Wednesday, December 12, 2018

RAIA WA MSUMBIJI AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii. 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kitengo cha makosa ya rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam, imemuhukumu Mwanamke mmoja Ana Moisie Chissano (36)raia wa Msumbiji kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia katika shtaka la kukutwa na Kg 3.03 za dawa za kulevya aina ya cocaine Hydrochloride.

Mshtakiwa aliyekuwa amefunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi namba 6/2016 amefungwa chini ya kifungu cha sheria cha 15(1)(b) cha sheria namba 5 ya 2015 cha sheria Kuzuia na kusababisha na kupambana na dawa za kulevya. 

Hukumu hiyo imesomwa leo Desemba 12.2018 na Jaji Lilian Mashaka baada upande wa mashtaka kuweza kuthibitisha mashtaka hayo pasipo Kuacha shaka baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao.

Aidha Mahakama Imeamuru dawa hizo za kulevya kuteketezwa kwa utaratibu unaostahili.Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Lilian Mashaka amesema ametoa adhabu hiyo kulingana na kifungu cha sheria namba 15 (1) (b) cha Sheria namba 5 ya 2015 ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.

Jaji Mashaka amesema sheria hiyo inaelekeza mtu yoyote anayejihusisha na dawa za kulevya anapopatikana na hatia anapaswa kutumikia kifungo cha maisha jela."Nimezingatia sababu zilizotolewa na mshitakiwa, lakini mahakama pia imezingatia sheria ambayo imeweka adhabu kwa mtu kupitia kifungu hicho inayosema mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa makosa ya dawa za kulevya basi adhabu yake ni jela maisha.

"Kwa mamlaka hayo, nakuhukumu wewe Ana Moisie Chissano kutumikia kifungo cha maisha kwa kosa ulilolitenda na iwapo haujaridhika na maamuzi una haki ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani," amesema Jaji Lilian.

Pia amesema dawa za kulevya ni tatizo linaloikabili jamii hivyo kwa njia yoyote yanapaswa kuzuiwa na jitihada za pamoja zinatakiwa zitekelezwe ili kupunguza tatizo ikiwemo kuwaadhibu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Kabla ya kutolewa adhabu, Jaji Lilian aliuliza upande wa mashitaka kama wanakumbukumbu zozote juu ya mshtakia, wakili Kakula alidai hawana kumbukumbu ya makosa lakini makosa hayo yamekuwa yakiongezeka na kusababisha kupotea kwa nguvu kazi kutokana na kutumia dawa za kulevya.

Hivyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa watu wote wanaojihusisha."Tunaomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa kwa sababu ni njia ya kuzuia wengine wanaotaka kujihusisha na vitendo hivyo," alidai Kakula.

Naye, Mshitakiwa kupitia Wakili wake, Hassan Ruwhanya aliiomba mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa kwa sababu ni kosa lake la kwanza na kwamba anategemewa na familia kwa kuwa ana watoto wawili wadogo.

"Tunaomba mahakama izingatie kutoa adhabu nyepesi kwa sababu tangu mshitakiwa afikishwe mahakamani amekaa mahabusu miaka mitatu na ameonesha kujutia kosa lake na amejifunza," amedai wakili huyo.

Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa serikali Mkuu Paul Kadushi akisaidiana na wakili wa serikali, Constantine Kakula na Batlida Mushi walidai kuwa mshitakiwa aliwasili nchini Novemba 16,2016 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na ndege ya Shirika la Ethiopia E 827 akitokea Addis Ababa Ethiopia.

Kadushi alidai kabla ya kufika maofisa wa polisi walikuwa na taarifa kwamba mshitakiwa huyo atawasili na ndege hiyo na atakuwa amebeba dawa za kulevya.

Alidai mshitakiwa huyo alikamatwa na alivyopekuliwa kwenye begi lake alikutwa na bahasha na ndani yake kulikuwa na unga uzaniwao kuwa ni dawa za kulevya.

Pia alidai baada ya unga huo kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali alithibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye uzito wa kilogramu 3.03.

No comments: