WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA MJI WA SERIKALI
*Akuta baadhi ya wakandarasi wanasuasua, wengine wako vizuri
*Aitisha kikao cha Mawaziri, Makatibu Wakuu wote kesho saa 5 asubuhi
*Ataka leo jioni apewe taarifa ya kila taasisi inayohusika Ihumwa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali
lililoko Ihumwa na kubaini kuwa baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi
inayotarajiwa na Serikali.
Waziri
Mkuu ameamua kuitisha kikao cha Mawaziri wote na makatibu wakuu wote
kesho (Ijumaa) saa 5 asubuhi ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini.
Ametoa agizo kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Desemba 27, 2018) mara
baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Mtumba lililoko km. 17
kutoka jijini Dodoma.
“Nimekagua
maeneo yote na kukuta baadhi ya wakandarasi wanatakiwa kujenga majengo
ya wizara nne hadi tano. Sijaridhika na baadhi ya kazi, nimeitisha kikao
cha Mawaziri wote kesho ili tuangalie ni mkandarasi yupi anaweza kumudu
hii kazi.”
“Nimebaini
kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama kokoto,
nondo, matofali na kikao cha kesho kitahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu,
viongozi wa Mkoa na Jiji la Dodoma, wakandarasi wote ili tukubaliane
kazi hii inaisha lini,” amesema.
Akitoa
mfano, Waziri Mkuu amesema wajasiriamali wanaotengeza matofali Dodoma
wako wengi lakini matofali tyao yako chini ya kiwango, kwa hiyo
wanatakiwa watu wa kutengeneza matofali mengi yenye uimara. “Tuna ujenzi
wa wizara 24, tunataka matofali imara siyo yale ambayo ukilishika tu,
mchanga unamomonyoka,” amesisitiza.
Akisisitiza
uharaka wa kazi hiyo, Waziri Mkuu amesema kazi hiyo ina malengo maalum
na inatakiwa ikamilike haraka sana. “Tarehe ya mwisho ya kukamilisha
ujenzi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais ilikuwa Desemba 31, mwaka huu
lakini kuna sababu zimetajwa kukwamisha ujenzi huo zikiwemo mvua na
uhaba wa kokoto,” amesema.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesifia kazi nzuri iliyofanywa kwenye Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu, Utumishi, Ujenzi, Katiba na Sheria, Maji na Elimu.
Kazi hizo zimefanywa na wakandarasi ambao ni Magereza, SUMA JKT, Wakala
wa Majengo (TBA) na Vikosi vya Ujenzi vya Mwanza na Dar es Salaam
vilivyoko chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Wakandarasi walioboronga ni JWTZ – Mzinga, National Housing na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Waziri
Mkuu amemwagiza Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la
Serikali kuhamia Dodoma, Bw. Meshack Bandawe ahakakishe anapokea taarifa
kutoka kila taasisi inayohusika na ujenzi huko Ihumwa na
akishaijumuisha, aiwasilishe kwake ifikapo leo jioni.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Godwin Kunambi
ashirikiane na Mkurugenzi wenzake wa Chamwiono kuhakikisha vijana wengi
wanapata fursa za ajira kwenye mradi huo.
“Mkurugenzi
wa Jiji wasiliana na Mkurugenzi mwenzako wa Chamwino mhakikishe vijana
na akina mama wanakuja kufanya kazi hapa. Pia itisha kikao cha waandishi
wa habari uwaeleze wananchi wako fursa zilizopo, kuanzia ufyatuaji wa
matofali, uuzaji wa nondo, kokoto na utengenezaji wa pavement blocks, hizi zote ni fursa, tuna wizara 24 na mahitaji ni makubwa,” alisisitiza.
Mapema,
akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
(Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Anthony Mavunde alisema zoezi la kusafisha
eneo la ujenzi wa mji wa Serikali lilianza Novemba 28, mwaka huu.
Alisema
wizara zote zimepata viwanja na zimeanza ujenzi isipokuwa Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) ambao bado wanasubiri kupatiwa
fedha.
Alisema
kazi ya ujenzi wa Mji wa Serikali inasimamiwa na Kamati ya Kitaifa ya
kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA,
ALHAMISI, DESEMBA 27, 2018.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma ramani ya Mji wa Serikali wakati
alipokagua Ujenzi wa mji huo, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27,
2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Afisa Mipango Miji katika jiji
la Dodoma, William Alfayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin
Kunambi na Kulia ni Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuhamishia Shughuli za
Serikali jijini Dodoma, Meshack Bandawe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Katibu wa Kikosi Kazi
cha Kuhamishia Shughuli za Serikali jijini Dodoma, Meshack Bandawe
kuhusu Ujenzi wa Mji wa Serikali wakati alipokagua Ujenzi huo, eneo la
Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua Ujenzi wa jengo Ofisi ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati
alipokagua Ujenzi wa Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa jijini
Dodoma, Desemba 27, 2018.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kazi ya kusuka nondo kwa ajili ya
nguzo za jengo la Ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati alipokagua Ujenzi wa Mji wa
Serikali, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. Kulia kwake
ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony
Mavunde.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua Ujenzi wa Msingi wa jengo la Ofisi za
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakati alipokagua Ujenzi wa
Mji wa Serikali, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment