Meneja wa Vodacom kanda ya Kusini, Henry Tzamburakis akikabidhi msaada wa chakula kwa kituo cha wa watoto yatima cha EAGT Rahaleo Manispaa ya Mtwara Mikindani. Wanaopokea msaada huo kutoka (kushoto) ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu Yasunta Rawland, Boniface Seleman, Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto cha EAGT Mtwara, Caroline Mkwele, Askofu wa kanisa la EAGT Rahaleo Mtwara pia (mwasisi wa kituo) George Mrope. Vodacom kanda ya kusini inatarajia kutumia Tsh.Milioni 3 kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali katika jamii ya kanda ya kusini.
Mkurugenzi wa kituo cha Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT) la Rahaleo Mtwara, Bi. Caroline Mkwele amesema kituo chake hakina majengo ya kuwalelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu takribani hamsini na tatu wanaolelewa na kituo hicho, hatua inayowalazimu watoto kuishi na walezi wao majumbani nakupelekea ugumu katika kuwalea katika maadili.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo wakati wafanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania walipo watembelea kituoni hapo na kukabidhi msaada wa chakula, fedha na vitu mbalimbali ambavyo vinatoka katika michango ya wafanyakazi kupitia mpango wa Pamoja na Vodacom unaolenga kutatua changamoto za ugumu wa maisha zinazoikabili jamii.
“Changamoto tulizo nazo ni nyingi lakini zaidi ni hili la kukosa kituo rasmi kwa maana ya majengo ya kuwahifadhi watoto hawa kwa pamoja, kwa sababu usipowaweka hawa watoto pamoja uwezekano wa kuwa na tabia tofauti ni mkubwa. Hivyo kutokana na ukosefu wa kituo inatulazimu kukutana na watoto hawa kila siku ya Jumamosi. Nawashukuru Vodacom kupitia Taasisi yao ya Vodacom Foundation kwa msaada huu, pia natoa wito kwa wafadhili wengine watusaidie watoto hawa, wasilifumbie macho tatizo hili.” Alisema Bi. Mkwele
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Meneja wa Vodacom Tanzania kanda ya kusini Henry Tzamburakis amesema watoto yatima wanahitaji kupata elimu na mahitaji muhimu kama walivyo watu wengine hivyo kampuni yake itaendelea kutoa msaada ili kuwapunguzia watoto hao ugumu wa maisha.
“Watoto hawa naweza kusema kwamba ni watoto wetu, wadogo zetu na ndugu zetu hivyo yatupasa kuwajali kwa kusikiliza mahitaji yao. Mimi binafsi ningependa kutoa wito tusingojee mpaka kampuni ijikusanye ndio tuje kutoa msaada, mtu yeyote anaweza kufanya hivi kwani haihitaji mpaka uwe tajiri sana, ukiwa na chakula, nguo, chochote kile ambacho unaona kitawafaa watoto hawa usisite kuwaletea.” Alisema Tzamburakis.
Kwa upande wao watoto wanaolelewa na kituo hicho walibainisha kwamba si kupenda kwao kuwa yatima hali hiyo inaweza kumkuta yeyote yule ndani ya jamii, wanawasihi watu wenye uwezo wa aina yeyote kuwasaidia.
“Tunashukuru kwa msaada huu, kwa kweli utatusaidia siku zote za maisha yetu, nawaomba msife moyo kutusaidia kwani bado tunahitaji sana na pia tunathamini kwa kile mnachokifanya.” Alisema Boniface Seleman mmoja wa watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha EAGT Rahaleo Mtwara.
Naye mtoto wa kituoni hapo, Sofia Said alisisitiza kuwa “tunashukuru kwa msaada huu, nawasihi na wengine kuiga mfano waliouonesha kampuni ya Vodacom, zaidi ya hayo ningependa kusema asanteni sana.”
“Napenda kuwaambia wanajamii wenzetu kama unamuona mtoto yatima na wewe una uwezo hata kidogo, sio lazima iwe pesa hata chakula unamsaidia tu.” Alimalizia Yasunta Rawland ambaye pia ni mtoto yatima wa kituoni hapo.
Kwa zaidi ya miaka kumi kampuni ya simu za mkononi Vodacom imekuwa mstari wa mbele kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ambapo katika kipindi hiki watoto zaidi ya 53 wanaolelewa na kituo EAGT Mtwara wamenufaika na msaada huo.
Ongezeko la watoto yatima limekuwa ni janga la kitaifa kwa muda mrefu nchini Tanzania huku serikali, taasisi, mashirika, makampuni binafsi na jamii kwa ujumla zikifanya jitihada mbalimbali za kupambana na kuondokana na changamoto hiyo inayotukabili.
Taasisi ya Vodacom Foundation imekuwa mstari wa mbele kushirkiana na serikali, mashirika, taasisi na wadau mbali mbali wa sekta za maendeleo nchini katika kuisaidia jamii ambayo kwa kiasi kikubwa ni wateja wake. Taasisi hiyo imejidhatiti kufanya kazi na kutoa ushirikiano wa aina yeyote kuhakikisha gurudumu la maendeleo la watanzania linasonga mbele kwa kasi inayotakiwa.
No comments:
Post a Comment