Wednesday, May 7, 2014

Dk. Kigwangala aitaka TAMISEMI kuwashirikisha Wananchi kubuni Vyanzo vya Mapato

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Hamis Kigwangala amezitaka Sekretarieti za mikoa na halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba inawashirikisha wananchi katika maandalizi ya bajeti kubuni vyanzo vya mapatao.

 Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bungeni leo kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2013, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Kigwangala amesema pia wananchi washirikishwe katika utungaji wa sheria ndogo za ukusanyaji ili kurahisisha zoezi la makusanyo bila manung’uniko.

Amesema ushiriki wa wananchi pia utasaidia katika zoezi zima la kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa pale ambapo Serikali kuu pamoja na Serikali za Mitaa zitakapokuwa zinatoa mchango wake kikamilifu katika miradi husika na hivyo nguvu ya wananchi kutopotea.

Dk Kigwangala ametanabaisha pia kamati yake inazitaka Halmashauri zote nchini kuacha kuwabughudhi na kuwanyanyasa wananchi wenye kipato cha chini kabisa kwa kuwalazimisha walipe kodi kubwa kuliko hata mtaji na thamani ya mali zao wanazouza, hususan wafanya biashara ndogo ndogo.

Ametolea mfano wa wafanyabiashara anaotembeza bidhaa za mikononi maarufu wamachinga na mama lishe, ambao mara kadhaa wamekuwa wakinyang’anywa biashara zao na migambo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kama wezi ndani ya nchi yao na migambo hao kinyume kabisa na maadili ya kiafrika wakizitupa, wakihodhi ama kumwaga chini.

“Vitendo vya kinyama dhidi ya watu wa aina hii ni vingi na kwa namna yoyote ile havikubaliki katika Taifa letu na hivyo basi Kamati inaitaka Serikali itekeleze Sera yake nzuri ya kuwalinda na kuwawezesha wananchi wenye uchumi wa chini kwa vitendo ili nao wajikwamue na umaskini, wakidhi mahitaji yao na waendelee kuiheshimu na kuipenda nchi yetu na Serikali yake,” alisema.

Amesema Kamati inaziagiza Serikali kutoa maelekezo sahihi kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuwajengea mazingira mazuri, wezeshi na ya kisheria wafanyabiashara wote wanaohangaika kutafuta mkate wao wa kila siku kwa uchuuzi wa bidhaa zinazohesabika kwa macho tu bila matumizi ya nguvu ili kulinda haki ya wananchi kujifanyia kazi.

Vilevile, Dk Kigwangala amezitaka Halmashauri zote nchini katika bajeti ya mwaka huu kutenga asilimia 60 ya makusanyo yake ya ndani  kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Dk Kigwangala alisema Kamati inaendelea kusisitiza kwamba sekretarieti za mikoa zikiongozwa na wakuu wa mikoa, kuimarisha ufuatiliaji kwa kuzisimamia halmashauri na kuhakikisha kuwa fedha za miradi ya maendeleo zitokanazo na makusanyo ya ndani na zinatoka nje zinatumika kuwaletea wananchi maendeleo.

Kamati yake pia imependekeza Serikali kuweka mikakati madhubuti ya ukusanyaji wa mapato ya majengo katika majiji, manispaa, miji na miji midogo, kwani fedha nyingi zinapotea kwa kutokusanywa kwa kodi hii.

Amezitaka Halmashauri kutumia mapato yake ya ndani kukamilisha miradi ya ujenzi wa majengo ya madarasa, majengo ya zahanati na vituo vya afya, nyumba za walimu, nyumba za wauguzi vijijini, mabarabara ya vijijini, kuchimba visima.

Dk Kigwangala alisema serikali kutegemea hela za wahisani hakuwezi kusaidia kuwapatia wananchi wake maendeleao.

No comments: