Askofu
Amos Muhagachi akitoa tamko juu ya tuhuma mbalimbali dhidi ya kundi la
201 la wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo 03 Septemba, 2014 katika
Ukumbi wa Spika, Mjini Dodoma.
Mwenyekiti
wa kundi la 201 ya Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Dkt. Francis Michael
akikanusha kuhusu madai ya wajumbe wa kundi hilo kupewa rushwa kuhusu
mchakato wa Katiba Mpya.
Sheikh
Hamid Jongo akiviasa vyombo vya habari kutoa ushirikiano ili
kuhakikisha kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya unafanikiwa kwakuwa hata
wao (vyombo vya habari) unawahusu pia.
Askofu Donald Mtetemela akichangia mada wakati wa mkutano wa kutoa tamko kuhusiana na tuhuma mbalimbali dhidi ya kundi la 201.
Baadhi
ya wajumbe wa kundi la 201 pamoja na waandishi wa habari wakifuatilia
tamko hilo leo 03 Septemba, 2014 katika mkutano uliofanyika ukumbi wa
Spika Bungeni mjini Dodoma.(Picha zote na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma).
========= ======== ======
Wajumbe Kundi la 201 watoa tamko dhidi ya wanaolichafua Bunge Maalum la Katiba na Wajumbe wa kundi hilo.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
03/09/2014.
WAWAKILISHI
wa Taasisi za dini wa Bunge Maalum la Katiba toka wajumbe 201 wametoa
tamko lao dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazoendelea katika kulichafua
Bunge hilo ikiwemo baadhi ya wajumbe wa kundi hilo wakituhumiwa kudaiwa
kupewa rushwa.
Tamko
hilo limetolewa leo 03 Septemba, 2014 na viongozi wa kiroho akiwemo
Askofu wa Kikristo Amos Joseph Muhagachi pamoja na Sheikh Hamid Masoud
Jongo wakiwa wameongozana na Mwenyekiti wa kundi hilo la 201, Mhe. Dkt.
Francis Michael na wajumbe wengine wa kundi hilo, wakati walipofanya
mkutano na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Spika uliopo Bungeni
mjini Dodoma.
Akisoma
tamko hilo, Askofu Amos Muhagachi ambaye pia ni Mjumbe wa kundi hilo
amesema kuwa kama ilivyoelezwa hapo awali kabla ya kuanza kwa shughuli
za Bunge hilo, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu
kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na
ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu bila upendeleo.
Askofu Muhagachi ameendelea kusema kuwa wameshangazwa na kusikitishwa kuona
kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hilo
kwa wananchi unachafuliwa taswira yake, Bunge Maalum la Katiba
linachafuliwa, shughuli zake kuingiliwa na kupotoshwa na wajumbe wenzao
walioko nje ya Bunge hilo, makundi, taasisi na vyombo mbalimbali vya
habari, uhalali na ukweli wa shughuli za Bunge hilo unapotoshwa na
wananchi wanaaminishwa mambo yasiyo na ukweli.
“Upotoshwaji huu umezua mijadala mbalimbali katika jamii ya Watanzania bado unaendelezwa”, alisema Muhagachi. Aidha,
Muhagachi amezitaja baadhi ya tuhuma zinazotolewa na wajumbe wenzao
dhidi ya Bunge hilo na wajumbe wa kundi hilo zikiwemo.
“Bunge
Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu
walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hawapo, kwamba Kanuni za
Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo, Kwamba kinachojadiliwa
sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine na si Rasimu iliyotayarishwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Inadaiwa
na watu pamoja na Taasisi mbalimbali kwamba viongozi wa dini, wajumbe
wa Bunge hilo na wajumbe wa kundi la 201 kwamba wanapewa rushwa baadhi
ya Vyombo vya Habari vimeandika tuhuma hizi, pia madai mengine ni kwamba
wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache ikilinganishwa na hao
waliopo nje ya Bunge na tuhuma ya nyingine ni ile ya kwamba Bunge hili
lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.
“Tunapenda
kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato wa Katiba una hatua
tatu kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mpaka hivi sasa ni
hatua moja iliyokamilika, aidha hatua ya pili ndiyo inayoendelea na
hatua ya tatu bado haijaanza”, alisema Muhagachi.
Akitoa
tamko hilo, Askofu Muhagachi amesema kuwa wao kama wawakilishi wa
Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni
moja ya majukumu yao katika jamii, hivyo wameskitishwa na taarifa potofu
zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi na baadhi ya vyombo vya
habari.
“Tukiwa
kama wajumbe wa Bunge hili ambao tunafahamu kwa kina na tunaridhika na
kila hatua ya mchakato huu, tuna wajibu wa kusahihisha upotofu huu
unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na hali
halisi inayojiri hapa Bungeni, Watanzania msifadhaishwe na wala
msibabaishwe, hali ni shwari, mchakato unaendelea kwa amani na utulivu”,
alisisitiza Muhagachi.
Naye
Sheikh Hamid Masoud Jongo ameviasa vyombo vya habari kutilia mkazo
katika kutoa taarifa zilizosahihi ili mchakato wa Katiba uendelee kwa
amani kwani nao ni moja ya kundi la watu inayowahusu.
“Vyombo
vya habari vina nguvu ya kuhabarisha umma juu ya mambo mengi
yanayoendelea nchini, ni vema tukishirikiana sote kwa pamoja ili
kuhakikisha kuwa tunapata Katiba yetu kwani hata nyie Katiba hii
inawahusu hasa katika kudai haki na uhuru wa vyombo vya habari”, alisema
Sheikh Jongo.
Aidha,
Mwenyekiti wa wajumbe wa Kundi hilo la 201, Mhe. Dkt. Francis Michael
ameongezea kwa kukanusha suala la rushwa kwa wajumbe wake huku
akisisitiza kuwa wajumbe wake katika kundi hilo ni watu wenye heshima
zao hivyo madai hayo hayana ukweli wowote ule.
No comments:
Post a Comment