Saturday, July 23, 2011

HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012

WAZIRI  MHE. BERNARD KAMILLIUS MEMBE
Naibu Waziri, Mhe. Mahadhi Juma Maalim

Katibu Mkuu, Bwana John M. Haule

Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha

A.                    UTANGULIZI

1.       Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

2.  Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Pili, ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Aidha, ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Bilal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile, ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, (Mb.) kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na Mhe. Rais na hatimaye kuthibitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.

3.   Mheshimiwa Spika, napenda nikupongeze kwa kuchaguliwa kwa kishindo kushika nafasi ya Spika wa Bunge letu tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu, miaka 50 iliyopita. Uteuzi wako ni kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya nchi yetu na imani kubwa tuliyonayo sisi Waheshimiwa Wabunge, juu ya utendaji wako uliotukuka. Kadhalika, nampongeza Naibu Spika, Mhe. Job Ndugai pamoja na Wenyeviti kwa kuchaguliwa katika kusaidia uendeshaji wa Bunge hili tukufu. Napenda pia kuwapongeza Mawaziri wenzangu pamoja na Naibu Mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupata heshima na dhamana kubwa ya kuwawakilisha wananchi wa majimbo pamoja na makundi mbalimbali ya jamii katika Bunge hili.
4.   Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee niwashukuru Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Mustafa Haidi Mkulo (Mb.) kwa hotuba zao ambazo zimetoa  mwelekeo wa Taifa letu katika mwaka huu wa fedha. Hotuba zao zimegusia mambo ya kimsingi yanayohusu Wizara yangu. Naomba pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wote walionitangulia katika kuwasilisha hotuba zao kwa kuzungumzia kwa ufasaha baadhi ya masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa wanayoyashughulikia katika Wizara zao. Wizara yangu imekuwa ikishirikiana vyema na kwa karibu sana na Wizara hizi, na mara zote imekuwa ikizingatia ushauri wao kwa umakini mkubwa.

5. Mheshimiwa Spika, napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya Uenyekiti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.) kwa ushauri wao ambao umekuwa wa msaada mkubwa katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu kwa mafanikio.

6.      Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru   Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye ameendelea kuwa wa msaada mkubwa kwangu katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, namshukuru Katibu Mkuu, Bwana John M. Haule; Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha, Wakurugenzi wote, Mabalozi wetu pamoja na wafanyakazi wenzangu wote Wizarani na katika Balozi zetu kwa bidii na kujituma kwao ipasavyo katika kutetea na kulinda maslahi ya nchi yetu ndani na nje na pia  kwa kufanikisha kwa wakati hotuba hii ya bajeti.

7.   Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wapiga kura wangu na wananchi wa Jimbo la Mtama, kwa upendo wao na imani yao kwangu. Napenda pia niwashukuru viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa Mkoa wa Lindi kwa uongozi thabiti na kwa ushirikiano wao mkubwa. Kwa upande wa familia yangu, ningependa kumshukuru sana mke wangu, Dorcas Membe, pamoja na watoto wetu kwa kunitia moyo na nguvu katika shughuli zangu za kila siku.  Mama Membe hayupo pale juu leo kwa sababu yupo nje ya nchi akimuuguza kijana wetu Denis ambaye amefanyiwa upasuaji mkubwa na namtakia afya njema.
B.          HALI YA DUNIA NA CHANGAMOTO ZILIZOPO

8. Mheshimiwa Spika,  hali ya uchumi na usalama duniani kwa ujumla ni shwari isipokuwa katika maeneo machache ambayo yanahitaji uangalizi wa makini wa jumuiya ya kimataifa.

9. Mheshimiwa Spika, hali ya uchumi katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, imeendelea kuimarika baada ya kipindi kigumu cha mdororo wa uchumi uliyoikumba dunia mwaka 2008 licha ya baadhi ya nchi kama Ugiriki, Uhispania na Ureno kuendelea kusuasua katika kuimarisha uchumi wao.  Kwa ujumla, hali ya usalama duniani inatia moyo ingawa kuna maeneo machache ambayo yamegubikwa na migogoro ya ndani, iliyosababishwa na shinikizo la kutaka mabadiliko ya kisiasa, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira.  Hali hiyo imeleta madhara makubwa katika nchi ambazo hazikuingia katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaliyoanza katika miaka ya themanini hadi miaka ya tisini.  Madhara hayo ni pamoja na vifo vya raia, ongezeko la wakimbizi, uharibifu wa miundombinu, kuzorota kwa shughuli za uzalishaji na hivyo kuongezeka kwa umaskini na hatari ya kuibuka kwa vitendo vipya vya kigaidi.  Wizara yangu imeendelea kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika michakato ya kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro hiyo.

Hali ya kisiasa na kiusalama barani Afrika

10.    Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, hali ya kisiasa na kiusalama Barani Afrika katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, ni nzuri isipokuwa katika nchi za Somalia, Sudan, Côte d’Ivoire, Tunisia, Misri na Libya ambako hali ya usalama siyo ya kuridhisha na hali ya kisiasa bado haijakaa sawa.  Hali hiyo imesababishwa na matukio mbalimbali ambayo sasa nitayapitia kwa ufupi.

11.    Mheshimiwa Spika, eneo la ukanda wa Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini limekumbwa na machafuko makubwa yaliyobatizwa jina la Mapinduzi ya Yasmini (Jasmine Revolution) kwa upande wa Tunisia au kwingineko kama Chemichemi ya Uarabuni (Arab Spring). Nchi za Misri, Libya, Oman, Jordan, Syria, Yemen na Bahrain zimekumbwa na vuguvugu hili ambalo limekuwa na madhara na matokeo tofauti.

12.    Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimewahi kueleza huko nyuma, sababu zilizochangia machafuko hayo ni nyingi na hakuna majawabu mepesi na wala hakuna jawabu moja linalokidhi hoja ya matukio yote. Lililo dhahiri ni kuwa baada ya nchi kama Tunisia  na Misri kufanikiwa kuziondoa Serikali zao zilizokuwa madarakani kwa njia ya amani, bado nchi hizo hazijawa na hali  ya utulivu wa kisiasa na kiusalama kwa sababu ya kugombania madaraka.

13.    Mheshimiwa Spika, machafuko hayo yameleta athari mbalimbali kwa bara la Afrika na dunia kwa ujumla. Athari hizo zinatokana na ukweli kuwa nchi za Afrika ya Kaskazini hususan Libya ni wawekezaji barani Afrika na wachangiaji wakubwa katika bajeti ya Umoja wa Afrika. Kuingia kwa nchi hizo katika machafuko kunaweza kuathiri bajeti ya Umoja wa Afrika (UA) na uwekezaji katika baadhi ya nchi za Afrika. Pamoja na hayo, hali ya usalama katika eneo la Kaskazini mwa Afrika itaendelea kuwa ya wasiwasi kutokana na hali ya usalama nchini Libya kutotengamaa hadi sasa. Hali hii inaweza kuleta machafuko katika nchi nyingine za Kaskazini mwa Afrika. Kwa upande wa uchumi, machafuko haya yatachangia katika kuongezeka kwa bei ya mafuta kutokana na kupungua kwa uzalishaji wake na hivyo kuathiri uchumi wa nchi zinazoagiza mafuta kama Tanzania. Tanzania, inaungana na wadau wote kuunga mkono jitihada za kuhakikisha kuwa nchi hizi zinavuka katika mtihani huu kwa njia ya amani.     
14.    Mheshimiwa Spika, tofauti na maandamano ya raia wa Tunisia na Misri yaliyoendeshwa kwa njia ya amani, hali haikuwa hivyo nchini Libya. Maandamano nchini Libya yalichukua sura ya uasi na ghasia kwa waandamanaji kutumia silaha za kivita na hivyo kusababisha mapigano kati yao na majeshi ya serikali. Hali hiyo imesababisha, madhara makubwa nchini Libya ikiwa ni pamoja na raia kupoteza maisha, kuikimbia nchi yao, miundombinu na mali nyingi kuharibiwa vibaya.

15.    Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua zilizochukuliwa na majeshi ya Serikali dhidi ya waasi, jumuiya ya kimataifa ilianza kuingiwa na hofu na hivyo kuamua kuingilia kati mgogoro huo. Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisimamisha uanachama wa Libya na  baadaye, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio Na. 1973 la tarehe 16 Februari, 2011 lililopiga marufuku ndege kuruka katika anga ya Libya (imposition of No fly zone).  Aidha, Azimio hilo liliitaka jumuiya ya kimataifa  kuchukua hatua za kulinda mali na raia wa Libya dhidi ya mashambulizi ya vikosi vya Serikali ya Libya.
16.  Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya  Azimio Na. 1973, ambalo Tanzania na Umoja wetu wa Afrika uliliunga mkono, utekelezaji wake umevuka mipaka ya madhumuni ya Azimio hilo.  Mashambulizi yanayofanywa na majeshi ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) na waasi wa Libya pamoja na majibu ya mapigo yanayotolewa na Majeshi ya Serikali yanaua watu, yanaharibu miundombinu na mali za raia kinyume na Azimio Na. 1973.   Kutokana na hali hiyo, Tanzania, Umoja wa Afrika, Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote na baadhi ya nchi za Kiarabu, zililaani na kupinga utekelezaji wa Azimio hilo la Baraza la Umoja wa Mataifa na kutoa wito wa kusitisha mashambulizi ili kutoa fursa ya mazungumzo kufanyika kwa pande zote zinazohusika na kumaliza mgogoro huo.
Hali ya maradhi barani Afrika
17.  Mheshimiwa Spika, Afrika bado inaendelea kukumbwa na maradhi sugu ya Malaria na Ukimwi.  Ugonjwa wa Malaria unaua watu 700,000 kwa mwaka Barani Afrika na kati ya hao, vifo 595,000 ni vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.  Kila mwaka, Afrika ina wastani wa wagonjwa wa malaria milioni 176 wanaopatiwa matibabu. Aidha, Bara la Afrika linapoteza dola za kimarekani bilioni 12 kwa ajili ya kununua madawa na  vyandarua pamoja na matibabu ya malaria.
18.    Mheshimiwa Spika, kwa kutambua uzito na ukubwa wa tatizo hili, Umoja wa Afrika umeamua kwenda vitani kupambana na ugonjwa huu. Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye sasa ni Mwenyekiti wa viongozi 39 wa Umoja wa Afrika waliopania kutokomeza ugonjwa wa Malaria Barani Afrika, yeye na wenzake wanafanya kazi kubwa ya kuunganisha nguvu za Mashirika mbalimbali Duniani yanayojihusisha na utokomezaji wa malaria, kuelekeza nguvu zao Afrika kwa lengo la kutokomeza na siyo kutibu tu malaria.
19.    Mheshimiwa Spika, sambamba na Malaria, yapo maradhi sugu ya Ukimwi Barani Afrika.  Hadi sasa, ukimwi umeua watu milioni 22.4 Barani Afrika tangu uanze mwaka 1984.  Kati ya hao watoto na akina mama wapatao milioni 11.2 wamepoteza maisha yao.  Tuna wagonjwa milioni 5 Barani Afrika wanaopatiwa matibabu na idadi ya watu wanaoambukizwa ukimwi kwa siku Barani Afrika wanakaribia 5,000.
20. Mheshimiwa Spika, ugonjwa huu hauna dawa.  Dawa ni sisi wenyewe.  Tuendelee kuelimishana na tubadili tabia zetu.
C.          JUHUDI ZA UMOJA WA AFRIKA KATIKA KUTATUA MIGOGORO
Libya
21.    Mheshimiwa Spika, tofauti na maoni ya baadhi ya watu kuwa mgogoro wa Libya ulipoibuka, Umoja wa Afrika ulikaa kimya, siyo ya kweli. Umoja wa Afrika ulichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuunda Kamati Maalum ya Usuluhishi inayojumuisha viongozi wa nchi tano za Mauritania, Afrika Kusini, Uganda, Mali na Congo ili kutathmini hali ya kisiasa nchini Libya na kukutana na pande zinazohusika kwenye mgogoro huo kwa lengo la kutafuta ufumbuzi kwa njia ya amani.
22.    Mheshimiwa Spika, Kamati hiyo ilitengeneza na kuwasilisha Mpango wa Amani wa kusuluhisha mgogoro wa Libya (AU Peace Roadmap) na  ulikuwa na vipengele vitano ambavyo ni:- kuwalinda raia na kusitisha mapigano; utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa raia na wafanyakazi wa kigeni; kuanzisha majadiliano ya kisiasa na pande zinazohusika ili kufikia makubaliano ya kumaliza mgogoro; kuanzisha kipindi cha mpito ambacho kitahusisha pande zote; na kuridhia mageuzi ya kisiasa ambayo yatakidhi matakwa ya Walibya wote.
23.  Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika walifanya mkutano maalum tarehe 25 Mei, 2011 mjini Addis Ababa, Ethiopia, na kusisitiza mshikamano kwa nchi za Afrika katika kutetea na kulinda uhuru na umoja wa Libya. Aidha, viongozi hao walilaani mashambulizi ya NATO na kutaka yasitishwe mara moja ili kuipa nafasi zaidi Afrika kutekeleza mpango wa Amani (Road map) uliowasilishwa kwao na Kamati Maalum ya Umoja wa Afrika.  Afrika inaamini kwa dhati kuwa amani ya kudumu nchini Libya haiwezi kupatikana kwa nguvu za kijeshi. Msimamo huo ulisisitizwa tena na Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano wao wa kumi na saba (17) uliofanyika Malabo, Equatorial Guinea mwishoni mwa Juni 2011. Napenda kuchukua nafasi hii kusisitiza msimamo wa Tanzania kuwa pamoja na nia nzuri ya Azimio Na. 1973 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Tanzania kama ilivyo kwa nchi zote za Umoja wa Afrika hazikubaliani na utekelezaji wake na hatima yake.  Tunazitaka pande zote zinazopigana, yaani NATO, Majeshi ya Waasi na ya Serikali kusitisha mapigano hayo mara moja na kuipa Afrika nafasi ya kumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani.
Côte d’Ivoire

24.    Mheshimiwa Spika, mgogoro wa Côte d’Ivoire ulihitimishwa baada ya Mhe. Alassane Ouatara kuapishwa tarehe 9 Mei, 2011 kuwa Rais mpya wa nchi hiyo kufuatia  ushindi katika uchaguzi uliofanyika tarehe 28 Novemba, 2010 na kupingwa na baadaye kuondolewa kijeshi kwa Rais aliyeng’ang’ania madarakani. Itakumbukwa kuwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa mchango mkubwa kama mmoja wa wajumbe wa Kamati Maalum ya Umoja wa Afrika iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo. Kutokana na mafanikio hayo, Tanzania inaendela kupata heshima kubwa katika masuala ya utatuzi na usuluhishi wa migogoro Barani Afrika.  Aidha, uzoefu wa kilichotokea Côte d’Ivoire unatufundisha kuwa Umoja wa Afrika unaweza kumaliza migogoro yake pale inapoachwa huru na bila kuingiliwa katika kushughulikia migogoro hiyo.

Sudan ya Kusini

25.   Mheshimiwa Spika, ninafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba hatimaye Sudan ya Kusini imekuwa Taifa huru tarehe 9 Julai, 2011 na hivyo kuongeza idadi ya nchi huru za Afrika kufikia hamsini na nne (54). Nachukua fursa hii kuwapongeza tena Rais Salva Kiir Mayardit na wananchi wote wa nchi mpya ya Sudan ya Kusini kwa kuvuna walichopanda; uhuru uliotokana na jasho na damu yao.  Aidha, Tanzania itaikaribisha kwa mikono miwili nchi ya Sudan ya Kusini itakapoamua kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Tanzania itamkumbuka daima mwasisi na mwanamapinduzi marehemu John Garanq kwa kuanzisha mapambano yaliyoleta Uhuru Sudan ya Kusini.

26.  Mheshimiwa Spika, aidha, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa, kwa kuongoza jopo la watu watatu mashuhuri walioteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kusimamia mchakato wa kura ya maoni nchini humo.  Ni matumaini yangu kwamba uhuru uliopatikana utapanua nyanja za ushirikiano kati ya nchi yetu na Sudan ya Kusini. Hivyo, natoa rai kwa Watanzania wenzangu wachangamkie, bila kuchelewa, fursa zilizopo katika taifa hilo jipya. Wizara yangu itatoa ushirikiano utakaohitajika ili kufanikisha azma hiyo.

Somalia

27.  Mheshimiwa Spika, hali ya usalama nchini Somalia katika siku za hivi karibuni inaleta matumaini  baada ya vikosi vya usalama vya Serikali ya Mpito ya Somalia na Umoja wa Afrika (AMISOM) kufanya mashambulizi makali dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab. Kutokana na mashambulizi hayo, maeneo mengi yaliyokuwa ngome ya Al-Shabaab mjini Mogadishu yapo chini ya Serikali ya mpito na hivyo kusaidia kuimarisha hali ya usalama na usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

28.    Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa hivi sasa kuhusiana na mgogoro wa Somalia ni uhaba wa askari wa kulinda amani. Tanzania inazisihi nchi zilizoahidi kuchangia vikosi vya kulinda amani zitekeleze ahadi zao. Aidha, tunatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa Azimio lake la kuongeza vikosi vya AMISOM kutoka 8,000 hadi kufikia 12,000 linatekelezwa haraka iwezekanavyo.

29.    Mheshimiwa Spika, Tanzania inaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro wa Somalia. Mwezi Aprili 2011, Rais wa Somalia Mhe. Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alifanya ziara hapa nchini, na kuonana na mwenyeji wake Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo mchakato wa amani nchini Somalia ulijadiliwa.

30.    Mheshimiwa Spika, kuzorota kwa amani na usalama kwa muda mrefu nchini Somalia, kumezusha baa la njaa nchini humo  na kuwafanya baadhi ya vijana wa kisomali kujihusisha na vitendo vya uharamia kwenye pwani ya Afrika Mashariki. Matukio ya uharamia yanazidi kuongezeka na hivyo kuathiri uchumi wa nchi yetu. Athari hizo ni pamoja na; kupanda kwa bei za bidhaa kutokana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji. Gharama hizo zinatokana na mahitaji ya ulinzi kwa ajili ya kusindikiza meli za bidhaa na kufanya doria katika eneo hilo, na kuongezeka kwa gharama za bima na meli kulazimika kuzunguka umbali mrefu  ili kukwepa maharamia.

31.    Mheshimiwa Spika, Tanzania haiwezi kukwepa athari za uharamia kutokana na mahali ilipo kijiografia. Hivyo, Wizara yangu inashirikiana na wadau wengine, zikiwemo nchi kubwa na zenye uwezo, kuongeza nguvu ya kukabiliana na changamoto hiyo. Juhudi hizi ni endelevu na zinahitaji ushirikiano mpana.


D.      UMOJA WA MATAIFA

32.    Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kushiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa hususan katika masuala ya amani na usalama, haki za binadamu na maendeleo.  Ushiriki huu wa Tanzania umetuletea sifa nyingi pamoja na kuijenga taswira ya nchi yetu katika medani za kimataifa.

33.  Mheshimiwa Spika, katika eneo la amani na usalama, Wizara yangu ikishirikiana na Wizara ya Ulinzi  na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeendelea kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa amani chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa.  Hivi sasa nchi yetu ni moja ya wachangiaji muhimu wa maafisa na askari kwenye misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, wakiwemo wanajeshi, polisi na maafisa magereza. Wote hao wameonyesha uhodari, utii na umakini mkubwa katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kuipatia nchi yetu sifa kubwa Duniani. Kwa kutambua mchango wetu mkubwa hususan kule Darfur, Meja Jenerali Wynjones Mathew Kisamba, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Ardhini wa jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ameteuliwa kuwa Naibu Kamanda wa Vikosi Mahuluti vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Darfur (UNAMID). Naomba tuungane kumpongeza yeye, pamoja na maafisa na askari wetu wote wanaotumikia Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri wanayoifanya.

34.  Mheshimiwa Spika, Tanzania ilishiriki kikamilifu katika Mikutano mikubwa ya Kimataifa  kama vile Jukwaa la Kimataifa la Uchumi (World Economic Forum) huko Davos, Switzerland, mwezi Januari, 2011 na Cape Town, Afrika Kusini mwezi Mei, 2011 ambapo nchi yetu ilipata fursa ya kunadi mkakati wake wa kuboresha kilimo nchini unaojulikana kama “The Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania - SAGCOT ”.  Aidha, mikutano mingine ambayo Tanzania ilishiriki kikamilifu ni pamoja na ule uliohusu Malengo ya Milenia, uliofanyika jijini New York mwezi Septemba, 2010 na ule wa Nchi Maskini Sana Duniani uliofanyika Istanbul, Uturuki mwezi Mei 2011.

35.  Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kupewa heshima kubwa na Umoja wa Mataifa baada ya Katibu Mkuu wa Umoja huo, kumteua Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Tume kuhusu Afya ya Akina Mama na Watoto (Commission on Information and Accountability for Women’s and Children’s Health). Tume hiyo ilipewa jukumu la kuunda mfumo wa kufuatilia ahadi na fedha zilizotolewa na mataifa na vyombo mbalimbali vya kimataifa  na namna zitakavyotumika kuboresha Afya ya Akina Mama na Watoto. Tume hiyo imekamilisha kazi yake na itawasilisha taarifa rasmi katika Kikao kijacho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2011.

36.  Mheshimiwa Spika, kupitishwa kwa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Misaada na Maendeleo nchini (United Nations Development Assistance Plan) utakaotekelezwa  kuanzia Julai, 2011 hadi Juni, 2015 katika kugharamia miradi mbalimbali ni kielelezo kingine cha mafanikio ya  Mradi wa Majaribio unaotekelezwa nchini na Umoja wa Mataifa ujulikanao kama “One UN”.

37.  Mheshimiwa Spika, hakika tunajivunia heshima kubwa ambayo tumepewa na Umoja wa Mataifa, kupitia kwa Bwana Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja huo.  Tunampongeza kwa dhati kwa kuchaguliwa tena kwa kishindo kuongoza Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kwa muhula mwingine wa miaka mitano. Tunaahidi kumpa ushirikiano  wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

E.  KUNDI LA NCHI ZISIZOFUNGAMANA NA UPANDE WOWOTE (NAM)

38.  Mheshimwia Spika, ninayo furaha kulieleza Bunge lako tukufu kuwa Kundi la Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) linatimiza miaka hamsini (50) tangu kuanzishwa kwake.  Kundi hili limeendelea kuwa sauti ya nchi zilizo katika Ukanda wa Kusini mwa Dunia katika kukabiliana na ubabe wa mataifa makubwa. Mikutano ya NAM imeendelea kutoa fursa nzuri kwa nchi wanachama kukutana na kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.  Sherehe za miaka 50 ya NAM zitahitimishwa mjini Belgrade, Serbia (zamani ikijulikana kama Yugoslavia) mwezi Septemba 2011. Kama historia inavyotukumbusha, NAM ilizaliwa jijini Belgrade mwaka 1961.F.  JUMUIYA YA MADOLA

      39.   Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara yangu ipo katika mchakato wa maandalizi ya ushiriki wa Tanzana katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Jumuiya ya Madola (CHOGM) utakaofanyika Perth, Australia kuanzia tarehe 28 hadi 30 Oktoba 2011. Kaulimbiu rasmi ya mkutano huo ni “Building National Resilience, Building Global Resilience”.

40.  Mheshimiwa Spika, Kaulimbiu hii inalenga zaidi katika kutekeleza shabaha mbalimbali za Jumuiya hiyo ambazo ni kuimarisha demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora miongoni mwa nchi wanachama. Aidha, changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia, mathalan, hali ya chakula, kusimamia maliasili, maendeleo endelevu, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na namna ya kujinasua kutoka katika mdororo wa kiuchumi ulioikumba dunia mwaka 2008 zitajadiliwa.

G.     UMOJA WA AFRIKA NA JUMUIYA ZA KIKANDA

Umoja wa Afrika

41. Mheshimiwa Spika, Umoja wa Afrika unaendelea na mchakato wa kubadili Kamisheni yake kuwa Mamlaka kufuatia maagizo yaliyotolewa na Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja huo kwenye kikao chao kilichofanyika Sirte, Libya mwezi Julai 2009. Hatua inayoendelea hivi sasa ni kukamilisha Itifaki ya Bunge la Afrika na Mahakama ya Afrika. Kwa ujumla Umoja wa Afrika unaendelea kuimarika licha ya changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika hususan migogoro, umaskini na maradhi. Umoja huo unafanya kila linalowezekana, kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa na wadau wengine, kukabiliana na changamoto hizo.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

42.  Mheshimiwa Spika, Tanzania inaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ushiriki huu umeleta manufaa mbalimbali katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Katika kupanua wigo wa ushirikiano, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamepitisha Itifaki ya Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya. Itifaki hiyo itazipa Nchi Wanachama fursa ya kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kidiplomasia na kikonseli kupitia Balozi zetu zilizopo nje ya eneo la Jumuiya yetu. Wizara yangu itaendelea kushiriki na kushauri vilivyo, hususan jinsi ya kutengeneza mfumo bora wa kuhakikisha Itifaki hii inatekelezwa bila kuathiri maslahi muhimu ya Taifa letu.

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)

43.  Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha demokrasia inashamiri katika eneo la SADC. Ustawi wa demokrasia umesaidia kudumisha mazingira mazuri ya biashara, uwekezaji, amani na utulivu katika nchi za SADC. Ukomavu wa demokrasia nchini, uliojidhihirisha kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambao ulishuhudiwa na waangalizi zaidi ya 100 kutoka nchi za SADC na kuthibitishwa kuwa ulikuwa huru na wa haki, umezidi kuijengea heshima kubwa nchi yetu, ndani na nje ya bara letu la Afrika.

44.  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka hamsini (50) ya uhuru, nchi yetu imejijengea heshima ya pekee katika harakati za ukombozi duniani, hususan Kusini mwa Afrika. Tumeendelea kuwa wasimamizi wa haki na usawa na hatujawahi kusita kuidai haki hiyo kwa niaba ya wale walionyanyaswa, kubaguliwa, kukandamizwa na kutawaliwa. Vilevile, nchi yetu imekuwa tegemeo la wengi katika usuluhishi na utatuzi wa migogoro iliyopo katika baadhi ya nchi za SADC. Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kuhakikisha heshima hiyo inadumishwa.

45.  Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mchango wetu, SADC ilimtunuku Mtanzania mwenzetu Brigedia Jenerali mstaafu, Balozi Hashim Iddi Mbita nishani ya SADC ya Sir. Seretse Khama (Sir. Seretse Khama SADC Award) kwa mchango wake katika harakati za ukombozi wa Mwafrika. Tukio hili la kihistoria lilifanyika sanjari na maadhimisho ya miaka 30 ya SADC pamoja na ufunguzi wa jengo la Makao Makuu ya SADC lililopo mjini Gaborone, Botswana mwezi Novemba 2010. Kiongozi mwingine aliyewahi kutunukiwa tuzo hiyo ni Mhe. Kenneth Kaunda, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Zambia.

46.  Mheshimiwa Spika, juhudi za kuziunganisha Jumuiya za SADC, EAC na COMESA ili kuwa na eneo moja huru la kibiashara zinaendelea. Mkutano Mkuu wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi zilizo katika eneo linalokusudiwa kuanzishwa ushirikiano, waliweka saini mkataba wa kuanzisha Soko Huru la Pamoja mjini Sandton, Afrika Kusini tarehe 12 Juni, 2011 na wakazindua rasmi majadiliano kuhusu soko hilo. Soko hili litajumuisha nchi 27 kati ya 54 za Afrika ikiwemo Sudan ya Kusini, zenye wakazi wasiopungua milioni 700 na pato la taifa la jumla la takriban dola za kimarekani  trilioni 1.6. Changamoto iliyo mbele yetu ni kujipanga vyema ili tuweze kunufaika na matunda ya ushirikiano huo.
H.          UTEKELEZAJI WA DIPLOMASIA YA UCHUMI

47.    Mheshimiwa Spika, pamoja na ufinyu wa bajeti, Wizara yangu imeendelea kuyapa uzito stahiki masuala ya diplomasia ya uchumi ambayo kimsingi yanahitaji fedha nyingi kuyatekeleza. Katika kufanikisha hilo, Wizara imejishughulisha katika maeneo ya kutafuta wawekezaji, kuhamasisha watalii na kutafuta masoko ya bidhaa zetu. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu ziara za viongozi wetu nje ya nchi na ushiriki wa Tanzania katika  Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPCs).

48.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/2011 viongozi wakuu wa kitaifa walifanya ziara na kuhudhuria mikutano katika nchi mbalimbali duniani zenye lengo la kukuza diplomasia ya uchumi, kukuza ushirikiano na kuimarisha ujirani mwema baina ya Tanzania na nchi nyingine pamoja na taasisi na mashirika ya kimataifa. Aidha, katika kipindi hiki viongozi kutoka nchi mbalimbali pamoja na taasisi za kikanda na kimataifa waliitembelea Tanzania.

49.    Mheshimiwa Spika, matokeo ya ziara hizi za viongozi wetu na viongozi kutoka nje, ni pamoja na kusainiwa kwa mikataba ya ushirikiano, kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii nchini. Kwa mfano; ziara ya Mhe. Lula Da Silva, Rais wa Jamhuri ya Brazil aliyoifanya mwezi Julai, 2010 ilifanikisha kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya shirika la petroli la Brazil (Petrobras) na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC); mkataba wa makubaliano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Mazingira ya Jamhuri ya Brazil kuhusu kupunguza hewa chafu itokanayo na ukataji miti na uharibifu wa mazingira na makubaliano ya ushirikiano katika masomo ya Diplomasia baina ya Chuo cha Diplomasia cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi ya  Ruo Branco ya Jamhuri ya Brazil. Na mwisho, mazungumzo ya Tanzania kufutiwa deni lake na Brazil yalifanyika.

50.    Mheshimiwa Spika, mfano mwingine ni ziara ya mwezi Aprili, 2011 ya Mhe. Dkt. Manmohan Singh, Waziri Mkuu wa India, iliyopelekea makubaliano ya awali ya Ushirikiano wa pamoja baina ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Hospitali ya Apollo ya India kuhusu kuanzisha hospitali kubwa ya kisasa itakayokuwa inatoa huduma za magonjwa ya moyo, ubongo na mifupa na Mpangokazi wa pamoja baina ya Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo la Tanzania (SIDO) na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo la India. Aidha, katika ziara hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya India zilifikia makubaliano ya mikataba ya kutolipisha kodi mara mbili na kuzuia ukwepaji wa kodi ya mapato.

51.  Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mikataba mbalimbali baina ya Tanzania na nchi nyingine duniani, Mikataba ya Kikanda na Mikataba ya Uenyeji. Katika kipindi cha 2010/2011, Wizara yangu imesimamia majadiliano yaliyofanikisha kusainiwa kwa mikataba ishirini (20) katika nyanja za biashara, mazingira, sayansi na teknolojia, utamaduni, usafirishaji na haki za binadamu. Tunatarajia Mikataba yote iliyosainiwa na mingine itakuwa ni chachu ya maendeleo kwa Tanzania. Natoa rai kwa taasisi za Serikali na nyinginezo zijipange vizuri kufanikisha utekelezaji wa Mikataba hii kwa manufaa ya Watanzania.

Kuwashirikisha Watanzania wanaoishi Ughaibuni (Diaspora)

52.    Mheshimiwa Spika, Wizara yangu tayari imeunda Idara ya Diaspora na tumefanikiwa kuwafikia kwa wingi Watanzania walioko nje kupitia mikutano na majukwaa mbalimbali na kupata maoni yao. Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Rais wa Zanzibar ameunda Kitengo cha Diaspora kinachoongozwa na Naibu Katibu Mkuu ambacho kipo chini ya ofisi yake na tunashirikiana nacho kwa karibu sana. Aidha, yapo maelewano na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Benki Kuu, Kituo cha Uwekezaji, Mamlaka ya Mapato, Shirika la Nyumba la Taifa, Mfuko wa Uwekezaji (UTT), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na wadau nje ya Serikali kama Benki za CRDB, Benki ya Exim (Tanzania), Commercial Bank of Africa, na Mawakala Binafsi wa Ajira (Recruitment Agencies). Maelewano haya yanasaidia katika mkakati mzima wa kujenga mazingira ya kisheria na kisera ya kuwezesha Diaspora kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.

53.    Mheshimiwa Spika, hatua iliyo mbele yetu ni kwa Wizara yangu kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwanasheria Mkuu, kujenga mazingira mazuri kwa wanadiaspora na kuondoa kero ambazo zinaathiri jitihada zao za uchangiaji katika maendeleo ya nchi yetu.  Hivi sasa Wizara zetu zinajiandaa kuwasilisha Waraka kwenye Baraza la Mawaziri, ili ujadiliwe na kisha kwa wakati muafaka, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kutakiwa kuwasilisha rasmi mbele ya Bunge lako Tukufu Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uraia kwa majadiliano. Kwa kuwa mchakato wa suala hili unagusa Katiba, ni azma yetu kuona kwamba suala hili linakwenda pamoja na mchakato wa Katiba mpya. Ni dhamira ya Wizara yangu kuona suala la Uraia wa nchi mbili linazinduliwa sanjari na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mchakato wa Kujitathmini kwa Utawala Bora Barani Afrika (APRM)

54.  Mheshimiwa Spika, mchakato wa APRM nchini Tanzania sasa unaelekea ukingoni baada ya kusimama mwaka jana kutokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Tunatarajia kupokea timu ya wataalamu kutoka makao makuu ya APRM mwezi Agosti, 2011 kwa ajili ya maandalizi ya tathmini itakayofanyika mwezi Septemba 2011. Inatarajiwa kuwa, taarifa kamili ya Tanzania itawasilishwa katika mkutano mkuu wa nchi wanachama wa APRM mwezi Julai 2012.

Huduma za Kikonseli

55. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ndiyo yenye dhamana ya kulinda maslahi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Kufuatia machafuko yaliyotokea hivi karibuni katika nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, hatua za makusudi na za haraka zilichukuliwa ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanaoishi katika nchi hizo hawapatwi na madhara yoyote. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwarudisha nyumbani watanzania themanini na tatu (83) kutoka Misri na Wanane (8) kutoka Libya; kuufunga kwa muda Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, kukusanya taarifa zote muhimu na kuziwasilisha Wizarani; kuwaita na kuzungumza na wawakilishi wa nchi husika hapa Tanzania ili kufahamu kwa kina mustakabali na hatua ambazo Serikali zao zinachukua katika kukabiliana na machafuko hayo. Aidha, Wizara imetoa taarifa kwenye vyombo vya habari juu ya maendeleo ya hali ya Watanzania na hali ya usalama katika nchi hizo.

56.  Mheshimiwa Spika, hali hii inatoa changamoto kwa Serikali kuchukua hatua za haraka katika kuwaokoa raia wake kila inapobidi. Hivyo, ninatoa wito kwa Watanzania wanaoishi nchi za nje kujiorodhesha kupitia jumuiya zao katika Ofisi za Balozi zetu ili kuwafikia kwa urahisi kila inapohitajika.
       
Heshima ya Tanzania Duniani

    57.  Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali nchi yetu imeendelea kujijengea heshima kubwa Kimataifa, kama Taifa lililokomaa katika nyanja za Utawala Bora, Usuluhishi wa Migogoro, Demokrasia, Utawala wa Sheria, utawala unaojali haki za binadamu na Utawala unaowekeza kwa watu wake.  Hali hii imefanya nchi yetu kuzidi kuaminiwa na mataifa mengine, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa.

    58.  Mheshimiwa Spika,  kutokana na hayo, Umoja wa Mataifa umemteua Rais wetu kuwa Mwenyekiti mwenza wa Kamisheni ya kupunguza vifo vya watoto na akina mama na pia imemteua Meja Jenerali Kisamba kuwa Naibu Kamanda wa Majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda Amani Darfur, Sudan. Aidha, viongozi wa Umoja wa Afrika wamepitisha jina la mtanzania Ludovick Utouh, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa mgombea pekee wa Bara la Afrika atakayewania nafasi ya ujumbe wa Bodi ya ukaguzi ya Umoja wa Mataifa kwenye uchaguzi utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu New York. Tuna hakika kabisa ya kushinda.  Naye mtanzania Prof. Chris Peter Maina amepitishwa na viongozi hao hao wa Umoja wa Afrika kugombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Sheria ya Umoja wa Mataifa.  Vile vile, Umoja wa Afrika kwa Kauli moja umepitisha jina la Tanzania kugombea nafasi ya ujumbe kwenye Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic (International Atomic Energy Agency).

    59.  Mheshimiwa Spika, nayasema haya yote ili kuwaeleza watanzania kuwa nchi yetu inaheshimika sana Duniani na tuwapuuze wale wachache wanaobeza kuwa nchi hii haiheshimiki Duniani!  Tunaheshimika sana.

60.  Mheshimiwa Spika,  hivi karibuni, Taasisi ya Kitaalamu ya ”Fund for Peace” ilitoa tathmini yake ambayo huitoa kila mwaka kuonyesha hali ya Usalama duniani.  Tathmini hiyo huzingatia vigezo kumi na mbili vikiwemo idadi ya watu, watu wanaolazimika kuwa wakimbizi katika nchi; uhasama na visasi baina ya makundi; hali ya haki za binadamu na utawala wa sheria; kukubalika kwa Serikali; mwenendo wa vyombo vya Usalama; taswira ya utumishi wa umma; tofauti za mgawanyo wa keki ya taifa; tofauti za matabaka ya umangimeza (factionalized elites); na uwezo wa kuhimili shinikizo kutoka nje.  Katika ripoti yao ya mwaka 2011, Tanzania ni moja kati ya nchi zilizoonekana kuwa salama zaidi dhidi ya hatari za kiusalama.  Tanzania ni nchi ya 65 kati ya nchi 193 duniani na inaongoza nchi zote za Afrika Mashariki na za SADC kwa amani na usalama.  Tuna kila sababu ya kuienzi amani yetu tunapoadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu na tusikubali kuruhusu mtu au watu wachache kuvuruga amani nchini.I.            UTAWALA NA MAENDELEO YA WATUMISHI WIZARANI NA KWENYE BALOZI ZETU NJE

61.    Mheshimiwa Spika, Wizara ina jumla ya watumishi 440, Kati ya watumishi hao 249 wako Makao Makuu, 19 wako Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar na 172 wako katika Balozi zetu Nje. Katika mwaka wa fedha 2010/11 Wizara iliajiri jumla ya watumishi wapya 49 kati ya 53 walioidhinishwa. Watumishi 4 ambao walifaulu usaili hawakuweza kujiunga na Wizara kutokana sababu mbalimbali.

62.    Mheshimiwa Spika, jumla ya watumishi 29 walipelekwa mafunzoni, kati ya hao 20 walipelekwa mafunzo ya muda mrefu na 9 mafunzo ya muda mfupi ili kuongeza ujuzi katika taaluma zao.  Aidha, jumla ya watumishi 59 walipandishwa vyeo na wengine 12 walithibitishwa kazini katika mwaka wa fedha 2010/11. Wizara itaendelea kusimamia maendeleo ya watumishi na kuboresha maslahi yao kadri hali itakavyoruhusu.
63.    Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyoelezwa hapo juu, changamoto kubwa inayoikabili Wizara yangu ni ufinyu wa bajeti. Hali hiyo imesababisha Wizara kutofikia ipasavyo malengo ya utekelezaji wa sera ya mambo ya nje.
J.     UDHIBITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA

64.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2009/2010, Wizara yangu imeongeza ufanisi katika masuala ya usimamizi wa bajeti na fedha kwa ujumla ambapo kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Balozi nane (8) zilipata Hati Safi za Ukaguzi wa Hesabu ikilinganishwa na Balozi tano (5) zilizopata hati kama hiyo kwa mwaka 2008/2009. Balozi ishirini na moja (21) zilipata Hati safi zenye Masuala ya Msisitizo ikilinganishwa na Balozi ishirini na tatu (23) mwaka 2008/2009. Aidha, Balozi mbili (2) zilipata Hati zenye Shaka ikilinganishwa na Balozi tatu (3) zilizopata Hati kama hiyo mwaka 2008/2009. Kwa mwaka 2009/2010, hakuna Ubalozi uliopata Hati isiyoridhisha ikilinganishwa na Ubalozi mmoja (1) kwa mwaka wa fedha 2008/2009. Wizara yangu itaendelea kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha za Serikali Wizarani na katika balozi zake thelathini na mbili (32) kwa misingi ya Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

65. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti matumizi ya fedha balozini, tayari Balozi saba (7) zimewekewa Mtandao wa Malipo ya Serikali (Integrated Financial Management System - IFMS). Wizara yangu kwa kushirikiana na HAZINA itaendelea kusimamia utekelezaji wa mpango huo katika Balozi zilizosalia. Vile vile, Wizara imeweka saini mikataba na Mabalozi wa Heshima kumi na wanne (14), ili kudhibiti taratibu za kukusanya maduhuli kwenye Balozi hizo. Wizara itaendelea kutekeleza zoezi hilo kwenye Balozi za Heshima zilizosalia.

K.       TAASISI ZILIZOKO CHINI YA WIZARA

Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)

66.    Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea na hatua za kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mikutano mjini Arusha kitakachojulikana kama Mt. Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC). Mradi huo ni moja ya nguzo muhimu utakaokiwezesha kituo kupanua wigo wa huduma zake.

67.    Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimepata Hati Safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2010. Kituo kilipata faida ghafi ya shilingi milioni mia tisa themanini na nane, mia nane tisini elfu na mia mbili sitini na sita (988,890,266.00) na kinaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi na bila kuwa tegemezi kwa Serikali.  Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012 Kituo kimepanga kuingiza mapato ya shilingi bilioni saba, milioni mia saba na sitini na tisa, mia saba arobaini na tatu elfu na mia saba thelathini na saba (7,769,743,737.00) kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato na kinategemea kupata ziada ghafi ya shilingi bilioni moja, milioni mia nne na tano, mia nane arobaini na moja na mia tisa na thelathini na moja (1,405,841,931.00).

Chuo cha Diplomasia
68.    Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kulieleza Bunge lako tukufu kuwa Chuo cha Diplomasia sasa kimepata usajili wa Baraza la Ithibati ya Elimu ya Ufundi (National Council of Technical Education - NACTE). Hatua hii itafanya mafunzo yanayotolewa na Chuo kutambulika kitaifa na kimataifa, hivyo kufanya idadi ya wanafunzi kuongezeka kuliko ilivyokuwa awali.

69.    Mheshimiwa Spika, Chuo kinaendelea kuishauri Wizara yangu katika masuala mbalimbali ya kidiplomasia. Aidha, Chuo kimekuwa kikijishughulisha na utoaji wa taaluma ya utatuzi wa migogoro, tafiti, na ushauri wa kitaalamu katika masuala ya itifaki, diplomasia ya uchumi, stratejia, menejimenti ya mahusiano ya nje na kutoa mafunzo kwa watumishi wa Wizara na wanafunzi wengine kutoka ndani na nje ya nchi.

L.       MAPATO NA MATUMIZI 2010/2011

70.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 Wizara yangu ilipangiwa kutumia kiasi cha shillingi bilioni mia moja kumi na mbili, mia tatu thelathini na sita milioni na mia tisa ishirini na nane elfu (112,336,928,000.00) Kati ya fedha hizo  shilingi bilioni sitini na nne, arobaini milioni na mia saba tisini na mbili elfu (64,040,792,000.00) ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida (OC); shilingi bilioni tatu, mia saba tisini na sita milioni, mia moja thelathini na sita elfu (3,796,136,000.00) ni kwa ajili  ya  mishahara ya watumishi na shilingi bilioni arobaini na nne na  milioni mia tano (44,500,000,000.00)  ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

71.    Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2011 Wizara ilikuwa imepokea kutoka HAZINA kiasi cha shilingi bilioni tisini na tatu, milioni mia tisa hamsini na tisa, mia tano arobaini na tisa elfu na mia sita na ishirini (93,959,549,620.00). Kiasi hiki cha fedha ni sawa na asilimia themanini na tatu nukta nne (83.40%) ya bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2010/2011.

72. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Balozi zake ilitegemea kukusanya kiasi cha shilingi  bilioni kumi na mbili, mia saba thelathini na mbili milioni na mia tatu elfu (12,732,300,000.00).  Hadi kufikia tarehe 31 Juni, 2011 kiasi cha shilingi bilioni kumi na tano, mia saba hamsini na sita milioni, mia tisa arobaini na tisa elfu na mia tisa thelathini na mbili (15,756,949,932.00) kilikusanywa, kikiwa ni makusanyo ya maduhuli Balozini na Makao Makuu. Kiasi hiki cha fedha ni sawa na asilimia mia moja ishirini na tatu nukta saba sita (123.76%) ya makusanyo ya fedha zote za maduhuli zilizokadiriwa kukusanywa Balozini na Makao Makuu kwa mwaka wa fedha 2010/2011.

M.    MALENGO YA WIZARA KATIKA MWAKA WA FEDHA WA 2011/2012
73.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, pamoja na mambo mengine, Wizara yangu imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 kama ifuatavyo:-
(a)      Kuitangaza nchi yetu kama moja ya nchi duniani zenye mazingira muafaka kwa ajili ya uwekezaji hasa kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa Kitaifa;
(b)     Kutangaza utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii tulivyonavyo na kuvutia watalii wengi kutoka mabara yote ya dunia waje kuviona;
(c)      Kuzitafutia masoko bidhaa zetu zenye ubora unaotakiwa katika nchi za nje kwa kushauriana na wazalishaji wa ndani wa bidhaa hizo;
(d)     Kudai mageuzi ya Umoja wa Mataifa hususan katika Baraza la Usalama la Umoja huo, kwa kuzingatia hoja ya wingi wa agenda zinazojadiliwa na kuamuliwa na Baraza hilo bila ya uwakilishi wetu;
(e)      Kushiriki katika utatuzi na usuluhishi wa migogoro inayotokea barani Afrika na nchi nyingine duniani, kama vile mgogoro wa Libya.
(f)       Kuendelea kutekeleza mpango wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya Ofisi na makazi balozini.
(g)      Kukamilisha mchakato wa kuitambua na kushirikisha Jumuiya ya Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa letu.N.     MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2011/2012
74.    Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu kazi zilizotajwa hapo juu, Wizara yangu imepangiwa kiasi cha shilingi bilioni mia moja ishirini na tano, milioni mia moja na mbili na mia nane sabini na tano elfu (125,102,875,000.00) kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni sabini na sita, milioni mia tatu themanini na saba na mia moja themanini na saba elfu (76,387,187,000.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (OC), shilingi bilioni nne, milioni mia mbili kumi na tano na mia sita themanini na nane elfu (4,215,688,000.00) ni kwa ajili ya mishahara na shilingi bilioni arobaini na nne na milioni mia tano (44,500,000,000.00) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.  
75.    Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara (OC) shilingi bilioni mbili, milioni arobaini na tisa na mia nne sabini na tano elfu (2,049,475,000.00) ni kwa ajili ya mchakato wa APRM, shilingi bilioni moja, milioni mia tano na nne, mia tano sabini na nne elfu na mia nne sabini na nane (1,504,574,478.00) ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na shilingi bilioni moja, milioni mia nne, mia nne thelathini na sita elfu na mia mbili ishirini na saba (1,400,436,227.00) ni kwa ajili ya fedha za mishahara na Matumizi ya Kawaida ya Chuo cha Diplomasia.

76.    Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara yangu inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na nne, milioni mia nane sabini na mbili na mia nne tisini na mbili elfu (14,872,492,000.00) kama maduhuli ya Serikali. Kwa maana ya utekelezaji wa Bajeti, kiasi hiki cha maduhuli tayari kimehesabiwa kama sehemu ya matumizi ya kawaida ya Wizara yangu.

77. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. 

No comments: