Tuesday, March 10, 2015

WAKUNGA WA JADI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WATALAM WA AFYA ZANZIBAR

Mmoja wa wakunga wa jadi Bi. Namboto Sheha Kombo akielezea jinsi wanavyofanya kazi zao za ukunga katika mkutano uliofanyika Hospitali ya Kivunge Mkoa wa kaskazini "A" Unguja.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mahamoud Thabit Kombo akizungumza na wakunga wa jadi, na kuwataka washirikiane na watalaam wa Afya katika kazi zao ili kupunguza vifo vya Akinamama na watoto.
Msaidizi daktari dhamana Hospitali ya Muembe ladu Ruzuna A.M. Shamte akifahamisha kitu katika mkutano wa wakunga wa jadi na watalam wa afya huko Kivunge Mkoa wa kaskazini "A" Unguja.
Baadhi ya Wakunga wa Jadi na watalam wa Afya waliofika katika mkutano wa kukuza mashirikiano huko Kivunge Mkoa wa kaskazini "A" Unguja wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mahamoud Thabit Kombo (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.
Dkt. Dhamana Hospitali ya Kivunge Khamis Hamad Ali akitoa nasaha zake katika mkutano wa Wakunga wa Jadi na watalam wa Afya wa kukuza mashirikiano katika kufanya kazi zao. Picha na Makame Mshenga- Maelezo Zanzibar.

Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar                                       
Dawa za Kienyeji wanazopatiwa kina mama wajawazito kutoka kwa  Wakunga wa Jadi wakati wa kujifungua husababisha matatizo ya kiafya kwa watoto wanaotarajiwa kuzaliwa pamoja na akina mama hao.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahamoud Thabit Kombo wakati akizungumza na Wakunga wa Jadi wa Vijiji vya Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali kuu ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyopo katika kijiji cha Kivunge mkoani hapo.
Amesema kuwa dawa hizo hua zinahatarisha zaidi maisha ya kina mama wajawazito na watoto wanaotarajiwa kuzaliwa hususan kwa akina mama wenye viashiria hatari wakati wa ujauzito ikiwemo maradhi ya Presha na Sukari ambayo yanaweza kusababisha kupoteza uhai wao kwa haraka zaidi.
Naibu Waziri huyo amesema ipo haja kwa Wakunga wa Jadi kuwafikisha kina mama wajawazito katika Vituo vya Afya pindi wanapobaini kuwa kina mama hao wana matatizo ya kiafya au mtoto kuleta matatizo wakati wa kujifungua na kuacha kung’ang’ania kuwazalishia nyumbani ili kuokoa maisha ya mtoto na mama mja mzito.
Kwa upande wake Daktari Dhamana wa Hospitali ya Kivunge Nd. Khamis Hamad Ali amesema ipo haja kwa Wakunga wa Jadi kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar ili kufanikisha zoezi la uzalishaji wa kina mama kwa usalama zaidi pamoja na kuwaomba Wakunga hao kwenda nao wagonjwa katika vituo vya afya kwa kupata uangalizi wa kitaalamu zaidi.
Amesema watoto wengi hupata matatizo ya magonjwa yakiwemo ya Kifafa na Utaahira kutokana na uchungu mkali unaowapata kina mama wakati wa kujifungua hususan kwa wale wanaojifungulia kwa Wakunga wa Jadi kwani wakunga hao huwa hawana vifaa vya kupunguza makali ya uchungu wa kina mama hao ikiwemo sindano maalum wanazochomwa kina mama kwa ajili ya kupunguza uchungu huo.
Sambamba na hayo Dkt. Khamis amesema inaripotiwa kuwa 5% - 15% ya wanawake wote Duniani huwa wanapata matatizo wakati wa kujifungua pamoja na kuwaomba kina mama kuwa wawazi kuelezea matatizo waliokwisha kuyapata kabla ya siku za kujifungua kufika pindi wanapokwenda katika vituo vya afya ili kurahisisha uzalishaji huo.
Nae Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Muembe Ladu Zanzibar Dkt. Ruzuna Abdulrahman Moh’d amesema ipo haja kwa Wakunga wa Jadi kupatiwa Taaluma na Elimu ya kisasa ili waendelee kuisaidia Serikali kwa kuwazalisha kina mama wajawazito kwa njia za kisasa na zilizo salama zaidi.
Ametanabahisha kuwa dawa za kienyeji zinaweza kutumika kwa kina mama waliokwisha kujifungua ikiwa mtoto amezaliwa bila ya matatizo yoyote ya kiafya.
Nao Wakunga wa Jadi wa Wilaya Kaskazini “A” Unguja wamesema kuwa akina mama wengi waja wazito huwa wanakimbia kwenda kuzalia Hospitali ili kukimbia manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa madaktari hususan kutoka kwa madktari wadogo na hivyo kuwaomba madaktari hao kujirekebisha kitabia ili kuokoa maisha ya kina mama na watoto kwa maendeleo ya Taifa.

Aidha wamewaomba madaktari kutoka serikalini kuendelea kutoa elimu ya uzazi kwa akina mama na Wakunga wa Jadi pamoja na kuwaasa wananchi wenzao hususan kina mama kwa kuyasikiliza na kuyafanyia kazi yale yanayotolewa na Wataalamu wa Afya kwa lengo la kujiongezea ujuzi katika kazi yao ya uzalishaji wa akina mama.

No comments: