Kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na
wadai wengine wawili wamefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu dhidi ya
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe na wengine wawili wakitaka
kulipwa fidia ya Shilingi bilioni 500 kwa kashfa alizotoa kimaandishi dhidi yao.
Mbali na IPTL, wengine waliofungua kesi hiyo mnamo
tarehe 4, Septemba kupitia wakili Melchisedeck Lutema wa Asyla Attorneys na Kay Felician Mwesiga wa Bulwark Associates
Advocates, ni kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania Limited (PAP) na
Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni hayo mawili, Bw. Harbinder Sing Seth.
Wadai
hao watatu, miongoni mwa mambo mengine wanahitaji malipo ya fedha kutoka kwa
Bw. Kabwe na washtakiwa wengine watatu ambao ni mhariri wa gazeti la Raia Mwema,
Kampuni ya Raia Mwema na kampuni ya Flint Graphics, kuwa kama fidia itokanayo
na makala ya kuwachafua iliyochapishwa kwenye gazeti hilo, iliyosababishwa na
washitakiwa hao.
Pamoja
na hayo, pia wanahitaji tamko rasmi toka mahakamani kwamba makala iliyokuwa na
kichwa cha habari "Fedha za IPTL ni Mali Ya Umma"
iliyochapishwa katika kurasa wa 7 na 14 za gazeti la tarehe 13 Agosti, 2014
ilikuwa ni ya kupotosha na kuchafua kwa kudhamiria na kuhitaji washitakiwa
kuomba radhi kwa kuandika na kuchapisha katika kurasa za mbele kichwa cha
habari ya kuomba msamaha katika matoleo mawili mfululizo ya gazeti hilo.
Zaidi ya hayo, wadai waliiomba mahakama kuweka vizuizi
vya kudumu kwa washitakiwa, watumishi wao, wafanyakazi, washirika, wawakilishi
au watu wengine wowote wanaofanya kazi chini ya washitakiwa kwa uchapishaji,
kuchapisha au kusababisha kuandika na kuchapishwa kwa makala yoyote ya
kuwachafua.
Wadai walisema kuwa, IPTL waliingia mkataba na Shirika la Usambazaji Umeme
Tanzania (Tanesco) kuwa umeme unaozalishwa na mdai utakuwa ukinunuliwa na
kusambazwa na TANESCO kwa bei waliyokubaliana.
Inadaiwa kwamba, katika kurasa namba 7 na 14 za gazeti la Raia Mwema la
mwezi Agosti 13, 2014, Mbunge wa Kigoma Kaskazini aliandika, wakati mshtakiwa
wa pili, wa tatu na wa nne walihariri, kuchapa na kusambaza makala ambayo
ilikuwa ni ya uongo na yakuwachafua wadai.
Katika hati
ya mashtaka, wadai walisema kuwa makala hiyo ilikuwa na maneno yafuatayo
yaliyokuwa si ya ukweli na ya kuwachafua wanaodai; “Kwa mara nyingine, serikali
kupitia viongozi wake akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wamedai kwamba
kiasi cha Dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika
“Tegeta Escrow Account’ si mali ya serikali na hivyo si mali ya umma. Akaunti
hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na kampuni ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL).”
Ilidaiwa
kuwa pasingekuwa na nia ya dhati ya kumchafua mdai, mdaiwa
hasingechapisha, na kusambaza maneno yaliyonukuliwa kama angefanya juhudi za
kuthibitisha ukweli kutoka upande wa pili (kwa mdai) au kutoka kwa maafisa
husika wa serikali ambao wangethibitisha kwamba:
“kiasi cha
fedha kilichowekwa kwenye akaunti ya Escrow ilikuwa ni dola za kimarekani
122,000,000.00 na siyo dola za kimarekani 250,000,000.00 kama ilivyodaiwa na
mshtakiwa,” ilisomeka sehemu ya hati ya madai.
Kwa mujibu
wa wadai, Tanesco kamwe haikuwa sehemu ya makubaliano ya Escrow kama
ilivyodaiwa na washtakiwa. “Fedha
ziliwekwa katika makubaliano ya Escrow na siyo kama fedha za umma lakini ni kwa
kutokana na mgogoro wa malipo yaliyotakiwa kufanywa na Tanesco kwa IPTL.
“Madai kuwa
fedha hizo ziliwekwa kama fedha za umma ni za uongo za kuupotosha umma na
kuwachafua wadai kuwa ni wabadhilifu wa fedha za umma”, sehemu ya hati ya madai
ilisomeka.
No comments:
Post a Comment