Tuesday, December 4, 2018

MICHAEL WAMBURA ARIPOTI TFF NA BARUA YA MAHAKAMA

Baada ya Mahakama Kuu kumrejesha kwenye nafasi yake ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Michael Wambura Novemba 30, leo amewasili ofisini hapo kuripoti kwa mujibu wa Mahakama Kuu.

Wambura amesema kuwa majukumu yake aliyopewa na Mahakama Kuu ameyatekeleza hivyo kwa sasa yeye ni Makamu wa Rais wa TFF kwa kuwa hakufutwa cheo chake bali alifungiwa kutojihusisha na masuala ya soka. 

"Ofisini wengi nimekuta hawapo zaidi ya mkurugeni wa fedha, na wahudumu wengine wa chini, ila kikubwa nimeweza kutimiza masharti ya Mahakama ambayo kwanza ni kuripoti ofisini, pili naleta taarifa ya mahakama ambayo imepokelewa na nimeweza kufika, kama utekelezaji hautafanyika basi nitarejea mahakamani. 

"30 Novemba nilianza kazi baada ya mahakama kuu ilipotoa maagizo, cha msingi ni kwamba nilikuja kutoa taarifa kwamba mimi nipo, walinisimamisha kujihusisha na soka ila hawakufuta cheo changu cha umakamu wa rais," alisema. 

Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtuhumu kwa makosa matatu. Katika taarifa yake, TFF ilisema kwamba ilichukuwa hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 

Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye Kamati hiyo kwa tuhuma za makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi barua na kushusha hadhi ya TFF. 

Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF iliyodai baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura ilionekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili. ”Nimefika hapa na barua yangu ambayo ilitolewa na mahakama na kutumwa TFF kuwa nirudishwe kazini na imepokelewa TFF na ikasainiwa kwahiyo leo nimekuja na itambulike kuwa nimeshaanza kazi tangu Novemba 30 siku ambayo uamzi wa mahakama ulitolewa”, amesema Wambura. 

Hata hivyo Wambura amesema licha ya kutowakuta viongozi wa juu, lakini yeye atafanya kazi kama kawaida kwasababu hakufungiwa kuwa makamu wa Rais bali alifungiwa kujihusisha na soka na uamzi huo umetenguliwa kwahiyo yupo huru kuendelea na nafasi yake. Aidha amesisitiza kuwa endapo hawatampa ushirikiano atarudi mahakamani kwenda kutoa taarifa kuwa maamuzi ya mahakama hayajatekelezwa. 

Wambura alifungiwa maisha kutojihusisha na soka, Machi 15, 2018, siku 10 kabla ya Machi 25, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilipomteua Athumani Nyamlani kukaimu nafasi hiyo ya makamu wa rais

No comments: