Na Saidi Mkabakuli
Wakazi wa mkoa wa Mbeya na vitongoji vyake wameanza kufaidi matunda ya uwekezaji wa kimkakati uliobainishwa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011 – 2016) kupitia ujenzi wa miundombinu ya maji, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, pamoja na ujenzi wa jengo la Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Rufaa iliyopo mkoani humo.
Hayo yalibainika wakati Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara ya ukaguzi wa baadhi miradi ya maendeleo kushuhudia hali ya utekelezaji wa miradi iliyopo mkoani humo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo mmoja wa Kiongozi wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri anayeshughulikia Huduma za Jamii na Maendeleo ya Idadi ya Watu, alisema kuwa katika kutambua changamoto zinazowakabili wakazi wa mkoa huo, Mpango wa Maendeleo uliweka bayana uanzishaji na uendelezaji miradi ya maendeleo ili kutoa huduma za kijamii kwa Watanzania wote.
“Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa ikiwemo miradi hii tunayokagua leo,” alisema Bibi Mwanri.
Bibi Mwanri aliongeza kuwa kwa kutambua changamoto za uhitaji wa maji kwa baadhi wakazi wa vijijini wa mkoa wa Mbeya, Serikali iliwekeza zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya uwekezaji katika miradi ya maji ya Mradi wa Maji ya Mtiririko Kijiji cha Igurusi na Mradi wa Maji wa Iwalanje.
“Hii ni baadhi ya miradi inayonufaisha wakazi wa mkoa huu ambayo tumetembelea. Kukamilika kwa Miradi hii kumetoa suluhisho la adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Mbeya na vitongoji vyake pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohudumiwa na Miradi hii,” alisema.
Naye Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara ambaye alikuwa kiongozi mwenza wa ukaguzi huo, alisema kuwa maendeleo ya miradi hiyo ni ishara tosha kuwa wakazi wa Mbeya na vitongoji vyake wataanza kuneemeka na uwekezaji huo wa Serikali kwa kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo kupitia miradi hio.
Akitolea mfano wa uwekezaji katika Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Prof. Rutasitara alisema kuwa kukamilika kwa Uwanja huo ambao umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 70, sio tu kutaongeza shughuli za kiuchumi mkoani Mbeya bali kunatoa fursa za kufungulia za kuwezesha ukuaji mpana wa uchumi wa nchi.
“Uwanja wa Songwe unatoa fursa za misingi wa uchumi kwa watu walio wengi, hizi ni juhudi za makusudi za Serikali za kuondoa vikwazo vilivyopo hivi sasa katika kutumia utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo mkoani Mbeya,” alisema Prof. Rutasitara.
Serikali imeaandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukiwa na lengo la kuwa na mfumo madhubuti wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Mpango huu utadumu kwa mwaka 2011/12 - 2015/16 na utakuwa wa kwanza katika mfululizo wa mipango mitatu itakayotekelezwa kwa awamu. Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Kiongozi wa Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri
(Wapili Kushoto) akipata maelezo ya maendeleo ya Mradi wa Majiya Mtiririko
Kijiji cha Igurusi kutoka kwa Mshauri wa Mradi huo Mhandisi Kimambo.
Wakaguzi walipata bahati ya
kujionea chanzo cha maji hayo kutoka nje kidogo ya Kijiji cha Igurusi.
Timu ya ukaguzi pia ilikagua maendeleo ya Tanki la kuhifadhia maji la
mradi huo. Pichani, Kiongozi wa Ukaguzi, Bibi Florence Mwanri akipanda ngazi
kwenda kujionea maendeleo ya ujenzi wa Tanki.
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi huku wakaguzi hao wakikagua. Tanki
hilo lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita laki tano ambalo limeshakamilika kwa
asilimia 90. Hadi kukamilika kwake Mradi utagharimu jumla ya Shilingi zaidi ya
Milioni 830.
Naibu Katibu Mtendaji wa
Tume ya Mipango (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara (Aliyenyanyua Mkono)
akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa Mradi wa Maji wa Iwalanje wakati Timu ya
Ukaguzi ilipotembelea Mradi huo.
Mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi milioni 273, ambapo mpaka sasa
Mradi unahudumia zaidi ya kaya 2, 506.
Viongozi wa Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Prof. Longinus
Rutasitara (Wanne Kushoto aliyenyanyua mkono) na Bibi Florence Mwanri (Watatu
Kushoto) wakipata maelekezo ya Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe.
Pichani ni ujenzi wa sehemu wa kukaa abiria ukiendelea.
Meneja uwanja wa ndege wa Songwe jijini Mbeya, Eng. Valentino Kadeha (Kulia) akitoa maelekezo
kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango ilipotembelea Mradi huo. Kwa Mujibu wa Mhandisi Kadeha Uwanja
huo umeshakamilika kwa aslimia 70 na utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria zaidi
ya 300 kwa saa.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa wa
hospitali ya rufaa Mbeya Dr Sankey (Wapili Kulia) akieleza changamoto
zinazozikabili Hospitali hiyo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango pia ilipotembelea Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya.
Aliyeambatana nae ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Humphrey
Kiwelu (Kulia).
Kiongozi wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (Mwenye nguo nyeusi) akionja maji kutoka moja ya
njia za kusambazia maji ya Mradi wa Maji wa Iwalanje. Kukamilika kwa Mradi huo
kumetoa suluhisho la adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Kijiji
cha Iwalanje na Taasisi mbalimbali za Serikali zinazohudumiwa na Mradi huo.
Ukaguzi wa Hospitali.. Kwa
kutambua umuhimu wa afya kwa maendeleo ya nchi, Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
pia ilitembelea Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya. Timu hiyo ilishuhudia
maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kitengo cha Dharura (linaloonekana nyuma).
No comments:
Post a Comment