Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB (Nzega), Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, akiongea na Waandishi wa Habari Kutangaza Nia ya Kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwaka 2015 Kwenye Ukumbi wa Zanzibar, Hyatt Regency, The Kilimanjaro Hotel, Dar es salaam, Siku ya Tarehe 7 Septemba 2014.
Utangulizi
Nianze
kwa kuwashukuru viongozi wa dini kwa dua za utangulizi.
Pia
nitume salamu zangu za rambirambi kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Eng. Evarist
Ndikilo na ndugu, jamaa na marafiki wa watu waliopoteza maisha kutokana na
ajali mbaya ya gari iliyotokea juzi. Pia nitumie fursa hii kutuma salamu zangu
za rambi rambi kwa Inspekta Mkuu wa Jeshi la polisi, IGP Ernest Mangu, ndugu wa
marehemu na askari wote wa jeshi la polisi kutokana na uvamizi wa kituo cha
polisi kule Bukombe. Na pia naomba nitumie fursa hii kumpa pole Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi, CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad kwa kupata ajali eneo la Misungwi, Mwanza.
Ndugu
zangu mlioko hapa, ni heshima na furaha kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Awali
ya yote nimshukuru Mwenyezimungu kwa kutujaalia uhai na kutukutanisha hapa siku
ya leo. Pili niwashukuru nyote mliofika hapa kuja kunisikiliza. Niwashukuru
zaidi waandaaji wa Mkutano huu kwa kujitoa na kwa namna ya kipekee niwashukuru
wazazi wangu, mke wangu na wanangu Sheila, Hawa na HK Jr kwa uvumilivu na kwa
kuendelea kunitia nguvu ya kusonga mbele.
Leo
nitasema neno zito kidogo, kama nilivyoahidi siku chache zilizopita. Neno
nitakalolisema hapa litabadilisha sura ya historia yangu milele. Ninawashukuru
nyote kwa kuitikia wito wa kuja kuwa mashuhuda wa namna historia itakavyoendelea
kuandikwa hapa.
Kinachotokea
hapa leo hii kina maana kubwa sana kwa watu wenye historia inayofanana na mimi.
Wale ambao wameyajua maisha ya shida na kukosa uhakika toka wakiwa tumboni mwa
wazazi wao kutokana na hali za uchumi wao. Wale wenzangu na mie ambao kesho yao
haina uhakika; wale ambao wengine hupenda kuwaita ‘wanyonge’, ambapo mimi
nikijitazama nilikotoka husema, hapana, hawa si wanyonge bali ni ‘simba
aliyelala.’
Shukrani Kwa Urithi Toka kwa Waasisi na Wazee Walionitangulia
Mimi
ninayezungumza hapa nimeyajua maisha ya mtu mnyonge na maskini kwa kuyaishi na
si kwa kusoma ama kusikia. Ninajua mtu akiongelea njaa anamaanisha nini,
sihitaji kufundishwa, najua. Nasema haya maana naujua ugumu wa kumuelewesha mtu
anayekula milo mitatu kwa siku, tena ya kujipakulia kuwa kuna wengine wanakula
pilau sikukuu hadi sikukuu. Ni ngumu sana kumuelewesha mtu wa aina hiyo kuwa
wapo watoto wanaogombania chakula kwenye sahani moja. Maana kila siku yeye
huwashuhudia watu wa dunia anayoishi
wakihangaika kutembea umbali mrefu ili wapunguze vitambi na wakae kwenye
‘shape’ na hajui kama kuna watu wanatembea umbali mrefu ili kutafuta chakula
wasukume siku!
Ni
katika nchi chache sana duniani, mtoto mwenye historia ya maisha kama yangu,
aliyewahi kutembea mitaani akiuza karanga, Big G, maandazi na jerebi ili
kusaidia wazazi kupata chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota ndoto
ya kuwa Rais wa nchi yake. Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza
kuwa Daktari.
Hii
inamaanisha jambo moja kubwa, kwamba misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa
na waasisi wa Taifa letu haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na
inafanya kazi. Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ama wa kiongozi, ndiyo
uoneshe kipaji chako. Inadhihirisha kwamba, ukipigana ndani ya Tanzania
unafanikiwa!
Hili
peke yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kusonga mbele zaidi –
nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu, kuwa sote
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa sawa bila kujali
nani anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni
lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania
itakayodumu kwenye misingi hii. Kwamba, ndani ya Tanzania, si lazima mtoto wa
mama ntilie awe ‘baba-ntilie’ – anaweza kuwa mmiliki wa hoteli kubwa ya
kitalii!
