Saturday, July 23, 2011

HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA MOSHI ALHAJI MUSSA SAMIZI KWENYE UFUNGUZI WA KONGAMANO LA WANAHABARI KUHUSU MAENDELEO YA ZAO LA KAHAWA NCHINI LILILOANDALIWA NA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA KILIMANJARO (MECKI), JULAI 23,2011.

Mkuu wa wilaya ya Moshi Mhe. Mussa Samizi
Mwenyekiti wa Mecki,
Katibu mkuu mtendaji wa Mecki,
Watoa mada kutoka taasisi ya utafiti wa Kahawa(TaCRI),
Bodi ya Kahawa Tanzania(TCB),
Chama kikuu cha ushirika Kilimanjaro(KNCU),
Naibu mkuu wa chuo kikuu kishiriki cha ushirika na biashara Moshi(MUCCoBS),
Mkurugenzi wa muungano wa vilabu vya wanahabari Tanzania (UTPC)
Wajumbe wa kamati ya utendaji MECKI.
Wanachama wa MECKI,
Waandishi wa habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na mabwana.


Nianze kwa kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia siku hii tukiwa wenye afya njema. Tukitekeleza majukumu yetu sote lakini kila mmoja kwa nafasi yake.
Kwanza niishukuru Klabu ya waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro kwa kunialika na kuona kwamba nina nafasi kubwa ya kufungua kongamano hili ambalo limeandaliwa kwa pamoja na wadau mbalimbali wa zao la kahawa.
Nilifahamu mgeni aliyepaswa kushiriki nasi leo hii alikuwa ni waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Samwel Sitta,lakini kutokana na majukumu ya kitaifa yaliyomlazimu yeye na viongozi wengine wa serikalini ameshindwa kujumuiknanyi.
Pamoja na udhuru huo anawatakia mafanikio mema kwenye kongamano hili, muhimu kwa maendeleo ya zao hili la kahawa ambalo pia ni muhimu kwa uchumi wa wakulima na mkoa wetu kwa ujuimla.
Vile vile napenda kutoa pongezi kwa uongozi mzima na wanachama wa MECKI, kwa kuwa na tukio kubwa kama hili, ni matumaini yangu kwamba mafanikio ya kongamano hili ni mafanikio yetu sisi sote.
Nimeelezwa kwamba dira ya kongamano hili ni kujenga mtazamo chanya kwa watanzania katika kufikia malengo ya maendeleo ya zao la Kahawa Tanzania.
Pamoja na dira ya kongamano hili pia nimejulishwa kwamba dhamira kubwa ni kutathmini hali ya maendeleo ya zao hili, wakati lengo kubwa kwa wanahabari ni kujadili hali ya Kahawa na kuuarifu umma yale yote yatakayotokana na kongamano hili.
Awali ya yote napenda kuihakikishia klabu ya wanahabari na wadau wengine kwa ujumla kwamba serikali inathamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari nchini katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Sisi serikali tunatambua kazi kubwa inayofanywa na waandishi wa habari nchini katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na za kina kuhusu yale yanayojitokeza kwa maendeleo ya jamii yetu.
Kongamano hili limekuja wakati mwafaka kutokana na harakati mbali mbali zinazofanywa wadau wa kahawa kuhimiza kilimo cha zao la kahawa baada ya bei kuanza kuimarika kwenye masoko ya nje na ndani ya nchi.
Ni matumaini yangu kwamba wadau na waandishi wa habari mtakuwa na muda wa kutosha kuelezana mikakati mbali mbali inayolenga kufufua zao la kahawa akini namna wakulima watakavyohamasishwa kurejea katika kilimo cha kahawa kama fursa muhimu ya uchumi kwao.
Jitihada zilizofanywa na Mecki katika kuibua mijadala wa zao la Kahawa zinaungwa mkono na serikali kwani hakuna asiyefahamu faida ya zao la Kahawa katika kuchangia maendeleo ya uchumi, na nimepewa taarifa kwamba asilimia kubwa ya wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na baadhi ya mikoa inayolima zao la Kahawa wamesoma na kupata maendeleo ya aina tofauti kutokana na kilimo cha Kahawa.
Ndugu mwenyekiti wa Mecki,
Zao la kahawa ambalo limelimwa nchini kwa miaka mingi sasa limekuwa likikumbwa na changamoto nyingi ambazo baadhi ya changamoto hizo zimekuwa sababu mojawapo iliyolenga kuwa na mjumuiko huu katika kuzijadili hatimaye kupata mawazo ya namna ya kukabiliana nazo.
Napenda kusema kwamba nimefurahishwa na ushiriki wa watoa mada katika kongamano hili, kwani jitihada zao zimeonekana na zinaendelea kuonekana katika kutekeleza mpango wa serikali wa kukuza sekta kilimo na zao la kahawa kwa ujumla.
Ni kweli wakulima wetu walikata tamaa na kilimo hiki lakini sasa hali ni tofauti kwani, wadau hawa kwa pamoja wamewahamasisha wakulima kulima hao kuzingatia ushauri wa kitaalam katika kulima zao hilo na kuachana na kilimo cha mazoea.
Napenda kutoa wito kwa wadau hususani watafiti wa zao hili kuhakikisha matokeo ya tafiti zao zinawafikia wakulima vijijini ili ziwasaidia kuwa na mabadiliko kwenye kilimo cha kahawa, ikiwemo kubuni aina mpya zaidi ya miche ya kahawa inayozalishwa kwa wingi na kwa ubora unaohitajika kwenye soko. Ndugu mwenyekiti wa Mecki,
Miaka ya nyuma baadhi ya wakulima wetu waliamini kwamba wingi wa Kahawa Ndiyo kunawapa bei nzuri katika soko la dunia lakini ukweli halisi ni kwamba bei nzuri ya Kahawa katika masoko mbalimbali inatokana na ubora wake.
Ni dhahiri kwamba wahusika katika maendeleo ya zao la kahwa wanao wajibu mkubwa wa kutoa elimu ya kina yenye lengo la kuwasaidia wakulima kuzifahamu mbinu mbali mbali za kuandaa kahawa iliyo bora, ili iweze kuwa na tija kwao.
Pamoja na matokeo ya utafiti lakini vyombo vya habari navyo vinao wajibu mkubwa katika maendeleo ya zao la kahawa nchini.
Hivyo basi nitoe wito kwa waandishi wa habari kutambua wajibu wao mkubwa katia kusaidia kufikisha elimu inayotolewa na wataalam hawa wa kahawa, hatimaye kumfikia mkulima wa kijijini.
Hivi karibuni nimesikia taasisi ya TaCRI imefanikiwa kubuni aina 14 za miche ya kahawa chotara ya Arabika na Robusta na matokeo ya utafiti huo yameelezwa kuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima ambao wamekuwa wakipata mavuno mengi na kahawa hiyo kukubalika kwenye masoko kutokana na ubora wake.
Pia utafiti huu umeleta unafuu mkubwa kwa wakulima kwani hpo awali walilazimika kutumia gharama kubwa katika kilimo cha kahawa ambapo asilimia 50 ya mapato yao yalielekezwa mashambani na kujikuta hawanufaiki na zao hilo.
Hii ni fursa sawia kwa waandishi wa habari kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha zao la kahawa linaendelea kuboreshwa kama njia moja wapo ya kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja,mkoa na taifa kwa ujumla.
Vyama kama KNCU na bodi ya kahawa Tanzania wana nafasi nzuri ya kushirikiana na waandishi wa habari ili kuwasaidia wakulima ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakipewa taarifa potofu kuhusu zao hilo huku wengine wakishawishiwa kutafuta mazao mbadala ili kupata fedha za haraka haraka, sina maana wakulima wasiwe na mazao mengine ya kusaidiana na zao hili lakini wataalamu katika taasisi zinazohusika watumike katika kuwashauri wakulima wetu njia sahihi za kufuata.
Mwisho kabisa napenda kuwashukuru waandishi wa habari kwa kuandaa kongamano hili na ninawaahidi kwamba serikali  itaendelea kuwaunga mkono katika mambo mazuri anayolenga kulijenga taifa letu, kama jinsi ambavyo tumekuwa tukishirikiana katika kipindi kilichopita.
Baada ya kusema hayo sasa napenda kutamka rasmi kwamba kongamano hili la wanahabari linalojadili maendeleo ya zao la kahawa nchini limefunguliwa rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments: