Mkurugenzi wa Kampuni ya Ibraline ,Ibrahim Shayo. |
Na Dixon Busagaga wa Globu ya
Jamii Moshi.
SIKU chache baada ya Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutangaza punguzo la
bei ya Mafuta Kampuni ya kutoa huduma ya usafirishaji wa ndani na nje
ya nchi ya Ibraline imetangaza kushusha nauli kwa nusu ya bei elekezi
ya SUMATRA.
Hatua hiyo inakuja wakati baadhi ya wananchi
kulalamika kutokuwepo na ahueni yoyote licha ya kwamba serikali imetangaza
kushusha bei ya bidhaa ya Mafuta kwa nchi nzima kufuatia bidhaa
hiyo kushuka bei katika soko la dunia.
Akizungumza ofisini
kwake mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ibrahimu Shayo alisema Kampuni imefikia hatua
hiyo ikiwa ni sehemu ya kutoa shukurani kwa wateja wake ambao wamekuwa
wakitumia huduma ya usafiri inayotolewa na Ibraline.
“Tumeamua kufanya hivi lengo ni kuwashukuru wateja wetu
wanao tumia huduma ya usafiri unaotolewa na kampuni yetu ya
Ibraline…ningewajua mmoja mmoja ningeweza kuwapa mkono lakini kwa kuwa
wanaishi maeneo tofauti ndio sababu tumeamua kurudisha kile tunachopata
kwa njia ya kuwapunguzia bei.”alisema Shayo.
“Hivyo basi kuanzia sasa magari yetu yatatoa huduma zake
kwa nusu ya bei elekezi inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri
wa nchi Kavuna
Majini (SUMATRA) ambapo abiria watatozwa kiasi cha Shilingi
17,000 badala ya 33,300 kwa usafiri wa kwenda na kutoka Dar es
Salaam wakitokea Arusha.”aliongeza Shayo.
Alisema unafuu wa ofa hiyo abiria wataipata endapo
watafika moja kwa moja katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko Mikoa ya
Kilimanjaro, Arusha na Dar es Salaam badala ya kutumia mawakala
wanaopatikana katika vituo vikuu vya mabasi katika mikoa
hiyo.
“Unafuu wa gharama ya nauli utaipata pekee endapo
utafika ofisi za kampuni yetu zilizoko mikoani ambapo kwa Arusha ofisi
ziko Kibla,Kilimanjaro tunapatikana barabara ya Ghala jirani na
kiwanda cha kubangulia Kahawa (Cofee Curing) na Dar es Salaam tuko
Ubungo ofisi namba 19.”alisema Shayo.
Aidha Shayo alisema
hivi sasa Kampuni yake imeanzisha safari za kuelekea Masasi mkoani Mtwara
baada ya kupokea maombi ya wakazi wa maeneo hayo na kampuni kuamua
kutoa gari tatu za kisasa kwa ajili usafiri wa kuelekea
huko.
Alisema kampuni ya Ibraline inategemea kuanza
kutoa huduma ya usafiri kwa mikoa zaidi ya nane na kwamba kinachofanyioka sasa ni
kuangalia uwezekano wa namna gani inaweza kuingia mikoa ya Dodoma
,Morogoro na
Mbeya.
Juzi baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro walidai
hakuna haueni yoyote wanayopata licha ya kushuka kwa huduma
hiyo.
Baadhi ya wakazi hao ,Joachim Kimaro, Andrea Lyimo
na Yusta Mafangavo waliliambia globu ya Jamii kuwa wanaofaidika na kushuka
kwa bidhaa za Mafuta zaidi ni wamiliki wa vyombo vya usafiri
.
“Wamiliki wa magari ya biashara kama mabasi na
magari makubwa ya kusafirisha mizigo ndio wamenufaika na kushuka kwa bei ya
mafuta ,kwa sababu nauli za kusafiria hata kusafirisha mizigo
hazijashuka bado ziko pale pale.”alisema Kimaro.
Alisema wengine wanao nufaika na kushuka kwa bei ya
mafuta ni wafanyabiashara wa bidhaa katika maduka ambao licha ya
kununua mafuta ya taa kwa bei elekezi ya EWURA bado wameendelea kuuza
bidhaa hiyo kwa mtumiaji wa kawaida kwa bei ile ile ya zamani.
No comments:
Post a Comment