Saturday, November 24, 2018

SERIKALI YARASIMISHA BANDARI BUBU NNE MKOANI TANGA










Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akipokea shukrani za Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Moa, Rambazo A. Mohamedi (wa kwanza kushoto) kwa kurasimisha bandari bubu ya Moa kuwa bandari rasmi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa bandari ya Tanga, Percival Salama

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akipokea taarifa ya utendaji kazi wa Bandari ya Tanga kutoka kwa Mkuu wa Bandari ya Tanga, Percival Salama (aliyesimama katikati) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua bandari hiyo

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akisikiliza kwa makini maelezo kuhusu upakuaji wa mafuta melini kutoka kwa Nahodha Andrew Matilya wakati wa ziara yake ya kukagua bandari ya Tanga. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Bandari ya Tanga, Percival Salama
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akipokea taarifa kuhusu bandari bubu ya Moa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Mark wakati wa ziara yake ya kukagua bandari bubu mkoani Tanga. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Bandari ya Tanga, Percival Salama


…………………………………………………………………………..


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amerasimisha bandari bubu nne mkoani Tanga kati ya bandari bubu 48 zilizopo mkoani humo wakati wa ziara yake ya kukagua bandari bubu hizo na kupata taarifa ya utendaji kazi wa bandari ya Tanga. Nditiye amerasimisha bandari bubu ya Moa iliyopo Wilayani Mkinga, Kigombe (Muheza), Kipumbwi na Mkwaja zilizopo wilayani Pangani.

Nditiye amesema kuwa amerasimisha bandari bubu hizo nne tu kati ya bandari bubu 48 zilizopo mkoani Tanga kwa kuwa zipo mbali na bandari ya Tanga, zipo mipakani na nchi za jirani, kusogeza huduma karibu na wananchi na kuiwezesha Serikali kukusanya tozo na kodi mbali mbali kwa ajli ya kutoa huduma kwa wananchi. “Naiagiza TPA kuhakikisha kuwa bandari bubu nne nilizorasimisha zinafanya kazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2019 na wahakikishe kuwa watumishi wa TPA na TRA wanakuwepo kwenye bandari hizo pamoja na ofisi zote za Serikali zinazohitajika ikwemo Jeshi la Polisi,”.

Pia ameitaka TPA kwa kushirikiana na TRA itoe elimu kwa wateja kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ya Serikali kwa kuwa kiwango cha kodi kinachotozwa ni kidogo ukilinganisha na athari wanazopata wananchi na wafanyabiashara kwa kuhatarisha maisha yao kwa kukwepa kodi na kutumia bandari bubu kupitisha mizigo na bidhaa nje ya bandari rasmi zilizopo na kupita maporini. Nditiye amesema kuwa, “tunahitaji bandari zetu zifanye kazi, wateja ni wengi na wana imani na nchi yetu kutokana na hali ya usalama iliyopo na ndio maana Serikali inapanua bandari ya Dar es Salaam na kuboresha bandari ya Tanga, tusisikilize maneno ya watu wachache wasio itakia mema nchi yetu katika ukuaji wa uchumi,”.

Nditiye amesema kuwa lengo la Serikali ni kudhibiti uwepo wa bandari bubu nchini ili kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia bandari rasmi zilizopo bila kukwepa kodi ili Serikali iweze kukusanya mapato kwa ajili ya kukuza uchumi na kuongeza pato la taifa letu. 
 

Amefafanua kuwa kodi inayotozwa na Serikali ni ndogo hivyo hamna haja ya wananchi kutumia bandari bubu kuhatarisha maisha yao kwa kusafirisha bidhaa na mizigo mbali mbali kwa njia ya magendo ambapo bidhaa nyingine zinakuwa zimepitwa na muda wa matumizi hivyo kuhatarisha afya ya watumiaji, zinakosa ubora na viwango vinavyohitajika kwa kuwa hazijakaguliwa na taasisi husika za Serikali kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Nditiye ametoa rai kwa watanzania kutoa taarifa za baadhi ya wavivu wasio waaminifu wanaohujumu uchumi kwa kujifanya wavuvi kwa kupakia, kushusha na kusafirisha bidhaa kwa njia ya magendo kwa kutumia bandari bubu.

Naye Mkuu wa Bandari ya Tanga, Percival Salama amekiri uwepo wa bandari bubu 48 mkoani Tanga ambapo amebainisha uwepo wa bandari bubu 12 Wilayani Mkinga, Tanga (20), Muheza (1) na Pangani (15). Katika hatua nyingine, Salama ameiomba Serikali kupitia kwa Nditiye kuhakikisha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi ya ukaguzi kwenye magari ya mizigo yanayokwenda nje ya nchi kutoka ukaguzi wa kwenye vituo 37 hadi vituo vitatu tu vya barabarani ili kupunguza kero na kuathiri mnyonyoro wa thamani na uchumi wa taifa letu na kushauri kuwa ukaguzi ufanyike kwenye maeneo yenye mizani ili kupunguza ucheleweshaji wa safari za magari hayo na kero kwa wafanyabiashara. Ameongeza kuwa Bandari ya Tanga ni bandari yenye kina kirefu kuanzia mita 12 hadi zaidi ya mita 20 na ina uwezo wa kuhudumia nchi saba zinazopakana na Tanzania

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Mkinga, Mkuu wa Wilaya hiyo, Yona Mark ameishukuru Serikali kwa kurasimisha Bandari bubu ya Moa iliyopo wilayani humo na wananchi wa kijiji cha Moa wametoa eneo kwa ajili ya TPA kuendesha shughuli za bandari hiyo. Pia, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Moa, Rambazo A. Mohamedi amesema kuwa wananchi wako tayari kushirikiana na Serikali ya Wilaya hiyo, Mkoa, TPA na taasisi nyingine za Serikali kuanzisha na kuendesha bandari ya Moa kwa kuwa iko umbali wa kilomita 14 tu kutoka kijijini hapo na nchi jirani ya Kenya.

Nditiye amewashakuru wananchi wa kijiji cha Moa kwa kutoa eneo lao kwa ajili ya bandari ya Moa na kuwaahidi kuwa watumishi wa TPA na TRA watakuwa Moa ifikapo mwezi Januari, 2019 na amewaomba wananchi wa kijiji hicho kuwapa ushirikiano. “Tanzania tuna eneo lenye ufukwe mrefu, kati ya vitu vinavyotupa changamoto ni kufidia ardhi, ila tunawashukuru wananchi wa Moa kwa kutoa eneo lenu ili litumike kuwa bandari,” amesema Nditiye

No comments: