Zaidi
ya wataalamu 600 katika sekta ya afya nchini Tanzania and kwingineko duniani wanakutana
jijini Dar es Salaam kwenye kongamano la 5 la afya (Tanzania Health Summit)
linaloanza Novemba 13(kesho). Litahitimishwa Jumatano Novemba 14. Kwa mara ya
kwanza, kongamano hili lilifanyika nchini mwaka 2014.
Kongamano la mwaka huu linakuja na fursa mbalimbali kwa wadau wote
walioko katika mfumo mzima wa afya nchini. Viongozi wa serikali, wawekezaji,
watafiti na wabunifu watakutana kujadili mada kuu kuhusu dira ya Tanzania
katika kuelekea uchumi wa viwanda. Kaulu mbiu ya mwaka huu ni, Ukuaji wa viwanda nchini Tanzania: Tathmini
ya ukuaji na jinsi ya kutatua changamoto zilizokithiri.
Waandaaji na waratibu wa kongamano hili ni TAMISEMI), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Wizara ya Afya ya Zanzibar, BAKWATA na Tume ya Kuratibu Huduma
zitolewazo na makanisa (CSSC), Tindwa Medical and Health Services na
Wasimamizi wa Hospitali za Binafsi(APHFTA).
Wataalamu wa
afya kunufaika
Kwa mara ya pili,
wataalamu wa afya nchini watakao hudhuria kongamano na watakaowasilisha
machapisho yao watapewa alama za kufuzu viwango vya kitaaluma. Hii itawasaidia
kukuza taaluma zao na kuongeza alama za ujuzi katika kile kinacho itwa Continuing Professional Development (CPD).
Kongamano la afya la Tanzania (THS)
limepewa ithibati ya kutoa alama hizo na Chuo kikuu ya tiba na sayansi
shirikishi(Muhas). Hii ni baada ya serikali, kupitia wizara ya afya, kutoa mwongozo
kwamba wataalu wa afya ni lazima watafute njia za kujiendeleza kitaaluma wawapo
makazini ili kukuza ujuzi na weledi katika taaluma zao.
Rais wa Kongamano la Afya Tanzania, Dkt Omary Chillo, amesema, “Wataalamu
wa afya wasibweteke baada ya kupata na kuanza kufanya kazi. Utaalamu huwa
unapotea taratibu na baada ya muda. Bila kuongeza ujuzi kitaaluma wataalamu
wengi wanaweza kujikuta wakibaki nyuma. Haijalishi kama wana uzoefu kiasi gani.
Kuna mabadiliko makubwa katika teknolojia za tiba na utandawazi. Kongamano hili
ni fursa pekee kwa hivi sasa kujieongezea alama kitaaluma.”
Zaidi ya taasisi 100 kushiriki, watoa
mada 40
Zaidi ya taasisi 100 zinashiriki
katika kongamano hili. Katika majukwaa yaliyoandaliwa katika ukumbi wa
kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), taasisi ya JHPIEGO itaonyesha mbinu
maalumu ya kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi usio salama hapa nchini.
Lakini pia, taarifa mbalimbali kuhusu sera za
afya na miradi ya maendeleo katika sekta ya afya zitatolewa na majukwaa ya
Wizara ya afya, Tamisemi na Wizara ya Afya ya Zanzibar.Kutakuwepo na majukwaa ya wasimamizi
wa hospitali za binafsi(APHTA), tume ya kuratibu huduma za kijamii zitolewazo
na makanisa(CSSC), Chuo Kikuu cha Mt Joseph, Hospitali ya Aga Khan na ShopsPlus.Zaidi ya machapisho 100 yatawasilishwa
na yatahusu waswala nyeti katika maendeleo ya sekta ya afya nchini. Mada kuu
sita zaitawasilishwa na watoa mada 40.
Wajumbe
kutoka mataifa mbalimbali, kitakacho zungumziwa
Wawekezaji
katika afya, mahospitali mbalimbali, wasambazaji wa vifaa vya afya na madawa,
watafiti katika nyanja ya afya, mashirika yasiyo ya kiserikali n.k,
wanategemewa kuhudhuria katika kongamano hili muhimu ambalo kwasasa linatimiza
miaka mitano baada ya kuonyesha mafanikio katika sekta ya afya.
Mazungumzo
ya hali ya juu ya kitaalamu yatatawala. Kutakuwepo na fursa za uwekezaji katika
sekta ya afya zitakazojionyesha wazi wazi katika machapisho ya kisayansi,
mijadala ya kitaaluma na maonyesho ya kibiashara (exhibitions).
Kwanini ukuaji wa sekta ya viwanda?
Kwa
miaka kadhaa sasa, sekta ya afya imekuwa ikipitia katika hatua za ukuaji hasa
tukizingatia mabadiliko yake katika ukuaji wa uchumi wa viwanda. Lakini,
hapakuwepo na jukwaa mahususi la wazi kutathmini mabadiliko hayo na namna nzuri
ukuaji huu unavyoweza kuleta tija na kujadili namna ya kuepuka hatari
zitokanazo na haya mabadiliko.
“Tunataka kutafuta changamoto
zilizopo katika sekya ya viwanda vya afya, na kuzitatua. Huu ni muda mwafaka
kwa watanzania wenyewe kubuni mbinu za kuendeleza sekta hii na ili kujenga
uwezo wa kuanzisha viwanda vya kuzalisha dawa hapa hapa nchini,’’ amesema Dkt
Chillo.Katibu wa Umoja wa wamiliki wa
Viwanda vya kuzalisha dawa nchini(TAPI), Abbas S. Mohammed, amesema, “Tanzania
iko katika nafasi nzuri ya kuanzisha viwanda vya kuzalisha dawa nchini. Na hivi
sasa bado viwanda vilivyopo havijatosheleza soko. Katika kongamano hili, mambo
kadhaa yatazungumzwa zikiwamo mbinu za kufikia malengo kama taifa.”
Dkt Ntuli A. Kapologwe, Dr
Ntuli A. Kapologwe, ambaye ni Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za
Lishe(DHSWNS)—TAMISEMI, amesema, “Sekta ya viwanda ikichukuliwa
kwa uzito mkubwa, haswa katika mutktadha wa ukuaji wa sekta ya afya italifanya
taifa letu kuwa imara zaidi na kuliwezesha hata kuwavutia watu kufanya utalii
katika maswala ya afya nchini(medical tourism).”
Mwenyekiti wa THS, Dkt Chakou
Halfani, amesema, “Katika kongamano hili,
tutajadili haya mambo kwa kina na kwa jicho la uchambuzi huru.Tuone
tumefanikiwa wapi mpaka sasa, na tunakwenda wapi. Tutafute ufumbuzi wa pamoja.”
Majadiliano haya yana maana gani kwa taifa? Mapendekezo
yatakayotolewa katika kongamano hili yatawekwa katika vitabu vya mpango kazi na
kila mchangiaji atapendekeza mambo ya muhimu ya kufanya kama suluhu ya namna
ambavyo yatasaidia katika kusaidia Tanzania kufikia uchumi wa viwanda.
Kwa
taarifa Zaidi: Barua pepe: info@ths.or.tz, admin@ths.or.tz Tovuti:
www.ths.or.tz Simu ya mkononi: +255 684 244 377 & +255 683 907 080 Simu ya
mezani: +255 22 171 555 Fax: +255 22 217 558
No comments:
Post a Comment