Monday, December 3, 2018

CCM YATOA NENO MJADALA UNAONDELEA MTANDAONI KUHUSU DK.BASHIRU NA MEMBE

*Yawataka Watanzania wakiwamo wanaCCM kupuuza uzushi, uchonganishi na fitna
*Kamati Kuu kukutana Desemba 17 na 18 Dar, yazungumzia pia ushindi wa kishindo 

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimesema kuwa kimefuatilia kwa ukaribu mjadala unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii  kuhusu wito ambao umetolewa na Katibu Mkuu wao Dk.Bashiru Ally kwa kada wa Chama hicho Benard Membe kama sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Katibu Mkuu kukutana na viongozi na wanachama wa CCM katika kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano.

Taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM Humphrey Polepole ambayo ameitoa leo Desemba 3 mwaka huu wa 2018 amesema kuwa wanatoa rai kwa rai kwa watanzania kuwa wito wa Katibu Mkuu ulikuwa ni wa kawaida wa kiongozi wa CCM kwa mwanachama wa CCM, hivyo uzushi, uchonganishi, fitina na uvumi mwingine wowote unaoendelea hasa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya magazeti yenye hila mbaya, wana CCM na Umma wa watanzania wanaombwa 
waupuuze.

"Chama Cha Mapinduzi kinawataka wana CCM na watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa na umoja, mshikamano na upendo zaidi katika kipindi hiki ambacho Rais Dk.John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anandelea kutuongoza katika mageuzi makubwa ya kiuchumi na ya kimaendeleo kwa watanzania wote,"amesema Polepole kwenye taarifa hiyo.

Wakati huohuo Polepole amesema kuwa CCM) inaujulisha umma wa wana CCM na watanzania kuhusu matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata 47 Tanzania Bara uliyofanyika tarehe 02 Desemba 2018 na kwamba CCM imepita bila kupingwa katika Kata 41 na katika Kata 6 ambako kumefanyika uchaguzi CCM imeshinda kwa kishindo.

Amesema katika chaguzi hizo ambazo CCM imeendelea kuongoza inajivunia umakini mzuri wa kufuata Taratibu, Kanuni na Sheria za Nchi yetu, Sera nzuri, ahadi zinazotekeleka na siasa safi na uongozi bora.Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuwashukuru watanzania na wanaCCM wote kwa kuendelea kukiamini na kukichagua na kwamba CCM itaendelea 
kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa haraka katika maeneo yao.

Aidha amesema Chama Desemba 17 hadi Desemba 18, 2018 jijini Dar es salaam kutakuwa na vikao vya Chama vya kawaida vya Uongozi Taifa ambapo Desemba 17, 2018 kutakuwa na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Desemba 18, 2018 Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitaketi. "Hivyo taarifa hii inawajulisha wajumbe wote wa vikao 
husika kufika katika vikao hivyo".

No comments: