Ujumbe kutoka Tanzania ulioshiriki kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Shirika la Biashara la Dunia (WTO) uliofanyika mjini Bali, Indonesia kuanzia tarehe 3 – 6 Desemba, 2013 ukiongozwa na Mhe. Dkt Abdallah O. Kigoda (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Dkt. Abdallah O. Kigoda (Mb.), Waziri wa Viwanda na Biashara akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Biashara wa Misri Mhe Mounir ABDEL NOUR na ujumbe wake walipokutana katika Mkutano wa Shirika la Biashara la Dunia (WTO) uliofanyika mjini Bali, Indonesia hivi karibuni.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Abdallah O. Kigoda (Mb) akijadiliana jambo na Ndg. Lucas Saronga, Mkurugenzi wa Idara ya Utangamano wa Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Shirika la Biashara la Dunia uliofanyika mjini Bali, Indonesia kuanzia tarehe 3 – 6 Desemba, 2013
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Abdallah O. Kigoda (Mb) akijadiliana jambo na Waziri wa Biashara na Uwekezaji wa Finland Mhe Alexander STUBB kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Shirika la Biashara la Dunia uliofanyika mjini Bali, Indonesia kuanzia tarehe 3 – 6 Desemba, 2013. Mwingine ni Ndg. Lucas Saronga, Mkurugenzi wa Idara ya Utangamano wa Biashara Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania.
Mkutanowa 9 wa Mawaziri wa Nchi wanachama wa Shirika la Biashara la Dunia, ulifanyika mjini Bali, Jimbo la Nusa Dua, nchini Indonesia kuanzia tarehe 3 hadi 6 Desemba 2013. Mkutano huo ulifunguliwa na Mhe.Bw.Susilo Bambang Yudhyono, Rais wa Jamhuri ya Indonesia. Mkutano wa 9 wamawaziri uliendeshwa na Mhe. Gita Wirwajan, Waziri wa Biashara wa Indonesia baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa mkutano. Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mhe. Dkt. Abdallah O. Kigoda, (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara.
Agenda kubwa ya mkutano wa 9 wa Mawaziri ulihusu masuala machache ya Kilimo yaliyokuwa yanajadiliwa katika duru la Doha, kama vile suala la usalama wa chakula pamoja na ruzuku inayotolewa na nchi zilizoendelea kwenye mauzo ya bidhaa za kilimo nje (export subsidies).
Masuala mengine ni pamoja na Uwezeshaji Biashara (Trade Facilitation) na masuala ya fursa za masoko kwa nchi changa kuingiza bidhaa zetu katika masoko ya nchi zilizoendelea kwa masharti ya kutotozwa ushuru na bila ukomo (Duty Free, Quota Free market access- DFQF) pamoja na kusamehewa katika biashara ya huduma, kubanwa na kanuni ya kupata upendeleo (Services Waiver).
Serikali ya Sweden iliahidi kutoa msaada wa ziada wa dola za Marekani milioni 3 kutumbukiza katika mfuko wa Enhanced Integrated Framework (EIF) kwa mwaka 2014. Hili ni ongezeko la dola za Kimareni milioni 14 ambazo Sweden walishatoa kuchangia mfuko huo.
Lengo nikuziwezesha nchi changa (LDC) kushughulikia changamoto za Uwezeshaji Biashara. Mfuko huo wa EIF husaidia nchi changa kutangamana na mfumo wa biashara ya kimataifa na kutatua changamoto za uzalishaji bidhaa kwa mauzo nje (supply side constraints). Vilevile, Denmark, Finland na Umoja wa Ulaya pia waliahidi kutoa fedha zaidi kutunisha mfuko huo.
Katika mkutano huo wa Mawaziri, Sweden pia ilitamka kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.6 za kuanzisha kituo cha mafunzo ESAMI- Arusha, Tanzania ambacho kitatumika kujenga uwezo kwa nchi za Afrika kuweza kutekeleza makubaliano mapya ya Mkataba mpya wa Uwezeshaji Biashara uliyopitishwa mjini Bali. Tanzania ilikuwa inaongoza kundi la nchi changa wanachama wa WTO kwenye majadiliano hayo ya Uwezeshaji Biashara.
China pia imechangia dola za Marekani laki nne zitakazosaidia kundi la Nchi changa katika mchakato wa kuwa mwanachama wa WTO. Australia imechangia dola za Australia milioni 2 na Uswiss imetoa Faranga (CHF) 40,000 kwenye mfuko wa Doha Development Agenda Global Trust Fund na hivyo kufikisha CHF 400,000.
Tanzania itanufaika na michango tajwa hapo juu isipokuwa fedha iliyotolewa kwa ajili ya kusaidia nchi change katika mchakato wa kuwa mwanachama wa WTO kwa sababu Tanzania ni mwanachama tayari.
Wakati wa mkutano huo Mhe. Waziri Kigoda alipata fursa ya kukutana na Mawaziri wa Biashara wa Misri, Sweden na Canada kwa lengo la kuchochea ukuaji wa biashara kwa manufaa ya nchi mbili.
No comments:
Post a Comment