Wednesday, November 14, 2012

MAREKANI YAZIDI KUBANWA DHIDI YA MSIMAMO WAKE JUU YA VIKWAZO KWA CUBA


Na Mwandishi Maalum
 Nchi 188 kati ya 193 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa,  zimepiga kura ya ndiyo kuunga mkono   Azimio linaloitaka   Marekani  kuiondelea  Cuba vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha.
 Upigaji kura  huo ,ulifanyika siku ya  Jumanne hapa Makao  Makuu ya Umoja wa Mataifa,  ikiwa ni   mwaka wa 21 ambapo nchi wanachama zimekuwa zikilipigia kura azimio hilo bila ya kuchoka.
Wakati   nchi 188 zilipiga kura ya  ndiyo , nchi tatu ikiwamo Marekani ilipiga kura ya hapana. Nchi nyingine zilizopiga kura ya hapana ni Israel na Palau, huku Marshall Islands na Micronesia zikipiga kura ya kutofungamana na upande wowote.  Baada ya Rais wa Baraza Kuu la 67 kutangaza matokeo hayo, wajumbe walishangilia kwa nguvu.
Kabla ya   kulipigia kura Azimio hilo ambalo liliwasilishwa na  Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bw Bruno Rodriquez Parrila. Wawakilishi wa nchi mbalimbali  walizungumza   kuonyesha mshikamano wao na Cuba kwa  kusisitiza pamoja na  mambo mengine kwamba sasa imetosha Marekani ifikie mahali na kukubali ukweli  halisi wa mambo na kuondoka vikwazo hivyo  ambavyo vimedumu kwa   miaka 50  tangu  kuasisiwa kwake  mwaka 1962.
Aidha, wasemaji kadhaa wameeleza kwamba vikwavyo hivyo na ambavyo vimepitwa  na wakati vinakwamisha juhudi za Cuba kujiletea maendeleo , kuupiga vita umaskini na   vinaifanya Cuba ishindwe kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Millenia.
Vilevile  wawakilishi hao wakaeleza bayana kwamba kuendelea kwa vikwazo hivyo siyo tu  ukiukwaji wa sherika za kimataifa, lakini pia   ni kubinya uhuru wananchiwa Cuba kujimulia mambo yao.
Baadhi ya wasemaji kama vile mwakilishi wa Urusi yeye alikwenda mbali zaidi kwa kusema, msimamo wa nchi yake dhidi ya vikwazo hivyo unajulikana wazi na haujawahi kubadilika.
Akasema nchi yake inapinga vikwazo vya  Marekani kwa Cuba na kusisitiza kwamba vikwazo hivyo ni masalia ya vita baridi ambayo yamepitwa na wakati.
Akiwasilisha Azimio hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Parrila, pamoja na kuainisha madhara na hasara  zinazotokana na  vikwazo hivyo ambapo alisema madhara ya kiuchumi katika miaka hiyo 50 yanakadiriwa kufikia trillion moja na dola bilioni sita  hadi mwishoni kwa mwaka jana.
 Ameitaka  serikali ya Obama  na hasa baada ya kurejea tena madarkani,kuonyesha utashi wa kisiasa kwa  kutekeleza  kwa ukamilifu uondoaji wa vikwazo hiyo badala ya kufungua milango nusu nusu.
 Kwa Upande wake, msemaji wa Marekani, akizungumza kwa nini nchi yake imepiga kura ya kupinga azimio hilo, alisema kwamba si kweli kwamba nchi yake imekuwa  ndiyo chanzo cha  wananchi wa Cuba kuendelea kuteseka  bali  wa kulaumiwa ni Serikali yenyewe ya  Cuba.
Akasema inachofanya serikali yake ni kuwawezesha wananchi wa Cuba kujiamulia mambo yao wenyewe na kuitaka serikali ya Cuba kuondoa sheria kandamizi  zinazowabana wananchi wake hoja ambayo ilipingwa vikali na msemaji wa Cuba.

No comments: