Monday, November 12, 2018

WAKUU WA MAGEREZA NCHINI WATAKIWA KUWA WABUNIFU UTATUZI WA NYUMBA ZA ASKARI

Na Lucas Mboje, Njombe

WAKUU wa Magereza yote nchini wametakiwa kuwa wabunifu ili kutatua changamoto ya uhaba wa makazi ya askari kwa kutumia nguvukazi ya wafungwa na rasilimali nyinginezo zilizopo katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa leo Novemba 12, 2018 na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua magereza yote ya Mkoa wa Njombe ambayo yanaendeshwa na Jeshi hilo. Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa lazima wakuu wa magereza wawe wabunifu katika kutatua tatizo hilo la uhaba wa nyumba kwani Jeshi hilo linazo fursa nyingi ikiwemo nguvu kazi ya wafungwa.

“Mkoa wa Njombe na mingineyo nchini haipo sababu ya kuwa na tatizo la uhaba wa nyumba za askari kwani kuna fursa ya kutosha ya kufyatua tofali za kuchoma kwa kuwatumia wafungwa ili kumaliza tatizo hili nchini”. Amesisitiza Jenerali Kasike. Aidha, Kamishna Jenerali Kasike amewataka mafisa na askari wote kuendelea kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni mbalimbali za uendeshaji wa Jeshi hilo.

Awali, akisoma taarifa ya Gereza la Wilaya Njombe, Mkuu wa Gereza hilo, SP. Charls Mihinga amesema kuwa tayari wameanzisha mradi wa ufyatuaji wa tofali za kuchoma katika kambi ya mdandu ili kumaliza tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi wa gereza hilo. “Katika msimu huu tumeweza kufyatua tofali kubwa zipatazo 30,000 ambazo tayari zimeshachomwa, tofali hizi zitatumika katika ujenzi wa nyumba za askari pamoja na ujenzi wa Ofisi mpya ya Mkuu wa Magereza Mkoani Njombe”. Alisema SP. Mihinga.

Pia, ameongeza kuwa malengo ya baadaye ni kuifanya kambi hiyo ya Gereza Njombe kuwa na taswira ya uzalishaji wa matofali kwa wingi kwa ajili ya kufanya biashara na hivyo kuongeza maduhuri serikalini.

Jeshi la Magereza linakabiliwa na uhaba wa nyumba za kuishi za Maafisa na askari hapa nchini, mkakati uliopo hivi sasa chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali wa Magereza ni kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatulika kwa kutumia njia ya ubunifu pamoja na fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Jeshi hilo.

 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoani Njombe Bw. Erick Shitindi akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP) Phaustine Kasike walipokutana  Mkoani Njombe alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa huo kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Njombe, leo Novemba 12,  2018.
 Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe wakimsikiliza  Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(hayupo pichani) alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya kuendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani humo.
 Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(wa kwanza kulia) akizungumza jambo alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Njombe. Wengine ni Maafisa Waandamizi wa Jeshi hilo.
 Mkuu wa Gereza Njombe, SP. Charles Mihinga(kushoto) akimtembeza Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini (CGP) Phaustine Kasike(kulia) alipotembelea gereza hilo leo Novemba 12, 2018.
 Baadhi ya Askari wa Gereza la Wilaya Njombe  wakifuatilia maelekezo katika Baraza lililoongozwa na  Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ambapo askari hao wameelezea changamoto zao kiutendaji leo Novemba 12, 2018.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa na askari wa Gereza Njombe( Picha na Jeshi la Magereza).


No comments: