Sunday, February 1, 2015

MAKALA SHERIA: USINUNUE KIWANJA/NYUMBA YA MIRATHI BILA KUPATA FOMU HII

Na  Bashir  Yakub

Nimeandika makala nyingi kuhusu namna  ya kisheria ya kuepuka  kununua nyumba/viwanja  vyenye  migogoro kwakuwa  migogoro ya vitu hivi inaumiza sana. Waliokutana na migogoro hii wanajua  vyema ninaongea nini. Katika mwendelezo wa kumuepusha mnunuzi  na janga hili, leo tena tuangalie taratibu za ununuzi wa nyumba/kiwanja cha  mirathi. 

Nataka ieleweke vyema kuwa taratibu za manunuzi ya nyumba/kiwanja  zinatofautiana. Tofauti kubwa  ni za kisheria hasa  namna ya uandishi wa mkataba  na nyaraka ambazo  zitaambatana na  mkataba huo. 

Eneo hili nalo naliongelea kwakuwa ni eneo ambalo kwa upande wake nalo limewaingiza wanunuzi wengi wa nyumba/viwanja katika migogoro  ambayo ingeweza kuepukwa mapema iwapo taarifa kama hizi pengine mnunuzi angezipata  mapema.  

Kisheria si kweli kuwa kila aina ya mkataba  unaweza kut umika kununua kila aina ya nyumba. Mkataba huandaliwa kutegemea na mazingira ya kitu chenyewe. Nyumba/kiwanja ambacho wauzaji wake  ni wasimamizi wa mirathi ni tofauti na nyumba/kiwanja ambacho  muuzaji si msimamizi mirathi.  

Tatizo  kubwa ambalo limewasumbua wengi mahakamani ni kununua nyumba/kiwanja  cha  mirathi  kwa  kutumia  utaratibu uleule  wa kununulia kiwanja/nyumba ya kawaida ambayo muuzaji wake ni mmiliki halisi  yaani si msimamizi wa mirathi. 

( 1 ) UTAJUAJE  KAMA NYUMBA/KIWANJA UNACHONUNUA  NI CHA MIRATHI.

Niliwahi kuandika  katika makala zilizopita  wakati nikieleza namna ya kitaalam ya kujua kama eneo unalonunua kama lina mgogoro au hapana  kuwa katika ununuzi  ardhi, nyumba/viwanja vimegawanyika sehemu  kuu tatu. Kwanza  kuna vyenye hati, Pili kuna vyenye leseni za makazi na tatu  ni vile vyenye mikataba ya kununulia. Hivi ni vile ambavyo havina hati  wala leseni za makazi. Sasa ili ujue  kuwa nyumba/kiwanja  unachouziwa  ni cha  mirathi au  hapana  , hatua  ya kwanza  ni kuwauliza wauzaji au muuzaji kama  eneo ni lake au  ni msimamizi wa mirathi.

 Kama atasema  yeye ni msimamizi  wa mirathi basi  hapatakuwa na shida mnunuzi utaendelea na utaratibu nitakaoeleza katika makala haya. Lakini akisema hapana  si msimamizi wa mirathi  basi utakachokifanya  ili kujua ukweli wake ni kuomba nyaraka  ya eneo husika zile nilizotaja hapa juu ili uone taarifa za mmiliki. 

Ukikagua  na kugundua kuwa hakuna  jina lake  basi atatakiwa kutoa maelezo kwanini  yeye  ni muuzaji na anachouza hakina jina lake.Hii ni  rahisi  wala  haina  ufundi sana isipokuwa tu ni katika hatua za mwanzo za kuonesha umakini. Kama  nyaraka atakayokuonesha itakuwa haina jina lake   na yeye anataka  kuuza  kama msimamizi  wa mirathi  basi hakikisha ana nyaraka hii  hapa chini.

( 2 ) MUUZA KIWANJA/NYUMBA  YA  MIRATHI  LAZIMA  AMPATIE MNUNUZI   FOMU HII KISHERIA.

Fomu na  4  ni fomu maalum anayotakiwa kuwa nayo muuzaji wa nyumba/kiwanja cha mirathi kisheria. Kuwa na fomu hii ni lazima  kisheria na nitoe angalizo kuwa mnunuzi kamwe asikubali  kununua kiwanja/nyumba ya mirathi  bila fomu hii.  Mnunuzi wa nymba ya mirathi anaponunua  bila muuzaji kuwa  amempatia fomu hii kisheria ni sawa  na hajanunua  bila ya kujali gharama alizotoa. Fomu hii ndiyo inayompatia  mamlaka  muuzaji  mali ya mirathi kuuza kwakuwa mali ile inakuwa si yake  kwa uhalisi.

( 3 ) FOMU  HII  HUTOLEWA  WAPI.

Fomu hii  hutolewa na mahakama za Tanzania.  Fomu hii hutolewa baada ya kuwa limefunguliwa shauri  la usimamizi wa mirathi  ambapo  huteuliwa  msimamizi  wa mirathi ambaye sasa ndiye  hustahili kuuza nyumba/kiwanja  ikiwemo mali nyingine  pia. Aidha mahakama za mwanzo huhusika na kutoa fomu hizi kwa wingi zaidi lakini pia  mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi  na mahakama kuu nazo  huwa na mamlaka  ya kutoa  fomu hizi kutegemeana  na matakwa ya kisheria. Suala la msingi kwa mnunuzi wa  nyumba anayekagua  fomu hii ni kuwa  ahakikishe  fomu hii imetolewa na mahakama kati  ya mahakama nilizotaja. 

( 4 )  MNUNUZI  WA NYUMBA/KIWANJA KUTHIBITISHA  UHALALALI  NA  UKWELI WA  FOMU.

Kutokana kuwapo utapeli  na  ghushi nyingi   hasa katika  manunuzi ya viwanja na majumba unaotokana  na  hamu kubwa ya wauzaji matapeli kutaka kukamata hela nyingi  za haraka zitokanazo na mali hizi  basi zimekuwapo  kesi nyingi ambapo fomu hizi za usimamizi wa mirathi  zimeghushiwa na  wanunuzi  kulazimika kuingia hasara. 

Kughushi nyaraka  hizi ni  rahisi mno kwa kuwa kinachotakiwa ni  kidogo tu ni sahihi na muhuri wa mahakama vitu ambavyo hutengenezwa halafu mtu anauza nyumba. Kuepukana na hili  njia  ya uhakika zaidi ni  kuomba upate nakala ya  fomu hiyo kutoka  kwa muuzaji  halafu kwenda nayo mpaka mahakama  husika  ambayo imeandikwa kwenye fomu hiyo na kuomba kuthibitishiwa kama ni kweli mahakama hiyo ilitoa hiyo fomu. Majibu utapata ya uhakika na yenye usalama kwako.

( 5 )  TAARIFA  GANI  MNUNUZI  WA NYUMBA ATEGEMEE  KUZIKUTA  KWENYE FOMU.

Kwanza kwa juu lazima iwe na picha ya muuzaji(Msimamizi mirathi). Pili itakuwa na  jina la mahakama  iliyotoa fomu hiyo namba  ya usimamizi wa  mirathi, tarehe ilipotolewa, jina la msimamizi mirathi ambaye ndiye muuzaji, jina la marehemu ambaye ndiye alikuwa mmiliki mali halisi na tarehe ya  kifo chake. Kwa chini mwisho itakuwa na  kiapo cha muuzaji  sahihi ya hakimu au jaji aliyeiidhinisha, tarehe ilipotolewa , muhuri wa mahakama pamoja na sahihi ya  msimamizi mirathi ambaye ni muuzji katika  makala haya.Mnunuzi  jihadhari , utapeli katika manunuzi  ya nyumba na viwanja  kwasasa ni janga la kitaifa. 

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com

No comments: