Wednesday, December 26, 2018

Teknolojia ya mawasiliano ilivyowarahisishia wakulima upatikanaji mifuko ya PICS


Miongoni mwa vitu vilivyokuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya kilimo ni wadudu wanaobangua nafaka, pamoja na wakulima wengi kujikita katika upuliziaji dawa ya kuzuia wadudu hao bado haikuzuia wadudu kushambulia nafaka kavu kwa asilimia 100.

Kero hiyo ilisababisha wakulima kulazimika kuuza nafaka hizo kwa bei ya hasara ili mradi kukwepa usumbufu wa kupuliza dawa na wengine kuuza nafaka hizo kwa bei ya kupangiwa na wachuuzi wakihofia zitakapokaa muda mrefu zitapoteza ubora wake wa awali.

Kero hiyo iliwasumbua wakulima wengi katika nchi za Kiafrika, kabla ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Purdue cha Marekani ambacho kilifanya utafiti katika nchi za Afrika Magharibi na kisha kuanzisha teknolojia mpya ya kuhifadhi nafaka kwa kutumia mifuko maalumu ya tabaka tatu kwenye nchi ya Cameroon.

Wasomi wa chuo hicho walitengeneza mifuko hiyo maalumu ya kuhifadhi nafaka iliyopewa jina la Purdue Improved Crops Storage (PICS) ambayo ni mahususi kwa kuhifadhi nafaka kavu bila kutumia kemikali.“Tanzania teknolojia ya PICS ilianza mwaka 2014 ambapo kiwanda cha PEE PEE Tanzania Limited (TTTL) cha Tanga kilipata kibali cha kutengeneza mifuko hiyo.

“Wakati unaingia nchini, tayari mradi huo ulikuwa umeenea katika nchi za Afrika Magharibi na Mashariki ya mbali ukifanyika chini ya ufadhili wa Taasisi ya Melinda and Gates Foundation,” anasema meneja mradi wa PICS Tanzania, Ladislaus Ngingo.

MATUMIZI YA MIFUKO YA PICS

Ngingo anasema tofauti ya mifuko ya PICS na mingine ya salfeti ni kwamba ile ya PICS imetengenezwa maalumu kwa ajili ya kuhifadhia nafaka kavu bila kubanguliwa na wadudu kwa zaidi ya miezi sita na mkulima hatohitaji kupulizia dawa nafaka atakazohifadhi kwenye mifuko hiyo.

“Katika kipindi chote hicho nafaka zitaendelea kubaki katika ubora ule ule kama kwamba ndiyo zimetolewa shambani muda huo, mifuko hii ina nailoni mbili ndani ambazo ni nzito kila moja ina ‘macron’ 80 ambazo zina upekee katika kuhifadhi nafaka kavu,” anasema Ngingo.


Familiya kijijini Mnenia, Wilayani Kondoa ikitoa ushuhuda wa usalama wa mahindi yao. Yalihifadhiwa miaka miwili, na mifuko ya PICS.


TEKNOLOJIA YA MAWASILIANO ILIVYORAHISISHA UPATIKANAJI PICS

Mbali na wasomi wa Purdue kubuni teknolojia ya uhifadhi nafaka, watengenezaji wa mifuko hiyo nchini wamebuni njia rahisi ya kuwarahisishia wakulima kupatikana kirahisi mifuko hiyo kote nchini.

Meneja Masoko wa PICS Tanzania, Thompson Mwakibinga anasema wamewarahisishia wakulima kwa kushirikiana na mitandao ya simu za mkononi ya Tigo na Airtel.“Unaweza kupata mifuko ya PICS au taarifa kuhusu mifuko hii kwa kubonyeza nyota 149 nyota 26 nyota 5 reli kisha unabonyeza kitufe cha kupiga simu ambapo itakuletea njia mbili za kuchagua, kwanza ni kutafuta wauzaji na nyingine ni kupata taarifa za PICS.

“Kama nilivyotangulia kueleza awali, teknolojia hii inawahusu watumiaji wa mitandao ya Tigo na Airtel na ukichagua kipengele cha kutafuta wauzaji, itakuletea majina na namba za simu za wauzaji wote wa mifuko ya PICS katika kila kanda nchini,” anasema Mwakibinga.

Anasema kwenye kipengele cha taarifa za PICS nako inaonyesha bei halali ya mifuko hiyo kwa wanunuzi wa rejareja na pia inamuelekeza mkulima au mtumiaji wa PICS kutambua bidhaa bandia.“Tumeamua kutumia teknolojia hii ya mawasiliano ambayo ni rahisi na inatumika kila sehemu ambapo sasa itamuelekeza moja kwa moja mkulima mahali ambapo wakala halisi wa mifuko yetu anapatikana katika mkoa aliopo na itamuwezesha kuwasiliana naye moja kwa moja kwa kupata namba ya wakala ya mkononi akiwa hata shambani,” anasema.

Anasema, kila mfuko mmoja wa PICS unaouzwa kwa Sh 5000 kwa bei ya rejareja una ujazo wa kilogramu 100 ambapo kwa kama Mkulima atakuwa na matumizi ya kawaida anaweza kuutumia kuhifadhia nafaka kavu kwa miaka mitatu.

Ndg Ngingo(Meneja wa Mradi PPTL/ PICS) dukani Planet Commercial Agent & Vet Service, Wilayani Manyoni, Mkoani Singida.


MAWAKALA, WAKULIMA WAELEZA FAIDA ZA PICS

Magdalena Sendasenda ni wakala wa mifuko ya PICS katika kanda ya kati, yeye anasema mbali na kuuza ni miongoni mwa watu waliokwishaitumia katika kuhifadhi nafaka.“Aliyeiita mifuko ya PICS kuwa ni Kinga Njaa wala hakukosea, wakulima wa kanda ya kati (mikoa ya Dodoma na Singida) wanaichangamkia, wanaiona kama mkombozi wao katika kuhifadhi nafaka,” anasema Magdalena.

Wakala Mkuu wa mkoa wa Shinyanga (Shinyanga farm), Adam James anasema mapokeo ya mifuko ya PICS kwa wakulima wa Shinyanga na mikoa jirani ya Tabora na Mwanza ni kubwa na kwa siku wana wastani wa kuuza hadi mifuko 50 mpaka 60 katika mkoa wa Shinyanga pekee.

“Kipindi hiki kidogo upepo sio mzuri hivyo mahindi yaliyovunwa sio mengi sana ndiyo sababu tunauza idadi hiyo, lakini upepo wa kilimo ukichanganya tuna uwezo wa kuuza hadi mifuko 500 kwa siku,” anasema.Helena Magere ambaye ni kulima wa maharagwe na mahindi mkoani Tabora anasema amekuwa mdau mkubwa wa mifuko hiyo tangu 2015 alipoikuta kwenye maonyesho ya Nane nane mwaka huo.

Anasema mwanzo hakuwa na Imani na mifuko, alichukua ili kufanya majaribio na sasa ndiye mkombozi wake mkubwa katika uhifadhi wa nafaka na hana presha ya mazao yake kuharibika hata baada ya msimu kupita.

Mkulima mwingine, Bwire Shija wa Lamadi yeye anaifahamu mifuko ya PICS kwa jina la Kinga njaa, ambayo anasema ujio wake nchini umewasaidia sio tu kuhifadhi nafaka kavu bali pia kuuza mazao yao kwa bei ile ile tofauti na awali ambapo walilazimika kuuza kwa bei ya chini ili zisiwadodee na kuharibka.


MAJARIBIO YALIFANYIKA KWENYE VIJIJI 4000


Meneja mradi wa PICS Tanzania, Ladislaus Ngingo anasema kabla ya kusambaza mifuko hiyo walifanya ‘Demo’ ya matumizi kwenye Vijiji 4000 katika mikoa tisa nchini“Tulipata ushirikiano kwenye Serikali za vijiji, uliitishwa mkutano wa kijiji ambapo tulitoa kila kijiji mfuko mitano ambayo iliwekewa nafaka za kuonyeshea mfano, mmoja wa wanakijiji alielekezwa namna ya kuhifadhi ndani ya mifuko na wengine wakishuhudia.

“Alipomaliza kuhifadhi kwa pamoja tuliandika tarehe ya siku ambayo nafaka kavu zimehifadhiwa juu ya mfuko na kuyahifadhi yale magunia yenye nafaka kwa wanakijiji, baada ya miezi sita tulikwenda tena kijijini na tulihitisha mkutano kwa ajili ya kufungua zile nafaka hakuna aliyeamini nafaka zilkuwa katika ubora ule ule kama kwamba zimetoka shambani siku hiyo” anasema.

No comments: