Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki akihutubua katika mahafali ya 14 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama - Lushoto wilayani Lushoto hivi karibuni.
Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) wameaswa kutumia elimu waliyopata kwa kuwatumikia wananchi kwa uaminifu ili kulinda heshima ya chuo hicho.
Akizungumza hivi karibuni katika mahafali ya 14 ya chuo hicho yaliyofanyika wilayani Lushoto mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshiwa Angellah Kairuki aliwakumbusha wahitimu hao kuwa waaminifu na kulinda maslahi ya umma popote watakapobahatika kufanya kazi.
“Nitumie fursa hii kuwaasa sana wahitimu kwamba, popote mtakapobahatika kupata kufanya kazi, fanyeni kazi kwa umahiri mkubwa na kwa uaminifu, kwa wakati na kulinda maslahi ya umma wa Tanzania na hivyo kubeba taswira nzuri ya Chuo ipasavyo,” alisema Naibu Waziri Kairuki katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Jaji Mstaafu John Mrosso.
Kuhusu upatikanaji wa ajira kwa wahitimu hao, Naibu Waziri Kairuki aliwashauri kuchangamkia nafasi zinazotangazwa na taasisi mbalimbali zikiwemo za utumishi katika sekta ya sheria ya hapa nchini.
“Kuhusu nafasi za ajira, ninawakaribisheni kujiunga na Wizara yangu pamoja na taasisi zake kwa kuzingatia nafasi zitakapokuwa zikipatikana. Tafadhali tumieni nafasi za ajira zitakazopatikana kutokana na utekelezaji wa maboresho katika sekta ya Sheria,” Naibu Waziri aliwaambia wahitimu hao 649 wa Stashahada na Astashahada ya Sheria.
Akizungumza katika mahafali hayo, Jaji Mrosso alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa chuo hicho na Serikali mwaka 1998 ni kuboresha utendaji kazi wa maafisa wa Mahakama na wasaidizi wao pamoja na taasisi nyingine zinazoshughulika na utoaji wa haki nchini.
Jaji Mrosso, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake, chuo hicho kimepata mafanikio kadhaa yakiwemo kuajiri na kuendeleza kitaaluma watumishi wake wa taaluma ambao kwa sasa wamefikia 22.
“Kwa sasa chuo kina jumla ya wanataaluma 22 ambao katika kipindi cha miaka 13 iliyopita wameendelezwa na na sasa wapo wenye shahada ya uzamivu, shahada ya uzamili na shahada ya kwanza,” alisema Jaji Mrosso na kuongeza kuwa chuo pia kimefungua tawi mkoani Mwanza.
Kuhusu hosteli za wanafunzi, Jaji Mrosso ambaye ni Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo amesema chuo chake kimekamilisha ujenzi wa jengo la hosteli ya wanafunzi wa kike inayojulikana kama “Mama Salma Kikwete” yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 278 na kufafanua kuwa ujenzi wa jengo la hosteli ya wanafunzi wanaume unaendelea na litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 320.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo hicho Jaji Ferdinand Wambali alisema kati ya jumla ya wahitimu 649 katika mahafali hayo, wahitimu wa Stashahada ya Sheria ni 386 na 263 ni wa Astashahada ya Sheria.
Aliongeza kuwa wahitimu wa Kampasi Kuu Lushoto wa Astashahada ya Sheria ni 183 ambapo kati ya hao wanaume ni 80 na wanawake 103. Wahitimu wa Astashahada ya Sheria katika Tawi la Mwanza ni 80 ambapo kati ya hao wanaume ni 35 na wanawake ni 45. Kwa upande wa wahitimu wa Stashahada ya Sheria ambao wote ni kutoka Kampasi Kuu Lushoto ni 386. Kati ya hao wanaume ni 197 na wanawake 189.
Kuhusu udahili katika mwaka huu wa masomo, Jaji Wambali alisema kimedahili jumla ya wanachuo wapya 610 wakiwemo wanachuo 256 kwa kozi ya Stashahada ya Sheria na wanachuo 249 kwa kozi ya Astashahada ya Sheria Kampasi Kuu Lushoto na wanachuo 105 wa Astashahada ya Sheria kwa Tawi la Mwanza.
Jaji Wambali pia aliwaeleza wageni waliohudhuria mahafali hayo kuwa kimeendelea na utaratibu uliokuwepo awali na baadaye kusitishwa kwa muda kwa kutoa mafunzo ya awali ya ufanisi wa lugha ya kiingereza kwa wiki tatu kwa wadahiliwa wapya kabla ya kuanza kwa mhula rasmi wa masomo.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto kilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 1998 baada ya mapendekezo ya taarifa za Tume na Kamati mbalimbali ikiwemo Tume ya Msekwa ya mwaka 1977 na Kamati ya Jaji Mark Bomani ya mwaka 1996. Taarifa hizi zilishauri kuanzishwa kwa chuo kitakachotoa mafunzo kwa maafisa na watumishi wa mahakama. Kwa sasa chuo kinatoa Stashahada na Astashahada.
No comments:
Post a Comment