Tuesday, January 8, 2019

SIMBA KUTUMIA 'YES WE CAN' KUUJAZA UWANJA KATIKA MECHI YAO DHIDI YA JS SAOURA YA ALGERIA ,KUCHUKUA POINT 3

*Manara asema wametumwa na Rais, lazima wachukue ubingwa, wachezaji kutua kesho wakitokea Z'bar

*Asifu uwezo wa Kocha wao,agusia umuhimu wa kununua jezi kuichangia Klabu yao

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KLABU ya Soka ya Simba imesema maandalizi ya mchezo wao dhidi ya JS Saoura ya Algeria Jumamosi ya Januari 12 katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam yanakwenda vizuri ,hivyo imewataka mashabiki ,wanachama wao na wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi na uwanja utakuwa wazi kuanzia saa nne asubuhi.

Pia imesema kutokana na jukumu ambalo lipo mbele yao la kutumwa nchini kwenye mchezo huo la ligi hiyo ya mabingwa Afrika ,wameamua wachezaji wao waliopo kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar watarudi kesho kwa ajili ya mechi iliyopo mbele yao.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Msemaji wa Klabu ya Simba Hajji Manara amesema wakati wakijiandaa na mchezo huo wa Jumamosi ,mchezaji wao Eras to Nyoni amepata majeraha wakati wa mchezo dhidi ya KMKM ya Zanzibar.

Amefafanua jopo la madaktari wa Simba pamoja na madaktari wataasisi nyingine wametoa ripoti kuwa Nyoni anahitaji tiba maalum na mapumziko ya kutosha,kimsingi ni kwamba atarudi uwanjani katikati ya Februari.Kuhusu mchezo wao dhidi ya JS Saoura amesema wanakwenda kucheza na timu kubwa na kwamba lengo lao la kwanza lilikuwa ni kuingia hatua ya makundi na baada ya hapo wanafikiria malengo makubwa zaidi.

Amesema katika mipango yao ni kuhakikisha wanapata alama tisa nyumbani na uozefu unaonesha wakiwa nyumbani watanapata alama za ushindi huku akizungumzia weledi wa Kocha wao ambaye anajua mechi za Afrika.

Pia amefafanua wanatambua Rais Dk.John Magufuli amewaagiza Simba kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabibgwa Afrika na wanauhakika watachukua ubingwa mwaka huu.Manara amewahimiza mashabiki wa Simba kuwahi kufika uwanjani mapema badala ya kwenda uwanjani saa nane au saa tisa mchana na kwamba siku hiyo kutakuwa na burudani ya muziki kutoka bendi ya African Stars'Twanga Pepeta'.

Amesema wamezindua kampeni maalum ya kuhamasisha Wana Simba kuujaza uwanja huo kwa kutumia kauli mbiu ya Yes We Can na wanaamini hakuna kitakachoshindikana kwani Simba ni nguvu moja.Wakati huo huo amewahimiza wana Simba wakaichangia Klabu yao kwa kununua jezi na kuingia uwanjani kwa wingi,wakifanya hivyo hakutakuwa na sababu ya kupitisha bakuli kuchangishana fedha.

"Tunahamasisha Wana-Simba kununua jezi za timu yao kwa kufanya hivyo watakuwa wamechangia Klabu yao na hilo ni jambo la heshima.

"Jezi zetu zinauzwa kwa utaratibu maalum na tumejipanga kuhakikisha hakuna wanaofanya hujuma katika uuzwaji wa jezi za Simba,akibainika tutawaambia Polisi wawakamate," amesema Manara.

No comments: