Friday, December 14, 2018

SERIKALI, MADHEHEBU YA DINI KUENDELEZA USHIRIKIANO

 Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hasani Musa Kabeke akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa kuchangia damu kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya BAKWATA  yaliyofanyika kimkoa jijini Mwanza.
 Mgeni rasmi wa zoezi la kuchangia damu kwa waumini wa dini ya kiislamu jijini Mwanza, Mratibu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Kanda ya Ziwa Abel Ntahorutoba akizungumza kwenye zoezi hilo wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya BAKWATA.
 Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza na Mratibu wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Abel Ntahorutoba (kushoto) wakichangia damu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.
 Katibu Muhtasi wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza aliyehamika kwa jina moja la Sikitu akichangia damu siku ya maadhimisho ya miaka 50 ya BAKWATA mkoani hapa. Wa kwanza kulia ni Katibu wa JUWAKITA Dotto Mangu.
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza Nurdin Mbaji akisiriki kuchagia damu kwenye maaadhimish ya miaka 50 ya baraza hilo.
Waumini wanawake wa dini hakuwa nyuma katika kuchangia damu kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya BAKWATA kimkoa yaliyofanyika jijini Mwanza. 
Afisa Eimu wa Dini ya Kiislamu Abdi Musa pamoja na waumini wa dini hiyo wakichangia damu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure. Picha na Baltazar Mashaka

SERIKALI,  MADHEHEBU YA DINI KUENDELEZA USHIRIKIANO

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

SERIKALI itaendeleza ushirikiano na madhehebu yote ya dini kwa kuwa ndiyo msingi wa amani na utulivu uliopo nchini na kuwataka viongozi  wa dini waisaidie kufichua ubadhirifu wa mapato ya serikali na kuiwezesha kuleta maendeleo ya nchi kwa maslahi ya wananchi. Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dk. Severin Mathias Lalika kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela,kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza Kuu la WaislamuTanzania (BAKWATA) yaliyofanyika kimkoa jijini humu.

“Tunaamini madhehebu ya dini ni msingi wa amani na utulivu wa nchi yetu, hivyo tutaendelea kushirikiana  kwa sababu viongozi wa kiroho mmeshikilia roho zetu hata mkitangulia kusema jambo letu la serikali linakubalika kwa haraka kwenye jamii,”alisema Mongela. Alisema Yesu na Mtume Muhhamad hakuna mahali hawakuhubiri upendo kwa matendo, amani na utulivu ambavyo kuwepo kwake ndio maendeleo na kutoa wito kwa viongozi wa dini waendelee kuisaidia serikali kuhubiri amani kwenye nyumba za ibada kwani hata katiba na sheria zilizotungwa msingi wake ni vitabu vya dini.

Alieleza kuwa taasisi mbalimbali za dini kushirikiana kuadhimisha miaka 50 ya BAKWATA mkoani Mwanza iwe chachu ya kupiga vita ya kiimani kati ya madhehebu ya Kiislamu na Kikrito ikizingatiwa ni watoto wa baba mmoja (Ibrahim), hivyo wakielewa hilo hakuna sababu ya kukosana. Mongela alisema serikali haijawahi kuwa na nia mbaya na wananchi wake lakini zipo changamoto zinazokwamisha maendeleo nazo ni dawa za kulevya, mimba za utotoni na VVU, hivyo viongozi wa dini shughuli zao za kiroho wanazofanya wayahubiri hayo.

“Sheria zinazotungwa na bunge na halmashauri zinatungwa wananchi wapate maendeleo ya pamoja.Penye changamoto na pasipoeleweka tuiteni tuje kufafanua.Pia nafahamu mnapenda sana Rais John Magufuli,mpendeni zaidi tupate maendeleo zaidi ya haya ya miaka mitatu maana hatukuwa na ndoto ya kujenga reli ya umeme,”alisema mkuu huyo wa mkoa. Alihimiza kuwajenga na kuwaimarisha vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa kwa kushirikiana na serikali na kutoruhusu maadui wa nje wanaokwamisha maendeleo.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hassan Musa Kabeke alisema BAKWATA imedhamiria kuleta mabadiliko kwa kudai na kukusanya mali za waislamu pamoja na kuwaunganisha bila kujali taasisi zao. Alisema katika uongozi wake mkoani humu ataunda baraza la wazee litakalokuwa chini ya BAKWATA, pia uhakiki wa vyeti vya ndoa utafanyika sambamba na kuwasajili wafungishaji wa ndoa wawe na leseni badala ya kutumia watu holela.

Aidha, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza Askofu Charles Sekelwa pamoja na Katibu Mwenza wa kamati hiyo Askofu Zenobius Isaya walisema ni fahari kuona waislamu na wakristo wakishirikiana pamoja. “Mwanzo tulikuwa maadui hata kutembeleana ilikuwa taabu sana,kumbe ulikuwa ujinga.Niwapongeze BAKWATA kwa kutimiza miaka 50 na kutembea kwa taasisi si jmbo rahisi na kuna changamoto nyingi.Hadi kufikia hapa viongozi walivumilia, kuna kudharauliana hivyo lazima tumshukuru Mungu,” alisema na kuongeza kuwa;

“Jambo la busara kwa binadamu ni kutazama mbele na si kurudi nyuma na kiongozi hapaswi kuangalia cangamoto za pembeni yake, hivyo tumwombee Mufti Abubakar Zuberi alipeleke jahazi la BAKWATA kule Mwenyezi Mungu alikokusudia.” Askofu Isaya yeye alisema akili na upeo wa kusimama kwa BAKWATA kumetokana uongozi wa mtu mwenye na maono ya baraza hilo kuhakikisha linakuwa kwa kiwango pamoja na taasisi zake.

No comments: