Monday, January 7, 2019

Wahitimu wa chuo cha NDF Waelezwa Fursa za Uwekezaji Zinazopatikana Rukwa

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amefafanua fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana katika Mkoa hasa sekta ya kilimo kwa wahitimu wa mafunzo kwa vitendo kutoka katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi waliotembelea mkoani hapa ili kujionea maendeleo ya mkoa.

Wahitimu hao kutoka katika nchi kadhaa barani Afrika wamelenga kutembelea katika viwanda vikubwa vinavypoaptikana katika mkoa, maeneo ya uwekezaji wa kilimo, kufika kwenye vivutio vya utalii, machimbo ya makaa ya mawe pamoja na hifadhi za misitu.

Mh.Wangabo alisema kuwa uwekezaji wa kwenye viwanda unahitajika kwasababu ya uwepo wa mazao ya kulisha viwanda hivyo ikiwemo viwanda vya kuchakata mahindi, maharage na mpunga na kuwaondoa shaka juu ya upatikanaji wa umeme kwani hadi kufikia mwaka 2020 vijiji vyote vya mkoa wa Rukwa vitakuwa na umeme.

“Maeneo mazuri ya uwekezaji upo kwenye viwanda hasa viwanda vya kuchakata mazao ndani ya mkoa wetu, pia mwaka huu tuna zao la alizeti kama zao la Kimkakati ambapo hadi sasa kuna tani za mbegu zaidi ya 11,000 ambazo zimeshanunuliwa na wakulima na kupandwa na hivyo tunategemea uzalishaji mkubwa wa alizeti kwa mwaka huu na hivyo tunawaalika wawekezaji kuweka viwanda vya uchakataji wa alizeti ikiwa ni zao la kimkakati kwenye mkoa wetu.” Alisema.

Aidha, alibainisha kuwa katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano, mkoa umejipanga kulima zao la kahawa ambalo ni moja ya mazao matano ya kimkakati kwa serikali, na kusisitiza kuwa upatikanaji wa samaki katika ziwa Tanganyika na ziwa Rukwa bado unahitaji uwekezaji ili kukuza sekta hiyo na hatimae kukuza vipato vya wavuvi wa maeneo ya maziwa hayo, huku akielezea uboreshwaji wa miundombinu ya barabara na kiwanja cha ndege cha mkoa.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Brigedia Generali Mohamed Montaser muhitimu kutoka nchini Misri aliyetaka kujua maeneo ya vipaumbele katika uwekezaji kwa mkoa wa Rukwa. Halikadhalika, Kiongozi wa wahitimu hao Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza SACP Justine Kaziulaya aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Rukwa kwa mapokezi mazuri waliyoyapata na kuomba kupokewa tena endapo watarudi Mkoa wa Rukwa katika miaka inayofuata.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Benard Makali (kulia) akipokea moja ya zawadi alizopewa na Uongozi wa chuo cha Ulinzi nchini ikiwasilishwa na Kiongozi wa Msafara huo Commodore M. Mumanga
Picha ya apmoja kati ya Wahitimu wa Chuo cha Ulinzi nchini pamoja na Wataalamu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakiongozwa na Mkuu wa mkoa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu toka Kulia).
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia)akipokea moja ya zawadi alizopewa na uongozi wa chuo cha Ulinzi nchini kama shukrani ya kuwapokea vizuri katika Mkoa, zawadi iliyowasilishwa na Kiongozi wa Msafara huo Commodore M. Mumanga. 

No comments: