Na
Bashir Yakub
Nimeandika makala nyingi kuhusu
namna ya kisheria ya kuepuka kununua nyumba/viwanja vyenye
migogoro kwakuwa migogoro ya vitu
hivi inaumiza sana. Waliokutana na migogoro hii wanajua vyema ninaongea nini. Katika mwendelezo wa
kumuepusha mnunuzi na janga hili, leo tena
tuangalie taratibu za ununuzi wa nyumba/kiwanja cha mirathi. Nataka ieleweke vyema kuwa taratibu
za manunuzi ya nyumba/kiwanja zinatofautiana.
Tofauti kubwa ni za kisheria hasa namna ya uandishi wa mkataba na nyaraka ambazo zitaambatana na mkataba huo. Eneo hili nalo naliongelea
kwakuwa ni eneo ambalo kwa upande wake nalo limewaingiza wanunuzi wengi wa
nyumba/viwanja katika migogoro ambayo ingeweza
kuepukwa mapema iwapo taarifa kama hizi pengine mnunuzi angezipata mapema. Kisheria si kweli kuwa kila aina ya
mkataba unaweza kut umika kununua kila aina
ya nyumba. Mkataba huandaliwa kutegemea na mazingira ya kitu chenyewe. Nyumba/kiwanja
ambacho wauzaji wake ni wasimamizi wa
mirathi ni tofauti na nyumba/kiwanja ambacho
muuzaji si msimamizi mirathi.
Tatizo kubwa ambalo limewasumbua
wengi mahakamani ni kununua nyumba/kiwanja
cha mirathi kwa
kutumia utaratibu uleule wa kununulia kiwanja/nyumba ya kawaida ambayo
muuzaji wake ni mmiliki halisi yaani si
msimamizi wa mirathi.
( 1 ) UTAJUAJE KAMA NYUMBA/KIWANJA UNACHONUNUA NI CHA MIRATHI.
Niliwahi kuandika katika makala zilizopita wakati nikieleza namna ya kitaalam ya kujua
kama eneo unalonunua kama lina mgogoro au hapana kuwa katika ununuzi ardhi, nyumba/viwanja vimegawanyika
sehemu kuu tatu. Kwanza kuna vyenye hati, Pili kuna vyenye leseni za
makazi na tatu ni vile vyenye mikataba ya
kununulia. Hivi ni vile ambavyo havina hati
wala leseni za makazi. Sasa ili ujue
kuwa nyumba/kiwanja unachouziwa
ni cha mirathi au hapana
, hatua ya kwanza ni kuwauliza wauzaji au muuzaji kama eneo ni lake au ni msimamizi wa mirathi. Kama atasema yeye ni msimamizi wa mirathi basi hapatakuwa na shida mnunuzi utaendelea na
utaratibu nitakaoeleza katika makala haya. Lakini akisema hapana si msimamizi wa mirathi basi utakachokifanya ili kujua ukweli wake ni kuomba nyaraka ya eneo husika zile nilizotaja hapa juu ili
uone taarifa za mmiliki. Ukikagua na
kugundua kuwa hakuna jina lake basi atatakiwa kutoa maelezo kwanini yeye
ni muuzaji na anachouza hakina jina lake.Hii ni rahisi
wala haina ufundi sana isipokuwa tu ni katika hatua za
mwanzo za kuonesha umakini. Kama nyaraka
atakayokuonesha itakuwa haina jina lake
na yeye anataka kuuza kama msimamizi wa mirathi
basi hakikisha ana nyaraka hii hapa chini.
( 2 ) MUUZA
KIWANJA/NYUMBA YA MIRATHI
LAZIMA AMPATIE MNUNUZI FOMU HII KISHERIA.
Fomu na 4 ni
fomu maalum anayotakiwa kuwa nayo muuzaji wa nyumba/kiwanja cha mirathi
kisheria. Kuwa na fomu hii ni lazima
kisheria na nitoe angalizo kuwa mnunuzi kamwe asikubali kununua kiwanja/nyumba ya mirathi bila fomu hii. Mnunuzi wa nymba ya mirathi anaponunua bila muuzaji kuwa amempatia fomu hii kisheria ni sawa na hajanunua
bila ya kujali gharama alizotoa. Fomu hii ndiyo inayompatia mamlaka
muuzaji mali ya mirathi kuuza
kwakuwa mali ile inakuwa si yake kwa
uhalisi.
( 3 ) FOMU HII HUTOLEWA
WAPI.
Fomu hii hutolewa na mahakama za Tanzania. Fomu hii hutolewa baada ya kuwa limefunguliwa
shauri la usimamizi wa mirathi ambapo
huteuliwa msimamizi wa mirathi ambaye sasa ndiye hustahili kuuza nyumba/kiwanja ikiwemo mali nyingine pia. Aidha mahakama za mwanzo huhusika na
kutoa fomu hizi kwa wingi zaidi lakini pia
mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi na mahakama kuu nazo huwa na mamlaka ya kutoa
fomu hizi kutegemeana na matakwa
ya kisheria. Suala la msingi kwa mnunuzi wa
nyumba anayekagua fomu hii ni
kuwa ahakikishe fomu hii imetolewa na mahakama kati ya mahakama nilizotaja.
( 4 ) MNUNUZI
WA NYUMBA/KIWANJA KUTHIBITISHA
UHALALALI NA UKWELI WA
FOMU.
Kutokana kuwapo utapeli na
ghushi nyingi hasa katika manunuzi ya viwanja na majumba
unaotokana na hamu kubwa ya wauzaji matapeli kutaka kukamata
hela nyingi za haraka zitokanazo na mali
hizi basi zimekuwapo kesi nyingi ambapo fomu hizi za usimamizi wa
mirathi zimeghushiwa na wanunuzi
kulazimika kuingia hasara. Kughushi nyaraka hizi ni
rahisi mno kwa kuwa kinachotakiwa ni
kidogo tu ni sahihi na muhuri wa mahakama vitu ambavyo hutengenezwa halafu
mtu anauza nyumba. Kuepukana na hili
njia ya uhakika zaidi ni kuomba upate nakala ya fomu hiyo kutoka kwa muuzaji halafu kwenda nayo mpaka mahakama husika
ambayo imeandikwa kwenye fomu hiyo na kuomba kuthibitishiwa kama ni
kweli mahakama hiyo ilitoa hiyo fomu. Majibu utapata ya uhakika na yenye
usalama kwako.
( 5 ) TAARIFA
GANI MNUNUZI WA NYUMBA ATEGEMEE KUZIKUTA KWENYE FOMU.
Kwanza kwa juu lazima iwe na picha ya
muuzaji(Msimamizi mirathi). Pili itakuwa na
jina la mahakama iliyotoa fomu
hiyo namba ya usimamizi wa mirathi, tarehe ilipotolewa, jina la
msimamizi mirathi ambaye ndiye muuzaji, jina la marehemu ambaye ndiye alikuwa
mmiliki mali halisi na tarehe ya kifo
chake. Kwa chini mwisho itakuwa na kiapo
cha muuzaji sahihi ya hakimu au jaji
aliyeiidhinisha, tarehe ilipotolewa , muhuri wa mahakama pamoja na sahihi
ya msimamizi mirathi ambaye ni muuzji
katika makala haya.Mnunuzi jihadhari , utapeli katika manunuzi ya nyumba na viwanja kwasasa ni janga la kitaifa.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
1 comment:
Utaratibu una tofauti yeyote kama ndugu mmojawapo wa warithi katika familia ananunua nyumba ya mirathi kutoka kwa nduguze?
Post a Comment