Thursday, May 8, 2014

Jiji la Abuja, Nigeria

Jiji la Abuja, ambao ndilo makao makuu ya nchi ya Nigeria, lipo katikati ya nchi hiyo kubwa na tajiri yenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi. Mji huu ulijengwa miaka ya 1980, na ukatangazwa rasmi kuwa makao makuu ya nchi December 12, 1991, kuchukua nafasi ya jiji la Lagos, ambalo linabakia kuwa ni jiji lenye wakazi wengi kuliko sehemu yoyote katika Nigeria. 
Kama ilivyo ada, Abuja limekua siku hadi siku huku likishuhudia ongezeko kubwa la watu kiasi cha serikali kulazimika kuanza kujenga miji ya pembeni (satellite cities) katika maeneo ya Karu, Suleja, Gwagwalanda, Lugbe, kuje na sehemu zingine ndogondogo ambako mji huo unaelekea.
Inakadiriwa mji wa Abuja una wakaazi takriban milioni tatu, hivyo kuwa mji wa nne wa Nigeria wenye wakaazi wengi, wa kwanza ukiwa Lagos (milioni 21), Kano na Ibadan. Inasemekana mwaka 2006 Lagos ilikuwa na watu milioni 17.5, kwa mujibu wa sense iliyofanyika mwaka huo. Kwa sasa, ongezeko la watu likiwa asilimia 3.2 kwa mwaka, jiji hilo sasa lina wakaazi milioni 21. 
Kwa Tanzania, jiji la Dar es salaam lina wakaazi 4,364,541 kwa mujibu wa matokeo ya sense ya watu na makaazi ya mwaka 2012. 
Jiji  la Dar liliacha kuwa na hadhi ya makao makuu ya nchi mwaka 1974, na mji wa Dodoma kuchukua nafasi hiyo. 
Historia ya mji wa Abuja  inaanza miaka ya 1970 wakati wa migogoro ya kidini na kikabila ilipokuwa kileleni. Ndipo mikakati ikawekwa kuwa na makao makuu ya nchi katikati ya nchi ambapo patakuwa huru na rafiki kwa kila upande unaopingana. 
 Sababu ingine ya kuhamishia makao makuu hapo Abuja ambako awali palikuwa na kijiji kidogo na misitu, ni msongamano kutokana na wingi wa watu katika jiji la Lagos. 
Mpango uliotumika ni kama ule wa Brazil ambao walichagua kujenga makao makuu yake Brasilia, kutoka Rio de Janeiro. Jiografia ya Abuja inajengeka kuanzia mwamba mkubwa uitwao Aso Rock, wenye ukubwa wa mita 400. 
Mji huu pia una sifa za kuwa mji uliopangika kwa ubora wa hali ya juu , tajiri na ghali sana kuishi barani  Afrika.











No comments: