Saturday, January 5, 2019

WAZIRI MBARAWA ASHIRIKI UPANDAJI MITI 15,000 CHANZO CHA MTO RUVU

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa ameshiriki zoezi la upandaji wa miti 12,000 katika bonde la Mto Ruvu kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji.

Zoezi hilo limesimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) na wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo kutoka Mikoa mbalimbali kushiriki katika mitambo ya Ruvu Chini.

Akizungumza baada ya kumaliza kupanda miti, Prof Makame amesema elimu waliyoitoa kwa wananchi ya kukaa umbali wa mita 60 kutoka vyanzo vya maji haitoshi bali wanatakiwa kushirikishwa katika kuvilinda na kuacha kufanya shughuli za kijamii.

Mbarawa amesema, lengo la Wizara ni kuona vyanzo vya maji na kampeni hii iendelee kwenye vyanzo vyote vya maji ili kufikia malengo ya Serikali kufika 2020 asilimia 95 ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kupata maji safi na salama.

Mbali na hilo,Prof Mbarawa ameitaka mamlaka hiyo kutafuta ufumbuzi wa haraka wa Ukadiriaji wa ankara za maji usio na uwiano na kurekebisha dosari mbalimbali zinazoiyumbisha ikiwamo upotevu mkubwa wa maji, ufinyu wa mapato na urasimu wa utoaji huduma.

Mbarawa alisema haridhishwi na utendaji wa Kitengo cha Masoko cha Dawasa na kumekuwapo na malalamiko kwa wateja wanaokadiriwa ankara kubwa na wapo wengine wanaotumia kiasi kikubwa cha maji hasa taasisi na makampuni huku wakilipa ankara ndogo hali inayoisababishia hasara Dawasa.

"Idara ya masoko na biashara nataka ibadilike nataka waone kwamba wakiona tatizo lolote kwenye mfumo wao wa kompyuta waweze kujua pale kuna shida," alisema Mbarawa.Alisema kutokana na hali hiyo, kitaanzishwa kitengo cha Udhibiti wa mapato (Revenue Investigation Unit) kitakachoshughulikia changamoto hiyo.

Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema lengo la mamlaka hiyo ni kupanda miti 100,000 ila kwa leo wameweza kupanda miti 12,000 ingawa awali walishapanda miti 3000 .Amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika chanzo cha Mto Ruvu kwa wananchi kufanya shughuli za kijamii na tumeanzia hapa ila tutaenda hadi Morogoro unapoanzia Mto Ruvu

Akizungumzia upotevu wa mapato, Luhemeja amekiri kuwapo kwa tatizo hilo ambalo hasa linajitokeza kwenye taasisi na kampuni kubwa."Tunachangamoto ya makusanyo lakini kwa maana yakuongeza nguvu tunakwenda kuwa na kitengo maalumu cha uchunguzi ambacho kazi yake kubwa ni kuchunguza mapato yote ya ndani pamoja na matumizi yake," alisema.

Alisema kitengo hicho kitaanza kazi wiki ijayo na kwamba lengo kubwa ni kuhakikisha mamlaka inapata pesa ili kufikia asilimia 95 ya usambazaji maji ifikapo 2020.Kwenye mpango huo, jumla ya miti 15,000 ilipandwa huku lengo likiwa ni kufikia miti 100,000 kwenye vyanzo vyote vya maji vya mto huo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akishiriki zoezi la upandaji wa miti katika chanzo cha Mto Ruvu Leo na kusisitiza Wananchi washirikishwe kulinda vyanzo hivyo
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja  akishiriki zoezi la upandaji miti leo Mkoani Pwani
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akijadiliana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati wa zoezi la upandaji wa miti katika chanzo cha Bonde la Mto Ruvu leo Mkoani Pwani.
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa akiwa anaelekea eneo la bonde la Mto Ruvu leo Mkoani Pwani

No comments: