Friday, December 7, 2018

WAZIRI WA KILIMO ASISITIZA MAWAZIRI JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUONGEZA MSHIKAMANO SEKTA YA KILIMO

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Katikati), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina (Kushoto) na Waziri wa Kilimo, Mifugo, Maliasili na Utalii-Zanzibar Mhe Rashid Ally Juma wakiwa katika picha ya pamoja katika ukumbi wa mikutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha, Leo tarehe 7 Disemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).
Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe Christophe Bazivamo, Waziri anayeshughulikia EAC nchini Burundi Mhe Isabelle Ndahayo, Waziri wa Kilimo nchini Kenya Mhe Mwangi Kiunjuri, Katibu Mkuu wa Kilimo nchini Rwanda Ndg Musabyimana Jean Claude, Waziri wa Kilimo Sudani Kusini Mhe Onyoti Adigo Nyikwec, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Tanzania Mhe Luhaga Mpina (Mb), Waziri wa Kilimo Tanzania Mhe Japhet Hasunga (Mb), na Waziri wa Kilimo, Mifugo, Maliasili na Utalii-Zanzibar Mhe Rashid Ally Juma wakiwa katika picha ya pamoja katika ukumbi wa mikutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha, Leo tarehe 7 Disemba 2018.


Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo-Arusha

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Mhe Japhet Hasunga amewataka mawaziri wenzake wa sekta ya Kilimo kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuongeza umoja na mshikamano ili kuakisi matakwa ya jumuiya katika Uzalishaji wa bidhaa bora za Kilimo.

Waziri Hasunga ameyasema hayo Leo tarehe 7 Disemba 2018 wakati akizungumza mara baada ya kumalizika mkutano wa 12 wa Baraza la kisekta la mawaziri wa Kilimo na usalama wa chakula wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.

Mhe Hasunga alisema kuwa kadri ushirikiano mwema utakavyoendelezwa ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii itaimarisha tija na mafanikio ya soko la bidhaa katika jumuiya hiyo na dunia kwa ujumla.Aidha, amewataka watendaji wote katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza taarifa mbalimbali zinazoandikwa kwa ustadi mkubwa kwani kwa kiasi kikubwa kumekuwa na utekelezaji duni wa mipango hiyo.

Mkutano huo wa mawaziri wa sekta za Kilimo umetanguliwa na vikao vya ngazi ya wataalamu na ngazi ya makatibu wakuu vilivyoanza tarehe 3 Disemba 2018.Katika mkutano huo maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuhusu mchakato wa CAADP katika Jumuiya hususani ripoti ya taaarifa ya utekelezaji wa Azimio la Malabo na kupitisha Mkakati wa kuendeleza Sekta ya Kilimo na Chakula (REGIONAL AGRICULTURE INVESTMENT PLAN - RAIP) sambamba na Programu ya kudhibiti sumukuvu (aflatoxin prevention and control).

Maeneo mengine ni kuhusu Programu ya masuala ya afya ya mimea na wanyama (SPS programme) hususani kuhusiana na biashara za kimataifa, ushirikiano kati ya EAC na Marekani katika masula ya biashara ya mazao ya kilimo, masuala ya pembejeo hususani mbegu na viuatilifu, Chakula na Lishe Mawaziri wameridhia Mkakati na Mpango kazi wa kutekeleza masuala ya Chakula na Lishe wa Jumuiya. 

Mkakati na mpango huo utatekelezwa katika mipango na mikakati ya nchi wanachama, Kwa Tanzania kupitia mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) na miradi mingine inayoendelea, Mradi wa kuhamasisha vijana kujiajiri katika Kilimo ambapo Vijana watatu watatu kutoka nchi zote wanachama watapokea tuzo za ushindi katika kujihusisha na kilimo.

Mjadala huo pia umehusu ripoti ya mifugo na samaki katika Jumuiya ambapo Maeneo muhimu yaligusa udhibiti wa magonjwa ya wanyama yanayovuka mipaka, Mkakati wa pamoja wa usimamizi wa magonjwa yanayoambukiza wanyama na binadamu, Masuala ya uvuvi yamezingatia changamoto za uvuvi haramu na jinsi zinavyoshughulikiwa, Sera ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe kwenye maji.

Pia mkutano huo wa 12 wa Baraza la kisekta la mawaziri wa Kilimo na usalama wa chakula wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki umejadili kuhusu Utafutaji wa rasili za kutekeleza mipango na mikakati ya Jumuiya, lakini Maeneo mengine ya muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na kirusi kinachoathiri mahindi, viwavi jeshi, homa ya bonde la ufa kwa upande wa mifugo, mabadiliko ya tabia nchi na namna ya kukabiliana nayo na masuala ya umwagiliaji.

Vilevile Waziri Hasunga amesema kuwa mkutano huo umemalizika kwa mafanikio makubwa ambapo mjadala kuhusu chakula na usalama wa chakula umekuwa na tina kwani umegusa maslahi ya wananchi.

No comments: