Sunday, December 2, 2018

OPERESHENI YA UVUVI HARAMU YAPAISHA MAPATO SERIKALI KUU, SAMAKI WAONGEZEKA



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelezo ya tathmini ya kitaifa ya operesheni sangara awamu ya III, mwaka 2018 kanda ya Ziwa Victoria kwa washiriki wa operesheni hiyo (hawapo pichani).
Afisa Mfawidhi kanda ya Ziwa Victoria Bw. Didas Mtambalike akisoma tathmini ya kitaifa ya operesheni sangara awamu ya III, mwaka 2018 katika kanda hiyo, kwa washiriki wa kikao kilichoongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.

Baadhi ya washiriki wa operesheni sangara awamu ya III, mwaka 2018 wakifuatilia maelezo ya tathmini ya operesheni hiyo ilivyokuwa ikitolewa katika kikao hicho.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi washiriki wa operesheni sangara awamu ya III, Mwaka 2018 katika Kanda ya Ziwa Victoria.


……………………


“Operesheni uvuvi haramu yapaisha mapato ya serikali kuu”

Operesheni za kudhibiti uvuvi haramu hapa nchini, zimeiwezesha serikali kuu kupata mrabaha wa Shilingi Bilioni 2.2 kuanzia Mwezi Desemba mwaka 2017 hadi Mwezi Novemba mwaka 2018, kutoka Shilingi Milioni 457.

Hayo yalibainishwa (01.12.2018) Jumamosi jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akiongoza kikao cha kufanya tathmini ya operesheni sangara kitaifa awamu ya tatu kwa mwaka 2018, kanda ya Ziwa Victoria, kikao kilichohudhuriwa na maafisa waliohusika katika operesheni hiyo, ambapo amesema kiasi hicho cha pesa kimeongezeka kutokana na mafanikio ya udhibiti wa mianya ya utoroshaji fedha.

“Mwaka 2017 mpaka tunafunga mwaka mwezi Desemba mrabaha wa serikali kuu kabla ya kufanya operesheni ulikuwa Shilingi Milioni 457, mwaka 2018 hadi Mwezi Novemba mrabaha wa serikali kuu ni Shilingi Bilioni 2.290, kutoka Shilingi Milioni 457 mpaka Shilingi Bilioni 2.290 unaweza kuona kwamba ni ongezeko la zaidi ya asilimia 200, hii maana yake kulikuwa na utoroshaji mkubwa wa fedha ambazo zingeingia katika mfumo mkuu wa serikali.” Alisema Mhe. Ulega.

Aidha, katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na baadhi ya wafanyabiashara wa samaki, Mhe. Ulega alisema kabla ya kuanza kwa operesheni za kudhibiti uvuvi haramu, takwimu zilionesha uwepo wa samaki wachanga zaidi ya Asilimia Tisini, lakini baada ya operesheni hizo samaki walianza kuongezeka kauli iliyoungwa mkono na wafanyabiashara waliohudhuria kikao hicho ambao walisema samaki wakubwa wameanza kupatikana kwa wingi katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Awali katika kikao hicho, akiwasilisha taarifa ya operesheni sangara kitaifa awamu ya tatu mwaka 2018 katika ukanda wa Ziwa Victoria, Afisa Mfawidhi wa kanda hiyo Bw. Didas Mtambalike alisema tangu kuanza kwa operesheni hiyo tarehe 18 Mwezi Oktoba Mwaka 2018 hadi tarehe Moja Mwezi Desemba Mwaka 2018 Shilingi Bilioni 1.172 zilipatikana kutokana na malipo ya faini walizotozwa waliojihusisha na mtukio ya uvuvi haramu.

Bw. Mtambalike pia alisema zoezi hilo limewezesha vyombo vingi vya uvuvi na biashara za bidhaa za uvuvi kusajiliwa na kupatiwa leseni kutokana na elimu ambayo wavuvi walikuwa wakipatiwa ili kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

“Kitu ambacho tumekibaini ni kwamba vyombo vingi sasa hivi vimesajiliwa vile vya uvuvi, vile ambavyo viko chini ya halmashauri vimesajiliwa lakini pia vile ambavyo viko chini ya serikali kuu vimesajiliwa ambavyo ni zaidi ya urefu wa mita 11.” Alisema Bw. Mtambalike

Baadhi ya wadau wa uvuvi ambao walipata nafasi ya kutoa maoni yao katika kikao hicho, walimuomba Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, uwepo wa bei elekezi kwa mazao ya samaki ili wavuvi waweze kuuza samaki kwa bei ya uhakika, pamoja na kulifanyia kazi ombi lao la kuendelea kuvua dagaa kwa kutumia taa zinazotumia mwanga wa jua kutokana na kusitishwa kwa ya taa hizo kwa shughuliza uvuvi hususana wa dagaa kutokana na uwepo wa madai ya samaki hao kuathiriwa na taa hizo, jambo ambalo Mhe. Ulega alisema serikali inalifanyia kazi.

Kikao cha tathmini ya operesheni sangara kitaifa awamu ya tatu mwaka 2018 katika kanda ya Ziwa Victoria kiliongozwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, ambapo kimefanya tathmini ya kutokomeza uvuvi haramu katika maeneo ya Singida, Sengerema, Ukerewe, Simiyu, Mwanza, Kagera, Geita na Mara ambayo yote yapo chini ya kanda ya Ziwa Victoria, ambapo kikao hivcho kimeridhishwa na mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika kudhibiti uvuvi haramu.

No comments: