Thursday, November 21, 2013

SOMO LA LEO: Mazingatio 10 juu ya majina ya website

Je umeshawahi kufikiria ni jinsi gani watu wananyohangaika kufika mtaani kwenu kama huo mtaa jina lake halieleweki au kukumbukika kirahisi? Chukulia mtaa wenu unaitwa "Kwa mporomosha matikiti", siyo tu hili jina ni refu, bali linajumuisha maneno ambayo yanachanganya sana "mporomosha" kwani sisi wengine tutaita "mpolomosha".

Majina ya Website ama kwa kingereza wanaita "Domain Names", kama ilivyo anuani za mitaa au nyumba zina maana kubwa sana kwenye ulimwengu wa Website. Uchaguzi wake ni moja ya vitu muhimu sana katika maisha ya website, jina lisiloeleweka, siyo tu litaweza kumpa faida mpinzani wako, bali kuwachanganya wateja na hivyo kupunguza kasi ya ukuaji wako kwenye mtandao.

Kabla hatujaendelea, lazima tujue ni kwa nini kuna majina ya website?
 Inteneti ni netiwoki ya kompyuta ambazo zimeunganishwa na zina uwezo wa kuwasiliana kwa kutumia kanuni za inteneti ( Intenet Protocol au kwa kifupi TCP/IP) .Ili mashine hizi ziwasiliane zinatakiwa zijuane, sawa na sisi tunavyojuana huko mitaani. 

Kwa machine hizi zinatumia namba zinazoitwa IP (mfano: 123.12.123.12) kama utambulishi wa mashine kwenye intaneti. Kwakuwa ni ngumu sana kukumbuka lundo la hizi namba, hapo ndipo majina ya website yalipoibuka.


Majina haya ni herufi zinazosomeka zikiwa ni njia mbadala wa kuwasilisha IP. Kwa mfano, mtu unapoandika Dudumizi.com, website inawasiliana na mahali hii domain ilipofunguliwa ili kuulizia IP yake, hivyo kwa mashine, zao zinatumia IP ila sisi binadamu tunatumia majina wya website. Kwa maneno mengi, majina haya ni kwa ajili ya kurahisisha matumizi kwa binadamu na siyo kwa ajili ya mashine.
Baada ya kuona historia fupi ya majina haya, hebu tuangalie ni vitu gani unatakiwa kuzingatia wakati unachagua majina ya website.

1.Liwe na Mvuto.

Mvuto wa jina ni kitu cha kwanza kabisa, si tunakumbuka kuna mwimbo wa Professor J aliimba, "Bitozi nyangema, anataka kuitwa 2Pac", kwanini alikataa kuitwa Nyangema na kutaka kuitwa 2Pac? ni kwa sababu jina la 2Pac linabeba taswira ya ujana, umjini, umarekani nk. Hii vilevile ipo kwenye majina ya website, jaribu jina litakalokueleza moja kwa moja. Kwa mfano, wewe unafanya biashara ya nguo, ukiwa na webiste yenye jina la nguobomba.co.tz au nguonzuri.com ni dhahiri kuwa mtu akifika tu anajua hii ni website ya nguo tena zilizo bomba.

Hakuna kujiuliza mara mbili utakuwa umeua ndege wawili kwa pamoja, umetangaza biashara ya nguo na umejipa taswira ya nguo bomba na hicho nicho kitu cha muhimu kwenye biashara za mtandaoni. Ingawa majina mengi mazuri tayari yameshachukuliwa, lakini unaweza kufanya utafiti zaidi.

2. Lisilochanganya herufi, uwingi na pia linatamkika kiurahisi.

Chukulia mfano, Dudumizi.com jina hili haijalishi utampa mmarekani au Mchina, wote wataweza kulitamka bila kujiuma ingawa kwa lafudhi tofauti. Kutamkika kwa jina inaamnisha watu wanaweza kuambiana hata kwa simu. Jina lililo rahisi kutamkika litakusaidia kusambaa zaidi na kuwafikia wengi nje ya mipaka yako.
Epuka kutumia uwingi, kwa mfano kwakuwa ciscotechnology.com limeshachukulia, ukaja na jina kama ciscotechnologies.com ni dhahiri kwa wengi wataishia kwenye umoja na hii ndiyo hulka ya binadamu. Kama jina unalolitaka limeshachukuliwa, usijaribu kulazimisha kwa kuongeza maneno au uwingi. Umiza kichwa njoo na jina la kipekee na lenye mvuto.

3. Liwe fupi na lisilo na mkanganyiko wa maneno.

Je ushawahi kuona majina kama businessssimplewaytanzania.com, na walengwa wake ni Watanzania? Jina kama hili siyo tu ni refu mno, bali pia lina mkanganyiko wa maneno mengi mno. Jina kama hili halikumbukiki kiurahisi, na pia ni ngumu kukaririka. Leo hii kwangu ni rahisi kukariri majina kama cisco.com,huawei.comfacebook.comdudumizi.com .

4.Liilinde brandi yako

Hii imeshawahi kutokea mara nyingi sana, jina la website liwe linaloweza kusimama na kuelezea brandi yako. Siyo lazima jina la website liwe sawa na jina la kampuni, kwa mfano, Huawei Technologies kama wangetumia huaweitechnologies.com basi ingekuwa ni ngumu sana ao kukumbukika, ila sasa watu wengi wanakumbua Huawei, IBM, Dudumizi, Cisco na hata Microsoft vilevile.
Jijenge online kwa njia ya kipekee ambayo inakumbukika. Mtu akisikia Dudumizi anajua ni kina nani, bila kuuliza mara mbili na hii ndyo lengo la matumizi ya tehama. Angalia watu kama Google, Yahoo! na Facebook. Wamefanikiwa na majina ya website zao zinawakilisha brand yao moja kwa moja.

5. Walenge wateja

Je umewahi kuona website ambayo walengwa wake wakuu ni Watanzania halafu yao ina mlundikano wa majina ya kingereza tena yale yenye mkanganyiko? Jaribu kutumia majina ambayo ama ni ya kipekee ama yenye maana fulani kwa watu wa eneo husika. Mfano, mtanzania anaposikia jina kama Dudumizi.com moja kwa moja atakuwa na shauku ya kujua kwanini Dudumizi? hivyo ataenda moja kwa moja kwenye website na kutaka kujifunza zaidi.
Ila ukiwa na jina kama tricksforcheapstuffs.com halafu mlengwa ni Mtanzania, siyo tu anaweza hata kukosea kwenye kuandika jina hilo, bali pia kuna uwezekano mkubwa sana akaona hii tovuti si ya Tanzania na akaipotezea. Jina la tovuti linaweza kujenga uzalendo kwa wateja au watembeleaji 
wako na kuona wao ni sehemu ya biashara yako.

MUHIMU: Tuache kasumba kuwa majina ya kingereza ndiyo bora, hii SI kweli na ninaweza kulitetea hili kwa mifano mingi tu. Njoo na majina ya kipekee na epuka kukopi na kupesti na utumwa wa lugha.

6 Tumia viendelezo husika lakini .com ndiye baba lao.

Ingawa .com, .co.tz na .net ni moja ya majina ambayo yanatumika sanasana, ila kuna viendelezo vingine vingi ambavyo unaweza kutumia. Kitu cha msingi ni kuwa, hakikisha unajua website yako inaangukia kwenye kundi gani, website ya shule inapendeza wakatumia .ac.tz badala ya .co.tz. Kwakuwa .com ni kiendelezo kinachotumika kwa wingi, hivyo hakikisha website yako inamiliki .com. Ifuatayo ni orodha ya viendelezo (TLDs) zaidi vya majina ya website;
.co : kifupi kwa ajili ya kampuni, duka la online na jumuiya
.info : kwa ajili ya website za taarifa
.net : tekinolojia, intaneti na mitambo
.org : kwa ajili ya website zisizo za kibiashara
.biz : kwa ajili ya website za biashara
.me : kwa ajili ya website za blog au biafsi

7.Epuka kutumia alama

Kwa mfano jina Dudumizi.com limeshachukuliwa, kuna watu wanaamua kutumia Dudu-mizi.com, ni dhahiri kuwa watembeleaji wengi wataangukiwa kwenye Dudumizi.com hivyo kukufanya upoteze watembeleaji wengi.


8.Ilinde brand yako

Ingawa tumeongelea juu ya kuhakikisha kuwa jina lako lina sifa zote, lakini pia ni jambo la muhimu kuhakikisha unailinda brand yako kwa kununua majina ya viendelezo vyote MUHIMU au vile vinavyoweza kukosewa. Kwa mfano, leo hii kuna makampuni mengi ya Tanzania wanatumia .com na kiendelezo cha .co.tz hakina mtu. Washindani wako wanaweza kununua jina hilo na kuanza kuharibu biashara yako.
Chukulia mfano, ukwata.org ni shirika la dini, halafu hawajanunua ukwata.com au ukwata.co.tz na akatokea mtu akanunua majina hayo na kutumia kwenye website za ngono. Ni dhahiri kuwa kuna baadhi ya watembeleaji wataangukia huko. Hii pia ni kwa kmakampuni, washindani wako wanaweza kutumia mianya kama hii kukumaliza 
kibiashara.

9. Acha ugoigoi

Watanzania wengi tuna kaugonjwa cha ugoigoi, hatuwezi kufanya mambo kwa haraka. Hivyo ukileta ugoigoi kwenye domain itakula kwako. Kwa mfano, binafsi nilinunua jina la Dudumizi.com mwaka 2010 kabla hata ya kuwa na wazo la kufungua kampuni.
Nilifanya hivyo ili kulilinda kwakuwa majina yananunuliwa haraka mno. Na siku hizi watu wa nje ndio wanapenda sana majina yetu, mfano, Joomla, mambo, matamko,kunena nk haya ni baadhi ya majina ya kiswahili ambayo yamenunuliwa na 
watu wasio waswahili.

10.Hakikisha unanunua toka kwa kampuni inayoeleweka

Tukiwa ni kampuni inayojihusisha na huduma za Tehama, wateja kupotea majina yao ni moja ya matatizo tunayokumbana nayo toka kwa wateja wanaokuja kwetu (hata sasa tuna wateja wawili ambao website zao hazipo hewani kwa sababu walinunua majina toka kwa kampuni ya uchochoroni).
Hakikisha kampuni unayonunua jina inaeleweka na ina picha nzuri kwa jamii inayoihudumia. Kwa kufanya makosa kwenye jina kunaweza kukugharimu kiasi kikubwa na hata kusababisha website isiwe hewani kwa miezi. Siyo kila muuza jina ni wa kumuamini. Akiwa ndiye mtu anayehifadhi jina lako, hakikisha unawafahamu vyema na unajua utendaji wao.
Hayo ni mambo kadhaa na muhimu pindi unapochagua wajina ya website, jina likiwa ndiyo ufahamisho ni dhahiri kuwa utaipa kipa mbele na umuhimu wa hali ya juu kabisa kwa maendeleo ya biashara yako.
Kwa makala zaidi za IT  Web: Dudumizi.com  Facebook: https://www.facebook.com/dudumizi

No comments: