Tukio hilo limefanyika leo kuanzia katika Ukumbi wa NSSF mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na waumini na viongozi wa dini ya mbalimbali wakiongozwa na Sheikh Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ismail Habibu Makusanya.
Wengine waliohudhuria ni viongozi wa vyama vya siasa na serikali,viongozi wa madhehebu mengine ya dini wakiongozwa na Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Dr. John Nkola na watu mbalimbali wenye mapenzi mema.
Akizungumza wakati wa kula chakula cha pamoja “Futari” mwandaaji wa chakula hicho ambaye ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Erasto Kwilasa alisema aliwashukuru waumini wa dini ya kiislamu kukubali kushiriki na kudai kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuonesha kwa vitendo kuwa anawapenda watu wa Shinyanga bila kujali makabila,dini wala rangi zao.
“Nawashukuruni sana tumekusanyika hapa,tupo hapa katika kushirikiana pamoja kwa kupata futari ya pamoja,mimi binafsi naamini katika ibada hii tutakuwa tumetenda jambo jema mbele ya mwenyezi mungu hasa katika kutekeleza nguzo muhimu miongoni mwa nguzo tano za kiislamu,funga ya mwezi mtukufu”,alisema Kwilasa.
“Ndugu zangu mlikuwa na nfasi ya kutoa udhuru kwamba mimi ni kiongozi wa chama,lakini kwa upendo mlionionesha leo hii,mmedhihirisha ule usemi wa serikali na chama havina dini bali wanachama wake wana dini zao na hii ndiyo maana mmekuja kwa wingi na mpaka sasa tupo pamoja hapa bila ubaguzi wa aina yoyote”,aliongeza Kwilasa.
Kwilasa alitumia fursa hiyo kuwataka wanasiasa kuacha kubaguana kwani binadamu wote ni wa mwenyezi mungu huku akimuomba mungu kupokea funga za waumini wote wa mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla.
“Kwa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na rais John Pombe Magufuli na timu yake yote,naomba tuendelee kumuombea sana kwa mungu ili aweze kufanikisha malengo yake aliyowaahidi wananchi”,alisema Kwilasa.
Katika hatua nyingine Kwilasa aliwaomba viongozi wote wa madhehebu ya dini kusaidiana na viongozi wa serikali mkoa wa Shinyanga kupiga vita vitendo vya mauaji dhidi ya vikongwe,ubakaji na ulawiti kwa watoto,utumiaji wa madawa ya kulevya na ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sheikh Ismail Habibu Makusanya alimpongeza mwenyekiti huyo wa CCM kuandaa chakula cha pamoja kwa ajili ya waumini wa dini ya kiislamu na kusema kuwa kitendo alichokifanya kina dhawabu kubwa kwa mwenyezi mungu.
“Ukimuona mja anashughulika kuwalisha watu, wa kweli na wasio wakweli,wacha mungu na wasio wacha mungu huyu ameshika kazi ya mungu..sasa mwenyeji wetu ulichokifanya hapa sisi hatuwezi kukulipa lakini hiki ulichofanya ni kafara kubwa sana katika maisha yako ,ni hifadhi kubwa sana katika maisha yako,ni sadaka kubwa sana,kuwaita na kuwalisha waliofunga ni kazi kubwa,mungu akuzidishie pale ulipotoa”,aliongeza Sheikh Makusanya.
Naye Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Dr. John Nkola alisema ni mara kwanza yake ya kwanza kukaribishwa kwenye futari kubwa kama hiyo na kuwashukuru waislamu kukusanyika pamoja kushiriki pamoja kwa futari na kwamba mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kwa ajili ya utukufu wa mungu.
Askofu Nkola alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania kujenga mshikamano na umoja uliopo kwani umoja wa madhehebu ya dini ndiyo uzima na amani ya taifa la Tanzania.
“Tukishikamana na kumhubiri mwenyezi mungu ambaye ni wa amani,nchi yetu itaendelea kuwa na amani sana,tuendelee kushikamana,na tuendelee kumuombea rais Magufuli anafanya mambo makubwa ambayo siyo kila mtanzania atayapenda hata kidogo”,alisema Askofu Nkola
“Sasa sisi kazi yetu siyo siasa lakini maandiko na misahafu inatuagiza kuwaombea wale ambao mwenyezi mungu amewapa madaraka ya kutawala,tumuombee sana rais wetu,pamoja na serikali yetu na nchi yote kwa ujumla tuendelee kutulia kwa amani,tuendelee kuwa kimbilio la wanyonge wanaonyanyaswa katika nchi zao”,aliongeza askofu Nkola.
Malunde1 blog huwa haipitwi na matukio,Mwandishi mkuu wa mtandao huu,Kadama Malunde alikuwepo eneo la tukio,ametusogezea picha 85..Shuhudia mwenyewe hapa chini
Juni 29,2016 kumefanyika tukio muhimu mjini Shinyanga ambapo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga ndugu Erasto Kwilasa (pichani) amewaandalia chakula cha pamoja “futari” waumini wa dini ya kiislamu mkoa wa Shinyanga ikiwa ni sehemu ya kuutukuza mwezi mtukufu wa Ramadhani.











