Na Mwandishi
Maalum
Wajumbe wa Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa (UM) wamekutana mwishoni
mwa wiki katika mkutano ambao pamoja na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa
Baraza Kuu la Usalama kwa mwaka
uliopita, ulizungumzia pia kuhusu mageuzi
ya kimfumo na uboreshaji wa utendaji wa
majukumu ya Baraza .
Kwa miaka 20 sasa, nchi wanachama wa UM wamekuwa
wakiendelea na majadiliano miongoni kwao, kwa lengo la kufikia muafaka na kukubaliana ni muundo
gani utakaokidhi matakwa ya nchi zote
ili kuongeza nafasi za ujumbe wa kudumu, na nafasi zisizo kudumu katika chombo hicho muhimu.
Pamoja na ukweli kwamba, kimsingi karibu nchi zote zinakubaliana na hoja na dhana nzima ya kulifumua Baraza
hilo, mgawanyiko wa kimakundi, kimaslani, ubinafsi,ubabe na hali ya kutotaka
kulegeza misimamo, kunachangia kusuasua na kukatisha tamaa kama kweli itafika
wakati ambapo chombo hicho kitakuwa shirikishi na chenye
kutekeleza majukumu yake kwa uwazi zaidi.
Katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki,
hapa Makao Makuu ya UM, karibu wazungumzaji kutoka nchi hamsini waliochangia mawazo yao
katika ajenda hiyo ya uwakilishi katika
Baraza Kuu, walionyesha wazi kwamba maneno yamekuwa mengi kuliko
vitendo.
Miongoni mwa nchi zilizochangia majadiliano hayo ni
Tanzania, ambayo kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa,
Balozi Tuvako Manongi ilisema.
“ Pamoja na
utendaji kazi wa kuridhisha wa Baraza
hili, tunaamini kwamba mfumo mzima wa
mageuzi ya Baraza hili umechelewa mno” akasema Balozi na kuongeza “ Nilazima tulifanyie mabadiliko Baraza hili ili liweze kuendana na
hali halisi ya hivi sasa na vilevile kikidhi matarajio ya nchi wanachama kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Umoja wa
Mataifa”.
Aidha Balozi Manongi akasisitiza kuwa mageuzi ya
Baraza hilo ni muhimu pia kwa
Baraza lenyewe ili liendelee kuthaminiwa.
Akabainisha kuwa Tanzania imekuwa ikipigia chapuo umuhimu wa mageuzi ya Baraza kama iliyoanishwa katika Makubaliano
ya Ezulwini na ambao ndio msimamo wa Afrika wa kutaka ipewe
viti viwili vya kudumu na haki zote zikiwamo za kupiga kura ya veto na viti vitano visivyo vya kudumu.
Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM aliongeza kwamba
ni haki wa Afrika kupata viti hivyo kwasababu
karibu mambo yote yanayojadiliwa katika Baraza hilo yanahusu
Bara hilo.
Akizungumza kuhusu misuguano inayojitokeza ndani ya
Baraza hilo, Balozi Manongi aliungana na
wasemaji wengine kwa kuwahisi wajumbe wa baraza kuzungumza kwa sauti moja hasa pale
wanapotakiwa kutolea maamuzi masuala ambayo yanahitaji msimamo wenye kauli
ya pamoja.
Aidha wajumbe wote wanakubaliana na ukweli kwamba
Afrika imeonewa kwakutokuwa na uwakilishi wa kudumu licha ya ukubwa wake.
Lakini pamoja na kuukubali ukweli huo kumekuwamo na mikakati na kauli za kusikitisha ambazo kwa
namna moja ama nyingine zinalenga katika kuendelea kuibinya Afrika.
Baraza Kuu la Usalama la UM , linaundwa na wajumbe watano wa kudumu maarufu
kama P-5,ambao wamekuwapo tangu kuundwa kwa chombo hicho. Na licha ya kutumia kura yao ya veto, lakini
ndiyo wenye maamuzi makubwa ndani ya Baraza na kwa
kiasi kikubwa kauli zao au misimamo yao ndiyo inayosimama.
Pamoja na
wajumbe hao watano wa kudumu, wapo wajumbe wengine kumi kutoka nchi
mbalimbali na ambao hupigiwa kura za
kuingia humo kwa kuzingatia kanda na hudumu kwa miaka miwili. Wajumbe hawana haki ya kupiga kura ya veto.
Afrika si bara pekee linalotaka haki ya kuingia katika
baraza yapo mabara ambayo hayana wawakilishi wa kudumu. Nayo kupitia makundi ama au kama nchi moja moja, yamekuwa yakidai haki hiyo ya kupata kiti cha kudumu
au uwakilishi usio wa kudumu.
Wakubwa ambao ni P-5
licha ya kuwa nao wanaona umuhimu wa kuiboresha hali hiyo, na wanakubali kwamba Afrika imebinywa, wamekuwa wakisisitiza kwamba kura
ya veto isiguswe, au kupinga nafasi za kudumu kuongozwa.
Katika
majadiliano yote ambayo yamekuwa yakiendelea, baadhi yao wameonyesha wazi wazi
nchi gani wanayoitaka ipatiwe kiti hicho
cha kudumu au wamekuwa wakitumia kigezo cha utajiri wa nchi na utayari wake wa kushiriki au hata kutoa
michago ya kifedha, vifaa au rasilimali watu pale linapotokea jambo la dharura.
Kwa maneno mengine
, nchi hizo kubwa katika kulinda
nafasi zao hizo tano na kura yao ya veto hawataki kupoteza hadhi hiyo na hivyo wamekuwa wakitoa kila sababu
kujaribu kukwamisha majadiliano ya kurekebisha dhuluma hiyo.
Baadhi ya wajumbe wakichangia majadiliano hayo, walifikia mahali pa kupashana ukweli,
kwamba maslahi binafsi, ubabe na kila
kundi kutokukubali kulegeza msimamo wake
ndiyo iliyowafikisha hapo.
No comments:
Post a Comment