Kwa
namna ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Taifa
letu kwa kuzilinda tunu hizi, maana ninaamini kuwa hatuwezi kuizungumzia kesho
bila kukumbuka shida na raha tulizopata jana.
Leo
nimefika hapa kwa sababu chama changu kina mfumo mzuri ulioasisiwa na Mwl. Nyerere
na umelindwa na wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi tumeukuta. Leo nimefika
hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri
Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Chama changu kuamua kuwa
nami nina haki ya kuwa Mbunge. Na leo nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi
hiyo hiyo itakayotoa uongozi wa Taifa letu katika awamu ijayo.
Babu
yangu mzaa baba aliishi Kijijini Goweko, eneo la Mlimani, na alikuwa mfugaji
mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi maisha ya
heshima kubwa pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa japokuwa Babu
yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU na baadaye
CCM katika ngazi ya Kata.
Babu
yangu mzaa mama alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora
School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alifanya
kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na alishiriki harakati za
kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU. Babu yangu aliamini
kuwa “binadamu
wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili heshima na kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake”, na kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo
kujitawala wenyewe dhidi ya utawala dhalimu wa wazungu ilikuwa ni haki yetu;
pia aliamini katika elimu, na hivyo alifanya juhudi kusomesha mabinti zake;
mama yangu aliishia kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini
kuwa Tanzania ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi
kuitekeleza kwa ajili ya mabinti zangu, Sheila na Hawa, na kaka yao, HK Jr. Ninaamini
kila mzazi wa kizazi changu ana ndoto inayofanana na yangu kwa watoto wake.
Ninaamini
historia ya maisha yangu siku moja itaandikwa na itawasisimua na kuwapa matumaini
makubwa vijana na watoto chini ya miaka 35 ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya
watanzania wote. Mmoja wa wajukuu zangu ataisoma na kusema ‘doesn’t it get
better than this?’
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya
maisha yangu ni mfano hai wa historia ya maisha ya watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo kwa kuwa
mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi vilivyonitangulia. Naliona
jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la
kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.
Mahusiano ya Watu na Serikali Yao
Kazi yangu imenifikisha sehemu
nyingi sana za nchi yetu – vijijini na kwenye majiji, imenikutanisha na watu wa kila
aina – matajiri kwa maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu
hawa anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa
kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda
kwa wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa matabibu wenzangu
pale hospitali ya Taifa Muhimbili, ama kwa wafanyabiashara na wachuuzi pale
sokoni Kariakoo, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na
wachache wasio waadilifu.
Watanzania
wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda
kule Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia
hawategemei Serikali itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua
Serikali haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi
kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo siku zote. Wanachohitaji wao ni kujengewa
mazingira wezeshi kushiriki shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe
namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija
na ufanisi, waelekezwe wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu,
wanahitaji, mwisho wa siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila
kudhulumiwa wala kucheleweshewa malipo.
Watu
hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote.
Lakini wanaamini kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu
vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo
namna tunavyoendesha uchumi wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili
muelekeo mzima wa maisha ya baadaye ya watoto na wajukuu zetu. Tutaiondoa Tanzania
miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani
kubwa kabisa kwamba, tunaweza kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza
kufungua milango ya maisha bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa
kila mtanzania kuishi kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote
ule kuanzia leo. Tutaweza kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye
kazi akitumaini na kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa
naye ataishi kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu,
kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, tukibadili namna
tunavyoendesha serikali yetu, haya ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo
yanayowezekana.
Watanzania wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi
sahihi wa vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye
uchumi wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya
nchi yetu kwa sasa na baadaye, tutafanikiwa.
Tamko Rasmi la Nia ya Kugombea Urais na Sababu
Ndugu zangu nyote mliopo hapa, natangaza rasmi, kuwa
ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa,
kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na
utayari wangu. Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa
kina: mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto za kizazi chetu; uwepo
wa fursa ya kugombea na kushinda uchaguzi ujao; uwezo wangu wa kuchambua mambo,
kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, na kuchukua hatua za utekelezaji na
kusimamia utekelezaji; uadilifu na uzalendo wangu; na zaidi nia yangu ya kuwa
sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika nchi
yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu ya mabadiliko ya namna tunavyochagua
vipaumbele vyetu kama Taifa na namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri
tunayojipangia.
Ninatangaza nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa
watanzania wanipime na kunitazama mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa kuwa
nitapimwa na kuungwa mkono ama kutoungwa mkono, si kwa rangi ya ngozi yangu, si
kwa jinsi yangu, si kwa umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye jamii, ama
dini yangu, ama kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa rekodi yangu, sifa,
utayari, dhamira na uwezo wangu, kama mtanzania.
Natangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya
Muungano ili nipate fursa ya kuukimbiza uchumi wetu kutoka hapa tulipo kwenda
mbele zaidi. Mimi ni mwanamabadiliko, ninaamini nikipewa fursa, nitashirikiana
na watanzania wenzangu na kwa pamoja tutaunyanyua uchumi wetu kutoka kiwango
cha kukua cha tarakimu moja kwenda kile cha tarakimu mbili kwa miaka yote ya
uongozi wangu. Ninaamini tutaweza kwa pamoja kuukuza mchango wa kilimo kwenye
GDP kutoka asilimia 4.2 kwenda zaidi ya asilimia 6. Tukiyafanya haya naamini
tutakuwa tumezalisha ajira nyingi zaidi kuliko leo.
Ninaamini katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka
50 ya kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuna kila sababu ya kuwa Taifa la
dunia ya kwanza, viongozi waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha
Tanzania kwenye matamanio yetu. Kizazi chetu cha viongozi kina jukumu na wajibu
wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye ahadi inayotokana na ndoto za waasisi wa
Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi
wowote ule, maana naamini tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa
na watu wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho: kupigana
na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa
vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa mambo ambayo
kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na umakini wa hali ya
juu.
Na
ndugu watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa tuna kazi ya ziada ya kufanya
mbele yetu. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo
tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye
kuchukua hatua za kutenda.
Kutathmini na Kuwapima Watia Nia
Nyote
mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la kututazama kwa
ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote;
tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa tajwa, na
wale wanaosubiri kuoteshwa, ili wakati muafaka ukifika muwape taarifa sahihi
watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa kuliongoza Taifa hili kuelekea
Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuwa
Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari wake wa
kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na kuamua kwa busara kutumia nguvu za
kijeshi pale inapolazimika baada ya kupima na kuchambua aina nyingine zote za
kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru,
haki na usawa na wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa na Katiba yetu, pia
asili na historia yetu, anayeamini katika haki ya kuabudu lakini asiyekuwa
tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana na dini zao.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya
kupata huduma bora za afya, elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri
wetu, kama wanavyopata mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata
wafanyabiashara na wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa
watanzania wote wanapata haki hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja
zao kijamii.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kila
mtanzania ana bima ya afya na ya maisha, na kwamba bima hiyo inampatia uhakika
wa kupata huduma bora za afya popote na kwa wakati anapozihitaji bila kumbagua kwa
hali yake. Kwamba, itakuwa mwisho sasa, ndani ya hospitali moja, kuwa na wodi
nzuri wanazolazwa ‘wateule wachache waliochangia bima ya afya’ na kuwa na wodi
za ‘ilimradi’ tu wanazolazwa wengine.
Kuwa, ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru
na kujitegemea kwenye masoko na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa
ndani, kujitegemea kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula,
kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili
tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za hasara na faida
za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu. Ili tulinde thamani ya
fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi
bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu?
Kuwa, ni nani kati yetu anaichukia rushwa, anachukia
wakwepa kodi wa makampuni makubwa ya kimataifa yanayovuna raslimali za nchi
yetu na hayalipi hata kodi tu! Kwamba, ni nani atalinda raslimali za nchi yetu
bila shaka. Kwamba, ni nani kati yetu atahakikisha tunapata hisa za kutosha
kutokana na uchumi wa raslimali za madini, vito, mafuta na gesi? Kwamba, ni
nani kati yetu atailinda ardhi ya watanzania na kuhakikisha haivamiwi na wasaka
ardhi kutoka nje ya Taifa letu, kwamba atahakikisha ardhi inabaki kutumiwa kwa
faida ya wakulima na wafanyakazi wa nchi yetu?
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kupambana na
changamoto za usafiri na usafirishaji, kuwa ataweza kuongeza tija na ufanisi
kwenye bandari zetu, na ataweza kufufua usafiri wa reli, ndege na meli?
Kuwa, ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi
zaidi ya watanzania walio wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake,
mtazamo wake, ndoto zake, zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji
sahihi la watanzania?
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye
uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi. Mtu ambaye ukimtazama
kwa nje ana mvuto na analeta matumaini kwa watanzania, ambaye ukimcheki hivi
unasema ‘he is just a cool guy’, lakini kwa ndani anaumia, anaungua moyo wake
kwa ajili ya Tanzania yetu.
E Pluribus Unum
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!
Kwamba;
Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa
salama kama wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka.
Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu pia, na
haiishii hapo tu, matatizo hayo si yangu na huyo mwenzangu tu, ni yetu sote
kama jamii.
Hivyo:
kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule
Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu.
Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa
mauaji ya kule Sombetini, Arusha, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo
yangu.
Mzee Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto
wake akakosa msaada na yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja
kwa siku ili asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo
babu yangu.
Mama John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage,
na ana wateja wengi mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Kariakoo;
akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na
kumwagiwa chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya
biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye
si mama yangu.
Kama kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule
Mrijo Chini, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mwanangu.
Kato na Kokugonza ni wanandoa wapya, wanaishi
kijijini kule pembezoni ya Katerero, Koku amepata ujauzito na amefikia kujifungua,
kwa hali yake na namna mtoto alivyokaa tumboni anapaswa akajifungulie hospitali
ya wilaya ili ikibidi kufanyiwa operesheni, basi afanyiwe; ikitokea uchungu
umeanza ghafla na akachelewa kufika hospitali ya wilaya sababu ya miundombinu
mibovu na kukosa ambulance mapema, akapoteza damu nyingi hadi umauti ukamkuta
yeye na mwanae, ni jambo lenye kuuma sana, si tu kwa Kato na wanafamilia wao,
bali na mimi pia linaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mdogo
wangu.
Bwana Kalumanzila ni mmachinga wa nguo za mitumba
mitaani. Yeye huchukua nguo zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko
la Karume, akiuza anachukua kifaida kidogo kinachozidi hapo juu na kurudisha
pesa ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata
inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake. Akifukuzwa barabarani na
akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na analazimika kumtumikia bosi
mwenye mali mpaka atakapofidia mali iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na
madhila anayoyapata bwana Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata
kama yeye si mjomba wangu.
Fikra hizi zinatokana, kwa kiasi kikubwa, na funzo
nililopewa na babu yangu wakati nikichagua kozi ya kusoma chuo kikuu, ambapo
nilipata kitendawili cha kuchagua kati ya kwenda kusoma udaktari ama sheria;
aliniambia kuwa, “ni bora ukachagua kusoma udaktari maana utapata baraka za
Mungu kwa kujitoa kuwasaidia watu walio na shida…” na akaendelea kusema kuwa
“…kwenye maisha yako ikitokea ukapata mali ama ukawa na nafasi kubwa ya kuamua
juu ya mustakabali wa maisha ya wengine, usisahau kumshukuru Mungu kwa kuwatendea
yaliyo mema wenzako na Mungu atazidisha Baraka zake kwako.” Leo miaka zaidi ya
15 baadaye naona maneno yake bado yanaishi moyoni mwangu. Maisha yangu yote
nimeikumbatia falsafa hii. Nimeifanya kuwa dira ya utumishi wangu kwa wenzangu
na kwa ulimwengu.
Falsafa hii imenifanya nishindwe kuvumilia
unyonyaji, ukandamizaji, uzembe, wizi na ubadhirifu wa baadhi ya wenzetu
walioshindwa kudumu kwenye njia ya kutoa haki, uadilifu, uwajibikaji na
utumishi uliotukuka.
Tamati
Ndugu wanahabari, Tarehe 4, Agosti 2014, Rais
Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha Maendeleo ya Dunia (Center for Global
Development) alisema: “…Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi
masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu
kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi
wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais wa
kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia
miaka ya awali ya uongozi wangu kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Kuna
watu wanadhani uwepo wa mfumo wa demokrasia imara, ama mfumo unaotoa uhuru na
haki kwa watu wetu, ama uwepo wa mfumo wa soko huria, ama utandawazi ni
muarobaini wa kudumisha amani yetu, mimi nasema, tunahitaji zaidi ya uhuru,
zaidi ya demokrasia, zaidi ya mifumo ya utandawazi, ama ya soko huria ili tudumishe
amani na mshikamano wetu – tunahitaji uhuru kwenye uchumi wetu. Tunahitaji
uhuru kwenye mifuko ya kila mtanzania. Uhuru wa kuchagua anachotaka kula, kuvaa
ama huduma kwa ajili yake na familia yake. Tunahitaji mabadiliko ya kifikra ili
kuleta mapinduzi ya uchumi tunayoyatarajia. Tunahitaji kupigana kuhakikisha
kila mtanzania anajitegemea kiuchumi. Hapo ndipo tutasema sasa tuna uhuru
kamili.
Mungu awabariki sana. Mungu ibariki Tanzania. Mungu
ibariki Afrika.
No comments:
Post a Comment