Sunday, December 2, 2018

LUGOLA ATAKA MAGEREZA KUANZA KUJENGA VIWANDA VYA SAMANI VYA KISASA NCHINI, ASEMA VILIVYOPO HAVIWEZI KUTUPELEKA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (wapili kushoto), akimsikiliza Kamishna Jenerali wa Magereza, (CGP), Phaustine Kasike alipokua anamuonyesha moja ya mashine iliyoungua na moto mwezi uliopita katika Kiwanda cha Samani cha Magereza jijini Arusha, wakati Waziri huyo alipokitembelea kiwanda hicho leo, kuangalia moto ulivyokiteketeza kiwanda hicho. Lugola aliwataka viongozi wa Magereza kuanza maandalizi ya ujenzi wa viwanda vya samani vya kisasa katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Tabora ikiwa ni hatua ya kwenda na kasi na uchumi wa viwanda nchini. Kulia ni Mkuu wa Kiwanda hicho, SP Victor Ngwale.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimpa maelekezo Kamishna Jenerali wa Magereza, (CGP), Phaustine Kasike (kushoto), akiwa nje ya jengo la kiwanda cha Magereza cha samani ambacho kiliungua mwezi uliopita jijini Arusha. Lugola alikitembelea kiwanda hicho leo, kuangalia moto ulivyokiteketeza na kumtaka CGP kuanza maandalizi ya ujenzi wa viwanda vya samani vya kisasa katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Tabora ikiwa ni hatua ya kwenda na kasi ya uchumi wa viwanda nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), akimsikiliza Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha Magereza, jijini Arusha, SP Victor Ngwale (kulia), alipokua akimfafanulia jinsi kiwanda hicho kilipotekea kwa moto mwezi uliopita na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha. Lugola alikitembelea kiwanda hicho leo, kuangalia moto ulivyokiteketeza na kumtaka CGP kuanza maandalizi ya ujenzi wa viwanda vya samani vya kisasa katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Tabora ikiwa ni hatua ya kwenda na kasi ya uchumi wa viwanda nchini. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Magereza, (CGP), Phaustine Kasike.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akimuaga Kamishna Jenerali wa Magereza, (CGP), Phaustine Kasike mara baada ya kumaliza ziara yake ya kukitembelea Kiwanda cha Magereza cha samani kilichoungua mwezi uliopita na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha. Lugola aliwataka viongozi wa Magereza kuanza maandalizi ya ujenzi wa viwanda vya samani vya kisasa katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Tabora ikiwa ni hatua ya kwenda na kasi na uchumi wa viwanda nchini. Kulia ni Mkuu wa Kiwanda hicho. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 


Na Felix Mwagara (MOHA), Arusha 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelitaka Jeshi la Magereza lianze maandalizi ya ujenzi wa viwanda vya samani vya kisasa kwa kuwa vilivyopo havina hadhi ya kwenda na kasi ya uchumi wa viwanda nchini. 

Alisema Viwanda vya Samani cha Ukonga, jijini Dar es Salaam, cha Arusha pamoja na cha Uyui Mkoani Tabora, havina hadhi ya kuitwa viwanda vya kisasa kutokana na uzalishaji wake kuwa mdogo na pia ukubwa wa viwanda hivyo ni mdogo. 

Akizungumza leo akiwa katika Kiwanda cha Samani cha Magereza kilichoungua moto mwezi uliopita eneo la Unga Limited, jijini humo, Lugola alisema kiwanda hicho kilichoungua hakuna haja ya kukijenga kingine katika eneo hilo kwa kuwa kiwanda hicho ni kidogo, hivyo maandalizi ya ujenzi wa kiwanda kipya cha kisasa uanze kuanzia sasa. Alielekeza kuwa, kwa kuwa eneo hilo ni dogo, linatakiwa liboreshwe kwa ajili ya kuhifadhiwa samani ambavyo zitakua zimetengenewa katika kiwanda cha kisasa kitakachojengwa jijini humo. 

“Kamishna Jenerali wa Magereza, aanzeni maandalizi ya ujenzi wa kiwanda kingine ambacho kitakua cha kisasa, hili eneo ni dogo mno, na pia hata cha kule Ukonga Dar es Salaam, eneo lake ni dogo, tafadhali anzeni kufikiria kwa upana zaidi kuanza maandalizi ya kutengeneza viwanda hivyo vya kisasa,” alisema Lugola. Lugola aliongeza kuwa, Jeshi la Magereza lina maeneo mengi nchini ya kuweza kujenga viwanda hivyo ambavyo vitaenda kuongeza kasi ya uchumi wa viwanda nchini ambao aliutangaza Rais Dk. John Magufuli katika mipango ya maendeleo ya nchi. 

“Tuongeze kasi kwa kuanza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kisasa, nyie mmeshakua wazoefu, eneo hili litatufanya tuwe na ufinyu wa mawazo kwasababu hata nusu eka halifiki, hili eneo ni dogo mno, na pia mkijenga kiwanda kikubwa mtaweza kutenganisha pia fenicha za chuma na fenicha za mbao katika kiwanda hicho, mnauwezo sana Magereza wa kutengeneza fenicha za kisasa zaidi na kwa wingi,” alisema Lugola. 

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Phaustine Kasike, alisema amepokea maelekezo hayo na atakaa na viongozi wenzake kuyafanyia kazi kwa kuwa Jeshi lake lina maeneo ya kujenga viwanda nchini. “Tumepokea maelekezo yako mheshimiwa Waziri, tunaahidi tutayafanyia kazi ipasavyo na pia tunakushukuru kwa kuja kututembelea na umefanikiwa kukiona kiwanda hiki kilichoungua na kutusababishia hasara ya mamilioni ya fedha” alisema CGP Kasike. 

Kiwanda hicho kiliteketea moto usiku wa kuamkia Novemba 17, 2018 na kusababisha hasara ya zaidi ya milioni nane kutokana na mashine mbalimbali, mbao pamoja na nyaraka zilizopo katika kiwanda hicho ziliteketea moto.

No comments: