresha  huduma za jamii kwa wananchi kutokana na  upatikanaji wa umeme mashuleni, mahospitalini na kwenye maeneo mengine ya  jamii  husika na hivyo kupunguza umasikini  kwa wananchi  jambo ambalo linaendana na malengo ya siasa ya nchi.

Akizungumzia lengo la  mradi,  Mhandisi Gwang’ombe alisema kuwa lengo la mradi  ni kuongeza  uwezo wa kusambaza umeme wenye kiwango  kinachotakiwa na  usiokatikakatika na kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)  kuweza kuwafikia na kuwapatia umeme  wenye uhakika wateja wengi zaidi  ambao bado hawajapatiwa huduma ya umeme.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini  (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba aliiambia  Kamati ya Bunge kuwa  ongezeko la wateja wa kawaida  na  viwanda lilisababisha ongezeko la kasi la matumizi  kufikia Megawati 70 hali iliyopelekea shirika   kuboresha  na kujenga vituo  vya  kupoozea na kusambazia umeme.

Mhandisi Mramba alisema, kabla ya  ujenzi wa kituo hicho, hali ya umeme katika jiji la Arusha ilikuwa ni mbaya hali iliyopelekea ujenzi wa kituo hicho na kusisitiza kuwa Shirika limeamua kufanya  mapinduzi katika sekta ya umeme kwa kuhakikisha linashirikiana na wawekezaji  mbalimbali na wataalamu wake katika ujenzi wa vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme ili kuzalisha nishati  ya umeme ya uhakika.

No comments: