Mkurugenzi wa Idara ya Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Jamala Adam Taib akimueleza Waziri wa Afya Mh. Rashid Seif kazi zinazofanywa na Idara hiyo alipofika ofisini kwake kuanza ziara ya kutembelea Hospitali hiyo.
Waziri wa Afya Mh. Rashid Seif akiongozana na Naibu wake Mh. Mahmoud Thabit Kombo wakitembelea eneo la Hospitali ya Mnzammoja katika ziara yake ya kutembelea Hospitali hiyo.
Mkuu wa kitengo cha maradhi ya kisukari katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja Dkt Miskia Ali akitowa maelezo kwa Waziri wa Afya juu kadhia ya maradhi hayo.
Waziri wa Afya akipata maelezo ya shughuli za Maabara kutoka kwa mtaalamu wa Maabara wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt. Marijani. Picha na Makame Mshenga wa Maelezo Zanzibar.
NA RAMADHANI ALI – MAELEZO ZANZIBAR
Mkurugenzi wa Idara ya Hospitali ya Mnazimmoja inayojumuisha Hospitali tatu, Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja, Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo chekundu na Hospitali ya Wazazi ya Muembeladu Dkt. Jamala Adam Taib amesema kazi kubwa inayofanywa na Idara hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2010 ni kuimarisha Hospitali ya Mnazimmoja ifikie kiwango cha Hospitali ya rufaa.
Amesema hatua zinazochukuliwa na Idara ni Kuimarisha miundo mbinu, kusomesha wataalamu wa fani tofauti za afya, kuimarisha uchunguzi wa maradhi na kuhakikisha madawa yanapatikana katika Hospitali hiyo.
Dkt. Jamala amemueleza Waziri mpya wa Wizara ya Afya Rashijd Seif Suleiman alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali hiyo kuangalia utendaji wa kazi na changamoto zinazoikabili Hospitali hiyo.
Amesema majukumu yote waliyopangiwa katika kuimarisha Hospitali Kuu ya mnazimmoja wamefikia hatua nzuri na hivi sasa wananchi wamejenga matumaini makubwa kutokana na huduma zake.
Dkt. Jamala amesema Idara ya Hospitali ya Mnazimmoja inawafanyakazi 800 wakiwemo madaktari bingwa 14 na Serikali inaendelea kusomesha wataalamu wa fani mbali mbali ambapo wanafunzi 200 wa fani ya udaktari wapo vyuoni .
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Dkt. Jamala amesema bado inakabiliwa na ufinyu mkubwa wa bajeti na mageuzi yanayoendelea ya kuifanya Hospitali hiyo iwe inajitegemea.
“Changamoto hizi hata hivyo haziathiri malengo yetu ya kuwapa wananchi matumaini ya kupata huduma bora katika Hospitali hii,” Dkt Jamala alimueleza Waziri wa Afya.
Msaidizi Mganga Mkuu wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Dkt. Muhidini Abdalla Muhamed amemueleza Waziri wa Afya ambae alifuatana na Naibu wake Mahmoud Thabit Kombo kwamba kliniki ya meno ya Hospitali hiyo inavifaa vya kisasa kutoka Shirika la MCW la Marekani na kuifanya kuwa kliniki bora zaidi kuliko hospitali nyengine za Zanzibar.
Amewahakikishia wananchi kwamba huduma za matatizo yote ya meno zinapatikana kwenye kliniki hiyo na kuwataka wananchi kutokuwa na wasi wasi na waendelee kuitumia.
Katika kitengo cha maradhi ya kisukari daktari msaidizi wa maradhi hayo Dkt. Miskia Ali Mohd alimueleza Waziri kwamba maradhi hayo yanaongezeka kwa kasi na kumekuwa na upungufu mkubwa wa dawa za maradhi hayo.
Amesema tatizo jengine linalokabili kitengo hicho ni upungufu wa chakula cha wagonjwa wa kisukari wanaolazwa katika Hospitali hiyo ambacho kinatakiwa kiliwe sambamba na matatibabu wanayopatiwa ili dawa wanazotumia zifanyekazi kwa ufanisi.
“Naiomba wizara ifanye juhudi za kuhakikisha dawa za maradhi ya kisukari na chakula maalum cha wagonwa wanaolazwa vinapatikana kwani maradhi haya yamekuwa hatari zaidi hata kwa watoto wadogo, ”alisisitiza Dkt. Miskia.
Waziri wa Afya kwa upande wake amewataka viongozi wa Idara hiyo kuimarisha umoja na mshikamano na watendaji wao ili kufanikisha malengo yaliyowekwa ya kuwahudumia wananchi na kuwapa huduma nzuri.
Ameupongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuanzisha utaratibu maalum wa kuangalia wagonjwa waliolazwa ambao umepunguza msongamano wa watu katika mazingira ya sehemu hiyo.
No comments:
Post a Comment