Friday, January 31, 2014

MH. PINDA AZINDUA RASMI MAPITIO YA MFUMO WA UWEKEZAJI TANZANIA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda (kulia) akikata utepe kuzindua ripoti ya hali ya Uwekezaji nchini Tanzania leo jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imegusia sera na na maendeleo ya uwekezaji nchini pamoja na changamoto zinazokwamisha ustawi wa uwekezaji Tanzania.
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akionyesha vitabu vya ripoti ya Uwekezaji Tanzania kwa wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya Uwekezaji nchini Tanzania leo jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akimkabidhi kitabu cha Ripoti ya hali Uwekezaji nchini Tanzania Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dkt. Reginald Mengi (kulia) leo jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda akisalimiana na wadau wa uwekezaji mara baada ya kuzindua ripoti kuhusu hali ya uwekezaji nchini Tanzania.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dkt. Reginald Mengi (kulia) akizungumza jambo na Bi. Marry Hobbs Mwakilishi wa masuala ya Kilimo na Maliasili wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani nchini Tanzania leo wakati wa Uzinduzi wa ripoti ya hali ya Uwekezaji nchini.
Wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa ripoti ya Uwekezaji nchini Tanzania leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Titus Kamani akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu changamoto na hali ya uwekezaji katika sekta ya Mifugo na uvuvi nchini. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika katika masuala ya uwekezaji nchini endapo itatekeleza kikamilifu Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji yaliyowasilishwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD).

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Januari 31, 2014), wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua kitabu cha  Mapitio ya Mfumo wa Uwekezaji kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Pinda  alisema kuwa malengo ya mapitio ya  mfumo huo ni kuboresha hali ya uwekezaji na biashara nchini ambayo matokeo yake yatasaidia kuongeza wawekezaji katika maeneo mengi.

“Kuna maeneo ya uwekezaji yanayopata uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (Foreign Direct Investment -FDI) ambayo ni umeme, mafuta, gesi, madini, viwanda, ujenzi na huduma za jamii.”

Amesema kuwa matokeo ya jitihada hizi ni makubwa na yameonekana ndani ya miaka miwili tu. Akitoa mfano, alisema: “Kilimo kimeweza kukua kutoka dola za marekani  milioni 304.5 mwaka 2010 hadi dola za marekani milioni 355.4 katika mwaka 2011. Vilevile kwenye sekta ya Umeme na Gesi imekua kutoka dola za kimarekani  milioni 328.6 hadi dola za kimarekani  539.8 mwaka 2011.”

Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi zikiwemo rasilimali, nafasi yake kijiografia na historia ya siasa safi ambazo zinaifanya iwe kivutio kikubwa cha uwekezaji. Hali hiyo Waziri Mkuu alisema, imesaidia Pato la Taifa kuendelea kukua kwa asilimia sita kwa miaka 10 mfululizo na mwaka jana ilikua kwa asilimia saba na sasa inatarajiwa kufika asilimia 7.2 kwa mwaka huu.

Miongoni mwa maeneo yanayohusishwa na mfumo huu wa mapitio ya Uwekezaji ni yale yaliyoainishwa katika Matokeo makubwa sasa ambayo ni Kilimo, Maji, Uchukuzi, Elimu na Nishati.

“Ili kufanikisha maeneo hayo ni muhimu tukajenga mazingira bora ya uwekezaji, hivyo Serikali inawataka wadau wote kwa kushirikiana na Sekta binafsi kuchambua kwa makini mapendekezo ya mapitio ya mfumo huo ambayo yanatumika pia kuharakisha mafanikio ya Matokeo makubwa sasa”, alisisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania inashukuru sana Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) kwa kuweka sura maalum kwenye kitabu hicho  inayozungumzia changamoto za uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Ninatumaini kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya utaongeza ufanisi wa mchakato huu na kuhakikisha kuwa tunazitumia fursa zilizopo na nyingine zaidi katika kuboresha uwekezaji katika kilimo nchini. Na kwenye kilimo ninamaanisha kilimo mazao, mifugo, uvuvi na nyuki,” aliongeza.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya OECD, Bw.  Rintaro Tamaki, alisema mazingira ya uwekezaji nchini yanabadilika kila mara kutokana na kuvumbuliwa kwa rasilimali mpya kama vile gesi, makaa ya mawe ambazo zinasababisha watu wavutive kuwekeza nchini.

”Kutokana na kugunduliwa na sekta hizo, Serikali isizipuuzie sekta za zamani hususan Sekta ya kilimo, cha msingi ni kuboresha sekta hii kwa kuanzisha viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yenu”.

No comments: