Monday, January 7, 2019

SERIKALI YAZIPA KANDARASI YA THAMANI YA 2.9BN KAMPUNI ZA VIJANA KUTEKELEZA MAFUNZO YA KILIMO CHA KITALU NYUMBA

Serikali kupitia Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imezipa Kandarasi ya thamani ya shilingi 2.9 bilioni kampuni tatu za vijana wa Kitanzania ili kutekeleza mafunzo kwa wakufunzi ya kilimo cha Kitalu Nyumba (Green House). 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana Mhe.Anthony Mavunde wakati akizindua mafunzo hayo  Januari 05, 2019 yanayoendelea katika Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro. 
Programu hiyo ambayo itatumia jumla ya shilingi 2.9bilioni katika utekelezaji wake ambapo kampuni zilizoshinda kandarasi hiyo ni Kampuni za vijana wazalendo wa kitanzania ambao ni wabobezi katika masuala ya kilimo ikiwemo kampuni na Royal Agriculture Ltd, Holly Agriculture  Group Ltd, na SUGECO. 
Mafunzo haya yatafanyika katika Mikoa yote Tanzania Bara na kuhakikisha Halmashauri 84 zinafikiwa kwa awamu hii ya kwanza lengo likiwa ni  kuwajengea vijana ujuzi kupitia kilimo cha kisasa ambapo tayari kwa mwaka huu wa fedha imeanza mafunzo hayo  kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (greenhouse). 
“Kwa kuanzia tutahakikisha kila Halmashauri tunatoa mafunzo kwa vijana 100 na kati yao vijana 20 watapatiwa mafunzo ya kujenga Vitalu Nyumba ili kwa wale watakaopenda kuendelea na kilimo hiki wasikose wataalamu wa kuwajengea Vitalu hivyo ”alisisitiza Mavunde. 
Aidha, Amewataka vijana kutumia fursa ya kilimo katika kujikwamua na changamoto za ajira na kuelezea umuhimu wa kilimo katika kuongeza pato la Taifa na kuchangia katika uchumi wa viwanda nchini.

“Wote tunatambua kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu kwani kwasasa kimeajiri takribani asilimia 65.7 ya nguvu kazi nchini na kinachangia asilimia 29.1 ya pato la taifa, pia sekta ya kilimo ndiyo chanzo kikuu cha chakula, ajira, na malighafi ya viwanda”Alisisitiza Mavunde.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO Bw.Revocatus Kimario alieleza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanafikia kundi kubwa la vijana nchini na kushukuru mchango wa serikali katika programu za ukujazi ujuzi kwa vijana.

“Kipekee naishukuru Wizara hii kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kuhakikisha inatoa mchango mkubwa kwa vijana na kusaidia kuwakwamua kiuchumi.”alisema Kimario.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Ally Msaki aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kwa kujiimarisha kupitia mafunzo hayo watakayoyapata ili kujikwamua na tatizo la ajira nchini.

“Tunataka vijana wawe mstari wa mbele katika kilimo cha kisasa ili kuendana na mazingira ya sasa na kujikwamua katika kundi la wasio na ajira nchini”.alisistiza Msaki.
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akizungumza na watendaji wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine pamoja na viongozi walioshiriki katika warsha ya uzinduzi wa Mafunzo kwa wakufunzi ya kilimo cha Kitalu Nyumba (Green House) yanayoendelea kwa siku tano katika Chuo hicho mkoani Morogoro.kushoto kwake ni Naibu waziri wa ofisi hiyo, anayeshughulikia wenye ulemavu Mhe.Stella Ikupa
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akizungumza na mtaalamu wa masuala ya kilimo cha kisasa kwa  kutumia mabwawa ya samaki (Acquculte) alipotembelea kukagua mradi huo, wa kwanza kulia ni Naibu Waziri Ofisi hiyo Mhe Stella Ikupa
 Manaibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu wakiangalia kiazilishe katika moja ya banda la maonesho la vijana walioshiriki mafunzo ya Kilimo cha kisasa cha kitalu nyumba. Katikati ni Mhe.Stella Ikupa anayeshughulikia Wenye Ulemavu na Kushoto ni Mhe.Anthony Mavunde (Kazi, Vijana na Ajira).
 Mkurugenzi wa Ajira Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Bw.Ally Msaki  akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
 Baadhi ya viongoizi wakishuhudia Naibu Waziri Ofisi ya Waziri (Wenye Ulemavu) Mhe.Stella Ikupa akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Muongozo wa masuala ya kilimo cha Kitalu Nyumba wakati wa warsha hiyo.
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akikagua biskuti zilizotengenezwa kwa kutumia nanasi ikiwa ni moja ya bidhaa zilizotengenezwa na vijana waliopewa mafunzo na SUGECO wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO Bw.Revocatus Kimario .
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akiangalia mapapai yaliyolimwa kwa njia ya kisasa katika mashamba ya SUGECO katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro.
 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akipewa maelezo na Mtaalamu wa masuala ya lishe (SUGECO) Jolenta Joseph kuhusu ukaushwaji wa viazi lishe wakati akikagua kaushio la jua (solar dryer).
 Manaibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde na Mhe.Stella Ikupa (Wenye Ulemavu) wakiangalia karatasi inayotumika kama  kifungashio cha unga unaotengenezwa kwa viazi lishe.
 Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Royal Agri.Co.ltd Bw.Jonathan Sangau akitoa maelezo kwa Manaibu Waziri kuhusiana na vifaa vinavyotumika katika  kufungia vitalu nyumba
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akimwaga zege kwa ajili ya kutengeneza vitalu nyumba kama ishara ya uzinduzi wa mradi huo. Picha na Nyamagory Omary wa PMO

No comments: