Thursday, November 29, 2018

WAZIRI UMMY AAGIZA HOSPITALI ZOTE ZA RUFAA ZA MIKOA KUTOA MATIBABU YA KINYWA NA MENO.

Na WAMJW - MARA.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya kuhakikisha kuwa kabla ya March 30, 2019 Hospitali zote za Mikoa kutoa Huduma za matibabu ya kinywa.

Ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Madaktari wa Kinywa wenye lengo la kujadili njia bora za kuboresha huduma za Afya ya kinywa na meno na namna ya kuikuza kada hiyo, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Waziri Ummy alisema kuwa "hatuwezi kusema kuwa Afya ya kinywa na meno ni muhimu alafu leo ni Hospitali za rufaa za Mikoa 10 kati ya 28 ndio zinavitendea kazi" alisema Waziri Ummy.Pia Waziri Ummy aliwahasa Wananchi kupambana dhidi ya magonjwa ya kinywa na meno kwa kujiepusha matumizi ya sigara, tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari.

"Magonjwa ya kinywa na meno yana visababishi vyake ikiwemo uvutaji wa sigara,sigara, tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye Sukari" alisema Waziri Ummy.Kwa upande mwingine Mhe. Ummy amewataka madaktari wa kinywa na meno kuwahamasisha wananchi ili kufahamu umuhimu wa kupiga mswaki japo mara mbili kwa siku ili kujiepusha katika hatari yakupata magonjwa ya kinywa na meno.

"Mnatuambia kwamba angalau tupige mswaki mara mbili kwa siku, hapo mnakazi kubwa sana ya kutushawishi, hivyo niwaombe tushirikiane nasi ili kuhakikisha kwamba tunaongeza elimu na hamasa kwa jamii katika suala hiki" alisema Waziri Ummy.

Akiwasilisha taarifa mbele ya mgeni rasmi, Rais wa chama cha Madaktari wa kinywa na meno Tanzania Dkt. Mwakitobe amesema kuwa idadi ya Wataalamu wa Afya ya kinywa na meno bado ni ndogo sana ukilinganisha uwiano wa watoa huduma na wagonjwa hali inayopunguza ufanisi kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.

"Idadi ya Wataalamu wa Afya ya kinywa na meno bado ni ndogo sana ukilinganisha uwiano wa watoa huduma na wagonjwa. Wataalamu hao no pamoja na dental therapist, Madaktari wasaidizi wa kinywa na Meno, Wataalamu wa maabara wa kinywa na meno, mafundi wa vifaa na vifaa tiba vya kinywa na meno, Madaktari wa kinywa na meno na Wabobezi kwenye maeneo hayo ya kinywa na meno" alisema Dkt. Mwakitobe.

Kwa upande mwingine Dkt. Mwakitobe alisema kuwa Huduma za msingi za kinywa na meno zinahitaji ushiriki mkubwa wa kila mtaalamu wa fani hiyo ya kinywa na meno, pamoja na kundi la wauguzi wa kinywa na meno, ambapo kwa sasa nchi yetu haina chuo kinachotoa mafunzo ya fani ya kinywa na meno.

Aidha, Dkt. Mwakitobe alisema kuwa idadi ya Madaktari bingwa wa kinywa na meno bado no chache na licha ya uhaba uliopo bado hawapati kipaumbele cha kujiendeleza 

"Katika kipindi cha masomo cha mwaka 2018/2019 kipaumbele hakikutolewa kwa waombaji wanaodahiliwa katika fani za uzamili kwenye masomo ya Afya ya kinywa na meno kwani kada hiyo ni muhimu na inasaidia wananchi kama kada nyingine za Afya" alesema Dkt. Mwakitobe.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee hma Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Madaktari wa Afya ya kinywa na meno (hawapo kwenye picha) wakati akifungua mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
 Baadhi ya Madaktari na Wadau wa Afya ya kinywa na meno wakifuatilia kwa umakini hotuba ya mgeni rasmi, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa mkutano wa mwaka wa madaktari wa Afya ya kinywa na meno uliofanyika mkoa wa Mara.
 Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu baada ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa Madaktari wa Afya ya kinywa na meno uliofanyika mkoa wa Mara.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mara, wakiendelea na ukaguzi wa jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa inayoendelea kujengwa.
 Muonekano wa Jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inayoendelea kujengwa, ikiwa ni jitihada   za Serikali ya awamu ya tano kuboresha Sekta ya Afya nchini.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (aliyesimama katikati) akiteta jambo na kamati kuu ya usalama ya Mkoa iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Adam Malima wakati wa ukaguzi wa jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara inayoendelea kujengwa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee hma Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya Madaktari wa Afya ya kinywa na meno (hawapo kwenye picha) wakati akifungua mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

No comments: