Friday, December 7, 2018

Benki ya Azania Yazindua Rasmi Tawi lake Dodoma.

Benki ya Azania imezidi kujitanua baada ya hii leo kuzindua tawi lake jipya jijini Dodoma ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo katika kukuza mtatandao wa matawi yake sambamba na kuunga mkono jitihada za Mh Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, kupitia huduma bora za kibenki.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya Uzinduzi wa tawi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe alisema kwa sasa benki hiyo ina matawi kumi na tisa ikiwemo tawi hilo jipya lililopewa jina la Sokoine- Dodoma ikiwa ni ishara ya benki hiyo kutambua mchango wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine katika ustawi wa taifa kwa ujumla.

“Malengo yetu ya kimkakati kwa sasa ni kukuza mtatandao wa matawi ya benki yetu , angalau matawi matatu kwa mwaka, na pia kukuza nafasi yetu ya umiliki wa soko( Market share) angalau kwa 3% ndani ya miaka mitatu.’’ Alisema Bw Itembe. Alisema nia ya benki hiyo ni kuwa katika hadhi ya Mabenki Makubwa daraja la kwanza( Tier One ) ndani ya miaka hii mitano ya kimkakati wa kibiashara.

Akizungumzia uamuzi wa kufungua tawi hilo jijini humo, Bw Itembe alisema: “Dodoma ni katikati ya nchi, pili ni makao makuu ya shughuli za kiserikali na pia ni mkoa unaokuwa kwa kasi kibiashara.’’ Aidha, alibainisha kuwa kupandishwa hadhi kwa manispaa ya Dodoma na kuwa jiji kumeiweka benki hiyo katika nafasi nzuri kwa kuwa ukuaji wa jiji hilo unaendana sambamba na mahitaji ya kifedha.

“Katika kuunga mkono sera ya Mh Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, ni lazima kuwa na mbinu ya kuweza kukuza kipato kupitia kufanya biashara na benki zenye msingi imara… Azania Benki tupo tayari kushirikiana na wananchi na serikali katika kufanikisha hilo,’’ alisema.

Akizungumza muda mfupi kabla hajazindua rasmi tawi hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji mbali na kuipongeza menejimenti ya benki hiyo, alitoa changamoto kwa taasisi za fedha hapa nchini ikiwemo benki hiyo kuhakikisha zinajipanga kikamilifu kukabiliana na suala la mikopo chechefu sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji ili ziweze kuwahudumia wateja wake kwa gharama za chini zaidi ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.

“Chanzo cha mikopo chefu ni watumishi wasio waadirifu kwenye taasisi hizi na ndio maana naomba sana bodi na menejimenti ziwachukulie hatua sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji kwasababu sisi kama serikali hatutavumilia uzembe wa aina yoyote katika utekelezaji wa hili.’’ Alisema. Dk Kijaju alitolea mfano uamuzi wa Benki Kuu kushusha riba kwa mabenki ya biashara kutoka asilimia 16 hadi asilimia 9, kuwa unalenga kuwapunguzia mzigo wa riba wateja wa benki hizo.

Aidha Dk Kijaji alionyesha kuridhishwa zaidi na namna benki hiyo inavyotoa kipaumbele katika kuboresha sekta ya ujasirimali mdogo na wa kati hatua aliyotaja kuwa itawasaidia makundi hayo kutoa mchango mkubwa katika sekta mbalimbali , ikiwemo ya viwanda vidogo ambayo ndiyo nia ya Serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Bw Eliud Sanga alisema benki hiyo inaenda vizuri kimikakati na kiutendaji na ndio maana mwaka wa kifedha ulioisha Desemba 2017, ilifunga na faida ya Tsh 1.8 bn/- toka kwenye hasara ya shs. 6 bn/- mwaka uliopita na kuweza kutoa gawiwo la faida kwa wanahisa wake.

Ili kufanikisha shughuli za kibenki hapa nchini hasa katika mkakati wa kujenga uchumi wa viwanda Bw Sanga alishauri masuala kadhaa ikiwemo kuwekeza nguvu ya elimu katika masuala ya fedha pamoja na vigezo vya kupata mikopo kwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

“Pia kuendelea na juhudi na kwa kasi nzuri ya kuboresha miundo mbinu kama vile barabara,umeme na huduma nyingine za msingi ili wafanyabiashara hawa waweze kufanya biashara zao kwa gharama ndogo zaidi na mabenki yaweze kuvutika kuwekeza maeneo hayo.’’ Alitaja.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa tawi jipya la benki ya Azania linalofahamika kwa jina Sokoine-Dodoma wakati wa hafla fupi ya uzinduzi huoiliyofanyika jijini Dodoma leo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Bw Eliud Sanga. 
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki ya Azania Bw Eliud Sanga (wa pili kushoto) akikabidhi zawadi maalum aliyoandaliwa iliyoandaliwa kwa ajili ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (wa pili kulia) wakati wa hafla hiyo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe (kulia). 
 Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania ,  Charles Itembe akizungumza kwenye hafla hiyo. 
 Muwakilishi wa familia ya Hayati Edward Moringe Sokoine akitoa salamu za familia kwenye hafla hiyo. Tawi hilo jipya limepewa jina la Sokoine- Dodoma  ikiwa ni ishara ya benki hiyo kutambua mchango wa Waziri Mkuu wa zamani,  Hayati Edward Moringe Sokoine katika ustawi wa taifa kwa ujumla.
 Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto (kulia) akiwasili kwenye uzinduzi huo. Pamoja na mambo mengine Kamanda Muroto alizitoa hofu taasisi za kifedha jijini humo kuhusiana na suala zima la kiusalama kwa kuwa jeshi la Polisi jijini humo limejipanga kikamilifu kukabiliana na waalifu. 
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki ya Azania Bw Eliud Sanga akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (kushoto) akisaini kitabu cha wageni wakati wa hafla hiyo. Anaeshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe.
 Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Azania wakifuatilia matukio mbalimbali ikiwemo hotuba ya Naibu Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati wa hafla hiyo.
 Baadhi ya wateja na wageni waalikwa wa benki ya Azania wakifuatilia matukio mbalimbali ikiwemo hotuba ya Naibu Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati wa hafla hiyo.
 Muonekano wa ndani wa Tawi la benki ya Azania jijini Dodoma linalofahamika kwa jina la Sokoine-Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wafanyakazi wa benki ya Azania mara baada ya kuzindua rasmi tawi hilo jipya.
Burudani ya ngoma kutoka kwa kikundi cha Mwinamila ikiwaburudisha wageni waalikwa pamoja na wafanyakazi wa benki ya Azania wakati wa uzinduzi wa tawi hilo.



No comments: