Thursday, December 6, 2018

WADAU WATAKIWA KUTEKELEZA KANUNI MPYA ZA NGOs KUDUMISHA MISINGI YA UWAZI NA UWAJIBIKAJI




Wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kiserikali (NGOs) wametakiwa kutekeleza Kanuni Mpya za Sheria namba 24 ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Mwaka 2002 ikiwa ni lengo la kuwa na uelewa wa pamoja katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika misingi ya uwazi na uwajibikaji.

Hayo yamebainika jijini Dodoma wakati wa mahojiano kati ya waandishi wa habari na Mkurugenzi Msaidizi Usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bw. Baraka Leornard wakati wa kikao baina ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini wanaotekeleza Sera zinazosimamiwa na Wizara.

Bw. Baraka ameongeza wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wamepitishwa katika Kanuni mpya ili kuwa na uwelewa wa kutosha katika utekelezaji wa Kanuni za utendaji wa mashirika hayo kwa ajili ya kutambua nini kinatakiwa kufanya na nini hakitakiwi kufanyika ili kuepuka kukinzana na Sheria, Kanuni na taratibu husika.

Amesisitiza kuwa mara baada ya kikao hicho Wadau watakuwa na uelewa mkubwa wa Kanuni hizo ambao utawasaidia kuweza kutekeleza wajibu wao bila kukiuka Kanuni zozote ambazo zinaenda na Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Mwaka 2002.

“Bado tunasisitiza uwazi na uwajibikaji kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika utoaji wa Taarifa za fedha na miradi wanayotekeleza ili kuona miradi inayoanzishwa inanufaisha wananchi zaidi ambao ndio walengwa wakuu” alisema Bw. Baraka

Kwa upande wake Msajili na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Neema Mwanga amesema kuwa Kikao hicho baina ya Wizara na Serikali kitasaidia kuweka Mipango ya pamoja katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikianisha mchango wa Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika ngazi ya Taifa, Mkoa na jamii.

Msajili huyo ameongeza kuwa Mada mbalimbali zimetolewa katika kikao hicho ikiwemo kutoka Idara ya Uhamiaji ambao wameelimisha kuhusu utoaji wa vibali vya wafanyakazi wa kigeni ambapo wafanyakazi wengi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wanatoka nje ya nchi hivyo kutakiwa kupata vibali vya kufanya kazi ndani ya nchi.

Amezitaja mada nyingine zilizotolewa kuwa ni Haki na Ustawi wa Watoto, Jinsia na Maada kutoka Shirika la Wil-Daf waliobainisha yaliyojiri katika Maadhimisho ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia kwa mwak 2018, na mada nyingine mbalimbali zilizotolewa na wadau kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja katikapata uzoefu na uelewa wa afua mbalimbali zinazoweza kutekelezwa kwa pamoja.

Naye Mratibu Msaidizi wa kutoka Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dodoma Azia Mlawa ameyasisitiza Mashirika Yasiyo ya Kiseriklai ambayo yanachukua wafanyakazi kutoka nje ya Tanzania kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za kuomba vibali vya kufanya kazi kwa wafanyakazi wao ili kuondokana na usumbufu utakaojitokeza kwa wafanyakazi na Shirika husika bila kufuata utaratibu.

Aidha Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na ulinzi wa Mazingira Bw. Boventure Mwalongo amesema kuwa wadau wanaendelea kushirkiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali na wamepokea maelekezo ya Wizara na watayatekeleza ili kuleta uwazi na uwajibikaji ambao ni nguzo pekee kati ya pande zote mbili yaani Serikali na Mahrika Yasiyo ya Kiserikali katika kutimiza majukumu yao.





Msajili na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bi. Neema Mwanga (katikati) akizungumza na wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakati wa kikao baina ya Wizara na wadau hao wanaotekeleza Sera zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kilichofanyika jijini Dodoma kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Usajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bw. Baraka Leornard na Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali BI. Tausi Mwilima. 
Wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa wakati wa kikao baina ya Wizara na wadau hao wanaotekeleza Sera zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kilichofanyika jijini Dodoma. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW 

No comments: