Friday, November 30, 2018

Serikali Yaandaa Mtaala Utakaotumika Kuwanoa Wanasheria Wapya Katika Utumishi wa Umma


Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais; Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Mick Kiliba akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Dkt. Laurean Ndumbaro leo Jijini Dodoma wakati wa hafla ya ufunguzi wa kongamano la wadau kutoa maoni kuhusu mtaala wa mafunzo elekezi kwa wanasheria wapya kwenye Utumishi wa Umma.Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. 
Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Paul Kihwelo (PhD) akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa kongamano la wadau kutoa maoni kuhusu mtaala wa mafunzo elekezi kwa wanasheria wapya kwenye Utumishi wa Umma leo Jijini Dodoma. 
Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Paul Kihwelo (PhD) akisisitiza jambo kwa washiriki wa kongamano la wadau kutoa maoni kuhusu mtaala wa mafunzo elekezi kwa wanasheria wapya kwenye Utumishi wa Umma leo Jijini Dodoma. 
Sehemu ya washiriki wa wa kongamano la wadau kutoa maoni kuhusu mtaala wa mafunzo elekezi kwa wanasheria wapya kwenye Utumishi wa Umma leo Jijini Dodoma. 
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais; Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Mick Kiliba akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa Kongamano la wadau kutoa maoni kuhusu mtaala wa mafunzo elekezi kwa wanasheria wapya kwenye Utumishi wa Umma leo Jijini Dodoma.kulia ni Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Paul Kihwelo (PhD).

Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Chadhamiria Kuwajengea Uwezo waajiriwa wapya Serikalini wa Kada ya Sheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt . Laurean Ndumbaro wakati akifungua Kongamano la Wadau lililolenga kupitia na kutoa maoni kuhusu mtaala wa mafunzo elekezi kwa mawakili na wanasheria wa sekta ya umma, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Mick Kiliba amesema kuwa lengo ni kuwajengeauwezo wanasheria hao ili waweze kujua mifumo ya uendeshaji wa shughuli za Serikali, Uongozi na Utumishi wa Umma.

“Lengo la kuwaandaa waajiriwa wapya wa Kada ya Sheria ni kujenga utumishi uliotukuka na bora katika Kada hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu”; Alisisitiza Kiriba.Akifafanua Bw. Kiliba amesema kuwa waraka namba (5) Tano wa mwaka 2011 wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, unaoelekeza kutolewa kwa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya katika Utumishi wa Umma.

Aliongeza kuwa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kimekasimiwa madaraka ya kuandaa na kutoa mafunzo ya awali na elekezi kwa waajiriwa wote wa kada ya Sheria katika sekta ya Umma nchini.

Aidha, Kuzinduliwa kwa mtaala huo ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka Mitano wa Chuo cha IJA wa 2018/19-2022/23. Katika kuandaa mtaala huo, Chuo cha IJA kilishirikiana na Wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya Umma kama vile Mahakama ya Tanzania ya Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Jaji Paul Kihwelo (PhD) amesema kuwa mafunzo kwa mawakili na wanasheria wa sekta ya Umma yamekuwa yakitolewa bila kuwepo kwa mtaala mahususi ambapo kwa sasa ni wakati muafaka kuwa na mtaala huo.Aliongeza kuwa kwa kuzingatia waraka namba 5 uliotolewa na Ofisi ya Rais; Utumishi na Utawala Bora kila Taasisi ya Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa waajiriwa wapya wa kada ya Sheria Serikalini wanapata mafunzo elekezi kupitia katika Chuo Uongozi wa Mahakama Lushoto.


Baadhi ya Mambo ya yanayoangaziwa katika mtaala huo ni pamoja na; kuwawezesha waajiriwa wapya kuelewa namna ya kuendesha shughuli za Serikali, Utumishi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma, Kanuni na taratibu, Namna ya kufanya mawasiliano ndani ya Utumishi wa Umma, kanuni na taratibu, namna ya kufanya mawasiliano ndani ya Utumishi wa Umma,pamoja na rasilimali watu.

No comments: