Saturday, July 23, 2011

HOTUBA YA MWENYEKITI WA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA KILIMANJARO-MECKI, KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA WANAHABARI KUHUSU MAENDELEO YA ZAO LA KAHAWA KWENYE UKUMBI WA UMOJA HOSTEL, MOSHI, JULAI 23, 2011.

MHESHIMIWA MGENI RASMI,
MHESHIMIWA KAIMU MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO,
WAHESHIMIWA WAKUU WA WILAYA,
NDUGU MKURUGENZI MTENDAJI WA UMOJA WA VILABU VYA WAANDISHI WA HABARI
TANZANIA-UTPC.
WAJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI YA MECKI.
WANACHAMA WA MECKI.
WAWAKILISHI KUTOKA CLUB WAANDISHI WA HABARI KUTOKA MKOA WA MANYARA,
ARUSHA NA TANGA, WAANDISHI WA HABARI, WAGENI WAALIKWA,
MABIBI NA MABWANA.

Mwenyekiti wa MECK Bi. Hilda Kileo 

Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana kwenye kongamano hili la wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro na wadau wengine kuzungumzia maendeleo ya zao la kahawa hapa  nchini.
Mh. Mgeni rasmi kwa niaba ya wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na wanachama wa MECKI, tunapenda kukushukuru wewe kwa kukubali mwaliko wetu wa kuja kutufungulia kongamano hili kwa siku ya leo.
Kipekee tunasema huu ni uungwaji mkono wa hali ya juu tulioupata kutoka kwako na pia ni hatua muhimu ya mafanikio ya kongamano hili, litakalosikika  nchi nzima kupitia vyombo vya habari.
Mh. Mgeni rasmi sisi viongozi na wanachama wa klabu ya wanahabari mkoa wa Kilimanjaro, tumeshirikiana na wadau wawezeshaji kutekeleza azma yetu ya kuandaa kongamano hili kwa malengo makubwa yafuatavyo:

1.      Kuanzisha na kuendeleza ushirikiano wa pamoja kati yetu sisi wanahabarai na wadau wote wa kahawa, katika kutekeleza mpango wa kufufua na kuendeleza zao la kahawa hapa nchini.
2.      Kutujengea uwezo sisi wanahabari kufahamu shughuli mbali mbali zinazofanywa na taasisi husika kwenye zao la  kahawa ili baadaye tuweze kuandika habari za kina kuhusu sekta ya kahawa hapa nchini.
3.       Kuonyesha dhamira yetu na utayari wetu kushirikiana na taasisi hizi kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha jamii kwa ujumla umuhimu wa kushiriki kwenye programu nzima ya kukuza na kuendeleza zao hili katika maeneo yao.
Mh. Mgeni rasmi , pamoja na sababu hizo tumelenga kuwa kongamano hili liwe na dira ya Kujenga mtazamo chanya kwa Watanzania katika kufikia malengo ya maendeleo ya zao la Kahawa Tanzania.
Vile vile ni fursa pekee kwetu sisi wanahabari kuweza kutathmini hali ya maendeleo ya zao la kahawa Tanzania, na baadaye tuweze Kujadili hali ya maendeleo ya zao hilo na kuutaarifu umma yatakayotokana na mjadala huu.
Mh. Mgeni rasmi, washiriki wa kongamano hili watapata fursa ya kusikiliza mada sita zitakazowasilishwa kwenye kongamano hili, kama jinsi zilivyoandaliwa na watoa mada mbali mbali kutoka katika taasisi za kahawa na wadau wengine.
Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa kwenye kongamano hili ni pamoja na Sera, sheria na mipango inayosimamia maendeleo ya zao la kahawa nchini pamoja na soko lake, kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania-TCB, Nafasi ya tafiti mbalimbali katika upatikanaji wa kahawa bora Tanzania, kutoka Taasisi ya utafiti wa kahawa Tanzania-TaCRI.
Mada nyingine ni Ushirika katika maendeleo ya zao la kahawa Tanzania,itakayowasilshwa na  Makamu Mkuu wa chuo utawala na fedha, Chuo Kikuu cha kishiriki cha ushirika na biashara Moshi-MUCCOBS, Nafasi ya waandishi wa habari katika maendeleo ya zao la kahawa, itakayowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Muungamano wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania, UTPC .
Vile vile mada kuhusu Mchango wa zao la Kahawa katika kuboresha maisha ya mkulima, kutoka chama kikuu cha ushirika mkoani Kilimanjaro-KNCU, itawasilishwa.
Mheshimiwa mgeni rasmi, kama nilivyoeleza hapo awali kuwa tumefanikiwa kuandaa kongamano hili kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika sekta hii ya kahawa hivyo basi naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa kulikubali wazo letu na kutuunga mkono.
Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Bodi ya Kahawa nchini-TCB, Kituo cha Utafiti wa Kahawa Nchini-TaCRI, Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Kilimanjaro-KNCU, ambao kwa pamoja wametuwezesha kuandaa kongamano hili linalofanyika kwa siku ya leo.
Kwa niaba ya kamati ya utendaji na wanachama wa MECKI, ninapenda kusema kuwa mchango wao umekuwa na manufaa makubwa sana kwetu sisi na kwa maendeleo ya zao la kahawa hapa nchini.
Mheshimiwa mgeni rasmi, kabla sijahitimisha napenda kutumia fursa hii ndogo kuelezea historia fupi ya klabu yetu ya waandishi wa habari mkoa wa Kilimanjaro-MECKI.
Klabu yetu ilisajiliwa rasmi April 19 mwaka 1999, ikiwa na jumla ya wanachama 11 waanzilishi lengo likiwa ni kuwaunganisha waandishi wa habari wa mkoa wa Kilimanjaro, na pia kuwa kiungo kati yao na wadau mbalimbali katika tasnia ya habari.
Tangu kuanzishwa kwa MECKI, imefanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha kuwaunganisha waandishi ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama kutoka 11 mwaka 1999 hadi 67 mwaka huu.
Katika kipindi hicho pia baadhi ya waandishi walifanikiwa kuongeza ujuzi katika fani ya habari, kwa kupatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwenye vyuo mbalimbali, yaliyowezeshwa na wadau mbalimbali kupitia MECKI.
CHANGAMOTO:
Mh,Mgeni rasmi, pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia zipo changamoto zinazotukabili ikiwemo ya kukosa ofisi ya kudumu ya MECKI, gharama za uendeshaji wa ofisi  kwa sasa  muungano wa vilabu vya waandishi  wa habari  Tanzania UTPC  wametupunguzia mzigo huu wa uendeshaji wa ofisi  tunashukuru sana kwa msaada wao mkubwa , viwango vyetu vya elimu kutoendana  na changamoto ya kiteknolojia iliyopo sasa duniani.

Hata hivyo tumekuwa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizi na mipango inayolenga,  hatua zinazoanza kufanywa lakini tunategemea sana mchango wa wadau wetu ili tuweze kufikia mafanikio.
Pamoja na mkakati huo,  kwa sasa tunaendelea kutekeleza mkakati unaolenga kuboresha mahusiano baina yetu kama klabu na wadau tunaoshirikiana nao kwenye tasnia ya habari, kuwa na ofisi yetu ya
kudumu ya MECKI, ili kupunguza gharama za uendeshaji wa ofisi, kutafuta vyanzo vya uhakika vya mapato, kwa kubuni miradi mbalimbali na kutafuta wadau /wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi watakaotufadhili waandishi wa habari, kujiendeleza kielimu, ili na sisi tuweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya kidunia.

Mh. Mgeni rasmi, baada ya kusema hayo sasa ni matumaini yangu kuwa wewe pamoja na wadau wengine mtatuunga mkono katika harakati zetu hizi zinazolenga kukijenga chama chetu kwa manufaa yetu sisi na wadau wetu.
Mwisho tunashukuru watoa mada wote kwa kukubali wito wa kuja kutoa mada katika kongamano hili tunaamini tutaongeza uwezo wetu pamoja na kufukia malengo ya kongamano hili .
Sasa nachukua nafasi hii kusema kuwa sisi washiriki tuko tayari kukusikiliza utufungulie kongamano letu..

No comments: