Monday, November 25, 2013

WAZIRI MKUU PINDA: Tamasha la Krismas ni wazo lisilotia ukakasi

WAKATI maandalizi ya Tamasha la Krismas yakipamba moto, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mizengo Kayanza Peter Pinda amesema wazo la kuanzishwa kwa Tamasha la Krismas ni zuri lenye lengo la kuwakutanisha Watanzania mahali pamoja kuabudu na kuliombea Taifa lao dhidi ya mabalaa yanayoitesa dunia likiwemo suala la ugaidi, utekwaji wa viongozi na kuteswa kwa Watanzania.

Waziri Mkuu Pinda ambaye ni maarufu kama mtoto wa Mkulima anasema kwamba Tamasha hilo ni zuri na litakata kiu ya mashabiki wa Muziki wa Injili nchini tanzania kwa sababu linawakutanisha kwenye uwanja mmoja waumini wa madhehebu mbalimbali.

Waziri Mkuu anasema tamasha hilo ambalo wazo la Muandaaji maarufu wa Matamasha ya Injili nchini, Alex Msama linapewa baraka zote kwa niaba ya serikali kwa kuwa lengo lake kuu ni kuwafanya Watanzania kuwa na hofu ya Mungu katika maisha yao yote wanayoishi hapa duniani.

“Mimi kama mwakilishi wa Serikali, kwa niaba ya serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa Baraka zote kwa Tamasha hili na ninaomba lifanyike kwa amani na utulivu ili lengo  la kuanzishwa kwake litimie,” anasema Pinda. Mbali ya Waziri Mkuu , Pinda baadhi ya  Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameiunga mkono kauli ya Waziri Mkuu inayowataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika Tamasha hilo la Krismas.

Lengo la kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo maaskofu, wanasiasa na watu maarufu ambao wanaweza kulizungumzia ipasavyo Tamasha hilo ambalo lina nia ya dhati ya kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya muziki  kwa Jamii yote ya Watanzania. Mbunge wa Viti Maalum (CCM)  Mkoa wa  Mbeya Mary Mwanjelwa amesema Tamasha la Krismas ni ubunifu ambao umekwenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba ni jambo la ubunifu kwa sababu Msama ameona kwamba kiu ya waumini haijakatwa hadi alipoamua kuandaa muendelezo wa Tamasha pendwa la Pasaka.

Mwanjelwa anasema lengo la Tamasha hilo ni mkusanyiko wa watu wa aina mbalimbali ambao wanakusanyika kwa ajili ya kusahau yale yote mabaya ambayo yana dhamira ya kupoteza taswira ya Tanzania ambayo ni kitovu cha amani.

Dhamira hiyo inatokana na sababu kwamba Tamasha hilo ni la Kijamii zaidi na pia ni takatifu kwani linashirikisha waimbaji na wadau mbalimbali wa Kimataifa ambao wanakutana kwa lengo la kuondosha tofauti zenye kuashiria uvunjifu wa amani.

Mwanjelwa anasema ujio wa waimbaji mbalimbali kutoka nje ya Tanzania kunachangia kukusanya wananchi kutoka nchi mbalimbali ambao hujitokeza kwa ajili ya kupata neno la Mungu na kuburudika, mikusanyiko hii pia huondoa ubaguzi wa nchi kwa nchi. Mbunge huyo anasema kutokana na mipangilio ya kuigwa inayofanywa na Msama, Serikali inatakiwa kuchangia nguvu zake katika kufanikisha mikakati inayofanywa na Msama kwani mikusanyiko ya Amani kama hii ni muhimu sana kwa utengamano wa Taifa na bara letu la Afrika.

“Serikali inatakiwa kumuongezea nguvu Msama kwa anayoyafanya, anawaunganisha watu wa mataifa mengi kwa lengo la kumtukuza  Mungu na kutoa michango yao kuwasaidia wanaoishi katika mazingira hatarishi,” alisema Mwanjelwa.  Mbunge wa Igalula (CCM), Athumani Mfutakamba anasema Tamasha hilo linaleta mshikamano, upendo pia linaunganisha waumini wa  imani tofauti  katika mikusanyiko ya kumwabudu Mungu.      

“Kwa sababu waumini mbalimbali watapata elimu na burudani,ambayo itazidisha  upendo amani na  mshikamano miongoni mwao kama viumbe wa mwenyezi Mungu, aliwataka waumini wa dini zote wajiandae kwa ajili ya Tamasha hilo ambalo ni la aina yake. Mfutakamba alisema kwamba upendo huo na amani vitakavyotangazwa  kwenye mikoa yote litakapofanyika Tamasha hilo, waumini wajiandae vilivyo na Tamasha hilo ikiwa ni pamoja na kupata maonyo ya Mwenyezi Mungu kupitia Injili.

Mfutakamba anasema hatua ya kuandaliwa kwa Tamasha hilo kunatokana na sababu kwamba dhamira ya dhati ya waasisi wa nchi hii waliweka sheria na haki ya kuabudu, kukusanyika  na kwenda kokote utakako pasi na kuvunja sheria.   
  
 Naye Mbunge wa Newala, Kapteni, Geroge Mkuchika amesema ni jambo la kheri kwa waandaaji wa Tamasha hilo kulifanikisha kwa sababu linakusanya waumini mbalimbali. Mkuchika anasema Tamasha hilo ni muhimu kwa Watanzania kwa sababu linazungumzia zaidi masuala ya amani, hivyo waumini wa dini mbalimbali linawahusu,alisema wadau wote wa muziki wa Injili wajitokeze kwa wingi siku hiyo uwanja wa Taifa kwa upande wa Dar es salaam na mikoa yote ambako matamasha yatafanyika.

Mkurugenzi wa Msama Promotions ambaye ni muandaaji wa Tamasha hilo, Alex Msama anapongeza jitihada za Wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanatambua mchango wake katika kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia muziki wa injili  na mapambio.

Msama anasema Tamasha hilo linalotarajia kufanyika kwenye mikoa mitano, Desemba 25 litafanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam siku inayofuata litahamia Morogoro, Dodoma, Tanga na Arusha.

“Wadau wa Dar es Salaam na mikoani wakae mkao wa kula kwa sababu nimejiandaa vilivyo kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa kishindo, natarajia kushirikisha waimbaji wa nchi mbalimbali ambao wataimba ‘live’,” alisema Msama na kuongeza. “Tamasha la Krismas litazungumzia Amani zaidi baada ya matukio kadhaa ambayo yanatishia maisha, hali ambayo haimfurahishi Mwenyezi Mungu,” alisema Msama.

Msama anasema Tamasha la Krismas litashirikisha waimbaji mbalimbali wa Tanzania na kutoka nje ya Tanzania, mfumo wa waimbaji utakuwa ni wa kuimba live tofauti na ilivyokuwa katika matamasha yaliyopita. Aidha Msama anawataja waimbaji waliothibitisha kushiriki katika Tamasha hilo ni pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro (Tanzania), Ephreim Sekereti (Zambia) na Solomon Mukubwa (Kenya).

Msama anamalizia kwa kueleza kwamba, fedha zitakazopatikana kwenye Tamasha hilo zitasaidia ujenzi wa kituo cha wenye uhitaji maalum kama Yatima, wajane na wanaoishi katika mazingira hatarishi kinachotarajia kujengwa Pungu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

No comments: